
Na Cartace Ngajiro, Tanga
Bandari ya Tanga kwa mara ya kwanza imeandika historia baada ya kupokea Meli ya MV PARNIA yenye Makontena 463 kutoka Iran.
Akiongea mara baada ya kupokea meli hiyo Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dkt. Balozi Batilda Burian, alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa alioufanya katika bandari hiyo na matunda yake kuonekana.

Alisema ujio wa meli hiyo katika Bandari ya Tanga kutoka Iran ni fursa kwa wafanyabiashara wa Mkoa wa Tanga na Mikoa mingine kufungua fursa za kibiashara baina ya Tanzania na Iran kwa kupitishia mizigo yao katika Bandari ya Tanga.
“Nampongeza Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono makubwa ya kuwekeza katika Bandari ya Tanga na leo hii tumeandika historia kwa kupokea meli yenye makontena mengi jambo ambalo halikuwahi kutokea huko nyuma kabla ya maboresho”, alisema Balozi Burian.
Katika hatua nyingine Balozi Burian aliahidi kuendelea kujenga ushirikiano wa kibiashara na Iran kwa kutumia bandari ya Tanga ili kuhudumia nchi za Afrika Mashariki na nchi za Ukanda wa SADC.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Dadi Kolimba alisema ujio wa meli hiyo katika Bandari ya Tanga ni fahari kwa wananchi kwani uchumi wa Tanzania utazidi kukua na fursa za kibiashara zitazidi kufunguka zaidi.
Akitoa maelezo kwa Mkuu wa Mkoa, Kaimu Meneja wa Bandari ya Tanga Bw. Peter Millanzi alisema kwa muda mrefu Bandari ya Tanga imekuwa ikipokea meli ndogo ndogo ‘Feeder ‘ kutoka Bandari za na nchi jirani kwa sababu sababu ya uwezo mdogo wa kupokea meli kubwa za makontena.
Alisema kutokana na maboresho makubwa yaliyofanyika kwa sasa Bandari hiyo ina uwezo wa kupokea meli kubwa na matokeo yake ni hitoria kuandikwa kutokana na kupokea meli kubwa ya makontena kutoka moja kwa moja nchini Iran.
Meli hiyo yenye urefu wa mita 174 na kina cha mita 10.3 imetia nanga katika Bandari ya Tanga ikiwa na makontena 463 ambapo makontena 261 ni ya Tanzania na makontena 182 yanakwenda katika nchi za za Rwanda, Zambia, Malawi na Uganda.


Leave a comment