Na Vincent Mpepo, Karatu

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania mstaafu, Profesa Elifas Bisanda ametoa wito kwa mamlaka za elimu kuingiza masomo ya Astronomia (anga za mbali) katika mtaala wa elimu kuanzia ngazi ya shule za msingi ili kuandaa wataalamu wa baadaye katika sekta hii mpya na inayochipukia kwa kasi.

Akizungumza katika siku ya kwanza ya mafunzo ya utalii wa anga za mbali (Astrotourism) yaliyofanyika Karatu, Arusha, Prof. Bisanda alisema utalii wa anga ni eneo jipya lenye fursa kubwa za kiuchumi kwa Tanzania na kuwaandaa wataalamu mapema kutaiwezesha nchi kunufaika ipasavyo.

“Kuanzisha masomo ya Astronomia na utalii unaohusiana nayo shuleni kutasaidia kuandaa wataalamu mahiri watakaoweza kutumia fursa hii ipasavyo,” alisema Prof. Bisanda.

Aliwahimiza washiriki wa mafunzo hayo kujiunga na Asasi ya Uhamasishaji Uhifadhi wa  Anga-giza la Tanzania unaolenga kulinda anga za usiku wenye giza totoro na kuendeleza utalii wa anga ili waanze kutekeleza kwa vitendo mafunzo waliyopata.

Kwa upande mwingine, Dkt. Noorali Jiwaji, Mhadhiri Mwandamizi wa Fizikia na mtaalamu wa Astronomia kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, alieleza masikitiko yake kuhusu kuondolewa kwa mada ya Astronomia katika mtaala mpya wa somo la Fizikia kwa Kidato cha Nne.

“Nashangaa tutawapata wapi wanafunzi wenye msingi wa astronomia wakati mtaala wenyewe umelitupa somo hili muhimu,” alisema Dkt. Jiwaji.

Kuhusiana na utalii wa anga za mbali (Astrotourism), Dkt Noorali Jiwaji amepewa tuzo la kulinda anga-giza hapa Tanzania na Chama cha Kimataifa cha Anga-giza.

Naye Nalayini Davis, Rais wa Chama cha Kimataifa cha Anga-giza kutoka New Zealand, alisema kuwa ni wakati muafaka kwa Tanzania kuanza rasmi utalii wa anga kwani ina faida ya kijiografia na hali nzuri ya hewa inayofaa kwa shughuli hiyo.

“Tanzania ina nafasi kubwa ya kuwa kinara wa utalii wa kutazama nyota barani Afrika. Ni lazima ichukue hatua sasa,” alisema Nalayini.

Mafunzo hayo utalii wa anga yameandaliwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), yameendeshwa na wataalamu kutoka New Zealand na Marekani, na kuhudhuriwa na washiriki 70 kutoka sekta binafsi na ya umma katika tasnia ya utalii wa ndani kutoka nchi mbalimbali.

Posted in

Leave a comment