
Na Vincent Mpepo, Songea
Wataalamu wa afya wa Zahanati ya Kijiji cha Mlete iliyopo Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma wamepongezwa kwa moyo wao wa kujitoa na kujituma katika kuhudumia wagonjwa.
Hayo yamebainishwa na ndugu wakiwemo watoto wa marehemu Amalia Chilongo wakati wa ibada ya mazishi yake jana huku ikibainika wazi kuwa watumishi wa Zahanati hiyo walikuwa tayari kufanya kazi muda wote walipohitajika kmhudumia marehemu Amalia.
Akizungumza kwa niaba ya familia, mtoto wa marehemu Manswetus Mwimba aliwashukuru wauguzi hao ikiwa ni miongoni wanajamii aliowashukuru wakati akitoa shukrani za familia wakati wa ibada hiyo.

“Kipekee ninapenda kuwashukuru sana wataalamu wa afya wa Zahanati ya Mlete kwa namna ambavyo walijitahidi kuokoa maisha ya mama yetu hata walipohitajika muda nje ya kazi”, alisema Mwimba.
Aliwaomba waendelee na moyo huohuo kwani kufanya hivyo siyo tu kutimiza majukumu lakini pia ni baraka na matendo mema.
Aidha aliwashukuru ndugu, jamaa, marafiki na wageni wote waliofika na kuhudhuria katika safari ya mwisho ya mama yake na kuwatakia kila la kheri katika safari za kurejea makwao.
Akihubiri katika ibada hiyo, Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu, Shule ya Tanga Jimbo Kuu la Songea, Padre Soo Sai Raj aliwataka wakristo kujiandaa na kuishi maisha ya kumpendeza Mungu kwa kuwa hakuna ajuaye siku wala saa ya kuitwa kwake.

Alisema kifo siyo mwisho wa maisha na muhimu zaidi ni kumuomba Mungu awajalie imani na waishi katika kulielewa fumbo hilo huku kila mmoja akifanya maandalizi.
Marehemu Bi. Amalia Chilongo alizaliwa mwaka 1935 na alifunga ndoa takatifu 1953 Mzee Daniel Mwimba (sasa marehemu) na katika uhai wao walijaaliwa kupata watoto sita na marehemu ameacha watoto 5, wajukuu 28, vitukuu 61, na vilembwe 4.
Ibada hiyo ya mazishi ilihudumiwa na Katekista Aron Mhagama na Kwaya ya Umoja ya Kigango cha Mlete ikijumisha kwaya ya Mtakatifu Joseph na Mtakatifu Bernadeta zote za kigango hicho huku ibada hiyo ikuhudhuriwa na wageni kutoka sehemu mbaalimbali mkoani Ruvuma na nje ya mkoa.


Leave a comment