
Na Vincent Mpepo, Mtwara
Wanandoa katika jamii wametakiwa kuishi kwa upendo, kusameheana na kuvumilana kwa kuwa kila mwanadamu ana udhaifu wake na hakuna mkamilifu.
Wito huo ulitolewa jana na Paroko wa Parokia ya Yesu Kristo Mkombozi – Magomeni, Jimbo Katoliki la Mtwara, Padre Silvanus Chikuyu wakati wa mahubiri katika ibada ya ndoa kati ya Edgar Joseph na Maria Danford na kusisitiza kuwa wanandoa wanapaswa kuishi kwa kuchukuliana ambako kuna msamaha, upendo na zaidi malengo mema ya kujenga familia.
Alisema kama wanandoa wana wajibu na ni mpango wa Mungu kuzaa watoto kuwalea na kuwatunza vizuri kiroho na kimwili ili kuendela kuwa na jamii inayomjua Mungu na yenye maadili mema.
“Mpango wa Mungu ni kuwa mkazae na kuijaza dunia, lakini msiishie tu kuzaa bali mkawalee watoto mtakaojaaliwa katika maadili mema”, alisema Padre Chikuyu
Aidha aliwataka ndugu na jamaa kutokuwa chanzo cha kuvunjika kwa ndoa badala yake wawe kimbilio na wasuluhishi wema ili kuifanya ndoa hiyo kudumu.
“Wakati mwingine wazazi, walezi, wifi na shemeji wamekuwa ni chanzo cha kuvunjika kwa ndoa, ninaomba ndugu na wasimamizi muwasaidie wanandoa hawa”, alisema Padre Chikuyu
Wakati wa hafla ya ndoa hiyo iliyofanyika katika Bwalo la Maafisa wa Polisi Mtwara, Mwakilishi wa familia ya Edgar Joseph, Francis Mpepo aliwataka wandoa kuishi kwa kujaliana iwe kwa shida na raha kwa kuangalia pande zote za upande wa mume na mke.


“Likitokea kwa mume, mke uwe wa kwanza kusaidia na kushauri na kwa likitokea kwa mke mume pia uhusike”, alisema Francis.
Mama wa bibi harusi, Zenapokea Makota, katika nasaa zake kwa wanandoa hao hao alimkumbusha Maria umuhimu wa kumpikia mumewe.
“Natamani usiende kununua vitumbua wala njugu kwa mama ntilie, badala yake uwe unapika mwenyewe nyumbani kwako”, alisema Bi Makota.
Kwa upande wake mwakilishi wa madereva Benedicto Tesha aliwaasa wanandoa hao kuwakimbilia wafanayakazi wenzao wakati wa shida na raha.
“Ninakuomba Edgar na mkeo Maria muwe na utayari kuwakimbilia wenzenu iwe katika shida au raha”, alisema Tesha.

Hafla ya ndoa hiyo imeshuhudiwa na kuhudhuriwa na wafanyakazi wa Idara mbalimbali za serikali kutoka Manispaa ya Mtwara ikiwemo Idara ya elimu sekondari, Idara ya fedha, Idara ya utawala na madereva kitu kinachoonesha uhusiano mzuri wa wafanyakazi katika manispaa hiyo.


Leave a comment