
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Profesa Alex Makulilo akizungumza na hadhara ya wafanyakazi wa chuo hicho jana Kinondoni, jijini Dar es salaam.
Na Vincent Mpepo
Uongozi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) umesisitiza dhamira yake ya kuboresha mazingira ya kazi ili kuongeza tija na kuboresha utoaji wa huduma kwa wateja.
Akizungumza katika Mkutano wa Makamu Mkuu wa Chuo na wafanyakazi uliofanyika jana Kinondoni, jijini Dar es Salaam, Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Alex Makulilo, aliwataka wafanyakazi kufanya kazi kwa bidii na weledi ili kuboresha huduma kwa wateja na kupunguza malalamiko.
Alisema huduma bora kwa mteja ni msingi wa mafanikio ya taasisi yoyote, na hivyo amewataka wafanyakazi kutilia mkazo suala hilo, vinginevyo taasisi inaweza kukumbana na malalamiko ya mara kwa mara na kupoteza wateja.
Akizungumzia maendeleo ya Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), Profesa Makulilo alisema mradi unaendelea vizuri licha ya changamoto katika baadhi ya vituo, ikiwemo kushindwa kwa baadhi ya wakandarasi kuendelea na kazi kutokana na sababu mbalimbali.
“Ufuatiliaji ulifanyika na kubaini kuwa wakandarasi hawawezi kuendelea na mradi,” alisema Profesa Makulilo.
Aliongeza kuwa taratibu zote za kisheria zilifuatwa katika kusitisha kandarasi hizo, na taratibu za kupata wakandarasi wapya zinaendelea kwa kushirikiana na wizara husika.
Vituo vya mikoa ambavyo utekelezaji wa mradi haukwenda vizuri ni Arusha, Mwanza na Kigoma, huku utekelezaji ukiendelea kwa ufanisi katika vituo vya Njombe na Mtwara.
“Kuchelewa kwa utekelezaji wa mradi kumetokana na changamoto mbalimbali za ndani na nje ya taasisi,” alifafanua Profesa Makulilo.
Aidha, alieleza kuwa uongozi umeimarisha mikakati ya kuhakikisha uendelevu wa mradi kwa kufanya uteuzi wa viongozi wapya watakaosimamia utekelezaji wake kwa ufanisi, huku akiwataka viongozi hao kutanguliza maslahi ya taasisi.
Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Huduma za Mikoa na Teknolojia za Kujifunzia, Profesa Leonard Fweja, alizungumzia uharibifu wa vituo vya Kahama na Kinondoni uliotokana na machafuko ya Oktoba 29.
Naye Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu, Profesa Saganga Kapaya, aliwashukuru wafanyakazi kwa kufanikisha mahafali ya 44 ya chuo hicho na kuwasisitiza kuendelea na moyo huo.
Akitoa taarifa kuhusu mrejesho wa mitaala kutoka Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), alisema kati ya mitaala 98 iliyowasilishwa, mitaala 21 ya marejeleo imerejeshwa na inakidhi vigezo vya ubora, huku 14 ikihitaji masahihisho madogo.
Aliwataka wakuu wa vitivo kuunda timu ndogo za kushughulikia masahihisho hayo na kuyawasilisha kwa wakati, akibainisha kuwa kazi hiyo inatakiwa kukamilika ifikapo 15/12/2025.
Wakati huohuo, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Mipango, Fedha na Utawala, Profesa Josiah Katani, aliwakumbusha wafanyakazi kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma, hususan suala la kuwahi na kuhudhuria kazini kwa wakati.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi (THTU) chuo hapo, Salatiel Chaula, aliushukuru uongozi wa chuo kwa ushirikiano wao katika kutatua changamoto za wafanyakazi, ikiwemo uboreshaji wa maslahi, na akawahimiza wafanyakazi kuendelea kujituma katika kazi.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi tawi (THTU) tawi la Chuo kikuu Huria cha Tanzania, Salatiel Chaula akisisitiza jambo wakati wa Mkutano wa Makamu Mkuu wa Chuo na wafanyakazi uliofanyika jana Kinondoni, jijini Dar es salaam. (Picha kwa hisani ya Kitengo Cha Mawasiliano na Masoko, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania).




Picha mbalimbali: Sehemu ya wafanyakazi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania wakati wa Mkutano wa Makamu Mkuu wa Chuo hicho na wafanyakazi uliofanyika jana Kinondoni, jijini Dar es salaam. (Picha kwa hisani ya Kitengo Cha Mawasiliano na Masoko, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania).

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Masoko cha Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Dkt. Adam Namamba akisoma jumbe za wafanyakazi kutoka vituo vya mikoa nje ya Dar es salaam walioshiriki Mkutano wa Makamu Mkuu wa Chuo na wafanyakazi uliofanyika jana Kinondoni, jijini Dar es salaam. (Picha kwa hisani ya Kitengo Cha Mawasiliano na Masoko, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania).
Leave a comment