Na Vincent Mpepo, Karatu

Wakristo wamekumbushwa faida na umuhimu wa kumtolea Mungu kwa uaminifu sadaka mbalimbali hususani fungu la kumi.

Ukumbusho huo umetolewa na Mwalimu wa neno la Mungu, Tumsifu Lema katika mahubiri wakati wa ibada ya kwanza katika ibada Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) leo, katika Usharika wa Karatu Mjini, Dayosisi ya Kaskazini, Jimbo la Karatu Mjini.

Alisema kuna faida nyingi za kumtolea Mungu kwa uaminifu na kuwa hakuna ambaye anamtolea Mungu kwa kumaanisha ataachwa hivyo alivyo akibanisha mojawapo ya faida ni kufunguliwa milango ya baraka.

“Mtu yeyote anayekwenda mbele za Mungu kwa uaminifu, imeahidiwa atafunguliwa milango ya baraka”, alisema Mwalimu Tumsifu.

Alianisha milango katika aina mbili ikiwemo inayoonekana naisiyoonekana na kwamba wakristo wengi wana ufahamu na milango inayoonekana zaidi ya ile isiyoonekana ambayo hutumiwa na watu wema na wabaya kutimiza malengo yao.

“Kuna milango ya kiroho ikifungwa utapata tabu sana”, alisema Mwalimu Tumsifu.

Aliongeza kuwa faida nyingine ya kuwa mwaminifu katika kumtolea Mungu sadaka ya fungui la kumi kuwa ni ulinzi dhidi ya maadui na kuinua uchumi wa mtoaji na kusisitiza kuwa kila mtu ana maadui kutokana na kitu afanyacho na wanaweza kuwa ni maadui wa mbali au wa karibu.

“Kuna watu wakikutazama wana wivu mbaya”, alisema Mwalimu Tumsifu.

Alianisha mambo muhimu ya kuzingatia katika utoaji akisisitiza kwa mtoaji kusamehe waliomkosea hata kama hawakuomba msamaha na kwamba utoaji wenye manung’uniko na lawama.

Aliwataka wakristo kuwa waangalifu na maneno au nia wawekazo wanapoenda kumtolea Mungu kwa kuwa Mungu hadhihakiwi na hujibu akitolea mfano wakristo ambao huahidi nyakati za harambee bila kutekeleza na kuwa wasikivu kwa sauti ya Mungu ndani yao.

Kwa upande wake, Mchungaji Kiongozi Usharika wa Karatu Mjini, Fanuel Sippu aliwakumbusha washarika kukamilisha michango ya sadaka kwa ajili ya Sikukuu ya Mikael na Watoto ambayo imekaribia ili kufanya siku hiyo muhimu kwao kuwa ya kuvutia.

Aidha aliwaomba kuchangia fedha kwa ajili ya ujenzi wa kanisa jipya la moja ya mtaa unaohudumiwa na Usharika huo.

Posted in

Leave a comment