Na Mwandishi wetu, Dodoma.

Waandishi wa habari nchini wametakiwa kuandika na kuripoti habari zinazohamasisha amani ili kuwa na taifa endelevu katika sekta mbalimbali kwa ujenzi wa nchi.

Akizungunza na waandishi wa habari zaidi ya 100 kutoka mikoa mbalimbali nchini wakati wa mafunzo maalumu kuhusu uandishi wa habari wa amani Jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Denis Londo amewataka wanahabari kuwa mstari wa mbele katika kulinda amani kupitia kazi zao za uandishi ili kupunguza au kuondoa kabisa mogogoro isiyo ya lazima.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Mhe. Denis Londo

Alisema tasnia ya habari ni wadau muhimu katika kuuhabarisha umma kuhusu masuala ya umuhimu wa jamii kupendana na kulinda amani katika kuhakikisha jamii inapata taarifa sahihi ili kuepusha migogoro na chuki.

Tunapaswa kuhamasisha amani na upendo miongoni mwa jamii zetu ili tuendelee kuwa wamoja kwa maslahi ya ulinzi na usalama wa taifa letu, alisema Londo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kanda ya Kusini mwa Afrika upande wa Tanzania (Media Institute of Southern Africa-MISA) Ndugu Edwin Soko, alisema vyombo vya habari nchini havitakubali kuchonganishwa na wananchi bali vitaendelea kusimamia maadili, uzalendo na weledi katika kutekeleza majukumu yao ya msingi ya kila siku.

Mwenyekiti wa MISA-TAN, Edwin Soko

“Jukumu letu kama wanahabari ni kutafuta, kuchakata na kusambaza habari sahihi kwa jamii”, alisema Soko.

Alisema sekta ya habari nchini imekuwa imara na inazidi kukua siku hadi siku na MISA-TANZANIA itaendelea kutoa mafunzo hayo ili kuimarisha msingi wa upatikanaji na utoaji wa taarifa sahihi kwa walaji (Jamii).

Msemaji Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, DCP David Misime aliwapongeza wanahabari nchini kwa namna wanavyoshirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama katika kutafuta na kuripoti matukio mbalimbali kwa usahihi na kuwaasa waandishi kuachana na habari za uchochezi.

Msemaji Mkuu wa Jeshi la Polisi, DCP David Misime

Kwa upande wao, waandishi wa habari Keneth Ngelesi na Elizabeth Kilindi walisema mafunzo hayo ni mwendelezo mzuri wa kujenga uelewa na kuwakumbusha misingi ya taaluma yao kwa kuzingatia sheria na maadili.

Baadhi ya washiriki wa semina hiyo ambao ni waandishi wa habari na viongozi wa taasisi mbalimbali za kidini nchini

Mafunzo hayo ya siku moja kwa waandishi wa habari yalifanyika katika Hoteli ya Morena Jijini Dodoma na kuhusisha wataalamu kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), wakufunzi wa vyuo vikuu, waandishi wa habari waandamizi na viongozi wa dini na yalipambwa na kaulimbiu  isemayo “Sasa ni wakati wa kulijenga Taifa letu”.

Posted in

Leave a comment