Na Damas Kalembwe

Mkuu wa Ushirikishwaji Jamii wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni, ACP Ally S. Wendo, akimwakilisha Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, SACP Mtatiro Kitinkwi, ameongoza kikao kazi na Kikundi cha Ulinzi Shirikishi cha Wilaya ya Kinondoni (USHITA), kilichofanyika katika ukumbi wa Club 361, Mwenge jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika kikao hicho, ACP Wendo alitoa wito kwa wanachama wa umoja huo kuendeleza uwajibikaji, nidhamu na mshikamano katika kutekeleza majukumu yao, akibainisha kuwa ulinzi shirikishi ni nyenzo muhimu katika kudumisha utulivu wa mijini.

“Amani ni injini ya maendeleo bila kuwa na utulivu hakuna shughuli za kiuchumi zinazoweza kufanyIka”, alisema ACP Wendo.

Aidha, aliwataka wanachama kuendeleza utamaduni wa kuchangia ada walizojiwekea ili kuimarisha uwezo wa kifedha wa umoja huo na kuweka msingi imara wa utoaji wa huduma kwa wanachama.

“Ninawaomba muendelee kuwa mabalozi wa amani katika mitaa yenu na kuendelea kushirikiana na Polisi kwa maslahi mapana ya usalama wa wananchi”, alisema ACP Wendo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa USHITA, Ndugu George, aliishukuru Polisi Mkoa wa Kinondoni kwa kujitoa mara kwa mara kutoa elimu ya ulinzi shirikishi, akieleza kuwa mwamko huo umeongeza uelewa na kuimarisha mahusiano kati ya jamii na Jeshi la Polisi.”Tunaona matokeo chanya ya elimu hii. Tunaiomba iendelee kufikishwa kwa wananchi wengi zaidi ili kujenga jamii inayowajibika, yenye uelewa wa usalama na umoja,” alisema.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa kikundi hicho, Lilygray Mwikosi, aliahidi kuwa USHITA itaendelea kuwa mshirika thabiti wa Jeshi la Polisi katika kulinda amani ya Dar es Salaam na taifa kwa ujumla.

“Amani ndiyo msingi wa ustawi wa maisha na uchumi. Tukiiweka hatarini, tunahatarisha kila hatua ya maendeleo tunayoyapa nchi yetu, alisema Lilygray.

Kikao hicho kimehitimishwa kwa makubaliano ya kuimarisha mifumo ya mawasiliano, mafunzo na uratibu kati ya Jeshi la Polisi na kikundi cha USHITA ili kukuza ufanisi wa shughuli za ulinzi shirikishi katika Mkoa wa Kinondoni.

Kikao hicho ni mwendelezo wa kuimarisha ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na vikundi vya ulinzi shirikishi, sambamba na kukuza uelewa kuhusu nafasi ya wananchi katika kulinda amani na usalama wa maeneo yao.

Kikundi cha Umoja wa Ulinzi Shirikishi Tanzania (USHITA), ni umoja wa wanachama wanaojitolea kuimarisha ulinzi wa jamii, pia hujishughulisha na mfuko wa kuchangiana kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za kifamilia na za kijamii zinazoikumba jumuiya yao.

Posted in

Leave a comment