Na Ummy Kondo, Dodoma

Wanakikundi wa PMO LEYD wametembelea na kutoa misaada mbalimbali kwa wazee wa Kambi ya wazee Sukamahela Wilayani Manyoni, Singida.

Msaada hiyo ilitolewa na wanakikundi hao hivi karibuni ikiwa ni sehemu ya taratibu na utamaduni wa kikindi hicho ili kuyafikia makundi yenye uhitaji na kwamba watumishi, mashirika na watu binafsi wajenge utaratibu wa kuwatembelea wahitaji ili kuwapa faraja na kuondoa upweke.

Akizungumza kwa niaba ya wanakikundi wenzake, Makamu Mwenyekiti wa kikundi hicho Venerose Mtenga alisema kikundi chao kina utaratibu wa kutoa kwa jamii wenye uhitaji mbalimbali kama sehemu ya malengo ya kikundi hicho.

“Ninawashukuru sana watumishi wa kituo hiki kwa huduma zenu, rai yangu kwenu endeleeni kufanya kazi kwa weledi na upendo kwani pamoja na yote mnafanya pia kazi ya kumtukuza Mungu kupitia wazee hawa”, alisema Bi Venerose.

Aidha Afisa Ustawi wa Jamii katika kituo hicho, Lilian Bujiba alisema serikali inafanya kazi kubwa ya kuwahudumia wazee hao ambao wengi wao ni waliokimbiwa na familia na kuishi mazingira hatarishi na waliokua na ulemavu wa kudumu ikiwemo ukoma upofu na viungo.

“Ninawashukuru wanakikundi cha PMO LEYD kwa msaada wao na ninawaomba wanajamii, mashirika ya umma na serikali kuhjitokeza kuwasaidia wazee hao kwa kadri watakavyoguswa, alisema.

Mwenyekiti wa wazee hao, Andrea Mkung’huni alisema wamefurahi sana kutembelewa na wanakikundi hao na wamejisikia faraja sana na kujiona fahari kua kuna watu wanawakumbuka na kuwajali.

Kituo hicho kipo Mkoa wa Singida Wilaya ya Manyoni Kata ya Solya kijiji cha Sukamahela kina wazee 16 wanaume 9 na wanawake 7 na ni moja ya kambi inayohudumiwa na serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum.

Posted in

Leave a comment