
Mgeni Rasmi wa katika maadhimisho ya Siku ya Kifaransa Duniani, Afisa Elimu Kata ya Upanga Magharibi, Mwalimu Immaculata Ngure katika picha ya pamoja na meza kuu pamoja na walimu wa Kifaransa waliohudhuria katika maadhimisho hayo jana Katika Shule ya Sekondari Azania, jijini Dar es Salaam. (Picha na Vincent Mpepo).
Na Vincent Mpepo
Wadau wa lugha ya Kifaransa nchini wamekutana katika Shule ya Sekondari ya Azania kuadhimisha Siku ya Kifaransa Duniani, ikiwa ni sehemu ya kuienzi lugha hiyo adhimu na kubainisha fursa mbalimbali zinazopatikana kwa wanaojifunza Kifaransa.
Katika maadhimisho hayo yaliyofanyika jana jijini Dar es Salaam, wahadhiri, wakufunzi, walimu na wanafunzi wa lugha ya Kifaransa walisema bado kunahitajika hamasa zaidi kwa jamii ili kuongeza uelewa na mapenzi ya kujifunza lugha hiyo.
Mwenyekiti wa Chama cha Walimu wa Kifaransa Tanzania (TAFT), Dkt. Costantine Njalambaya, alisema Kifaransa si lugha ya kujifunza pekee, bali ni daraja la utamaduni, ubunifu na mshikamano linalowawezesha watu kujieleza na kuunganishwa kimataifa.

Mwenyekiti wa Chama cha Walimu wa Kifaransa Tanzania (TAFT), Dkt. Costantine Njalambaya akihutubia hadhara ya wanafunzi, wakufunzi, wahadhiri na wadau mbalimbali wa Lugha ya Kifaransa katika maadhimisho ya Lugha hiyo yaliyofanyika jana katika Shule ya Azania jijini Dar es Salaam. (Picha na Vincent Mpepo).
Alibainisha kuwa maadhimisho ya mwaka huu yenye kaulimbiu “Kuimba, Kucheza, Kufundisha: Lugha ya Kifaransa katika Muziki” yameangazia namna sanaa na michezo vinavyoweza kutumika kuboresha ufundishaji wa lugha hiyo.
Aidha, aliushukuru Ubalozi wa Ufaransa kwa msaada wa kifedha uliowezesha kufanyika kwa maadhimisho hayo, akisisitiza kuwa mchango huo umeendelea kuimarisha jitihada za chama hicho katika kukuza ufundishaji wa Kifaransa nchini.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Walimu wa Kifaransa Mkoa wa Dar es Salaam ambaye pia ni mwalimu wa Kifaransa katika Shule ya Sekondari Chang’ombe, John Daudi, alisema chama hicho kimepiga hatua kubwa, huku akishukuru serikali kwa ushirikiano inaotoa.
“Kwa mfano, mwaka jana tuliandaa Siku ya Walimu wa Kifaransa katika Kituo cha Utamaduni cha Kifaransa hapa Dar es Salaam, na mwaka huu tumefanya hapa Sekondari ya Azania,” alisema Mwalimu Daudi.
Naye Mgeni Rasmi wa maadhimisho hayo, Afisa Elimu Kata ya Upanga Magharibi, Mwalimu Immaculata Ngure, aliyemwakilisha Afisa Elimu wa Jiji la Dar es Salaam, alikipongeza chama hicho kwa juhudi za kuwaunganisha wadau wa lugha hiyo wakiwemo walimu, wakufunzi, wahadhiri na wanafunzi.

Afisa Elimu Kata ya Upanga Magharibi, Mwalimu Immaculata Ngure akihutubia washiriki wa maadhimisho ya Siku ya Walimu wa Kifaransa Duniani yaliyofanyika jana katika Shule ya Azania jijini Dar es Salaam. (Picha na Vincent Mpepo).
Alisema wakati umefika kwa serikali kuongeza idadi ya walimu wa somo la Kifaransa kutokana na umuhimu na manufaa yake kwa nchi na kwa mtu mmoja mmoja. Alisisitiza pia kuwepo kwa uhamasishaji zaidi ili watoto wawe na motisha ya kujifunza lugha hiyo.
Akizungumzia matumizi ya nyimbo katika ufundishaji wa lugha, Mwalimu Immaculata alisema nyimbo ni zana muhimu inayosaidia kuongeza uelewa na kuhifadhi kumbukumbu za kudumu kwa wanafunzi, hasa watoto.
Aidha, alieleza kuwa kuanzia mwaka huu Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) limeanza kutahini wanafunzi wa shule za msingi katika lugha mbalimbali ikiwemo Kifaransa, Kichina na Kiarabu, akibainisha kuwa hatua hiyo ni fursa kubwa kwa wanafunzi kupata manufaa ya lugha hizo za kimataifa.
Katika maadhimisho hayo, mada mbalimbali ziliwasilishwa ikiwemo umuhimu wa kutumia muziki katika ufundishaji wa Kifaransa, ambapo ilibainika kuwa mbinu hiyo inachochea uelewa wa haraka na husaidia wanafunzi kukumbuka wanachojifunza kwa urahisi.
Maadhimisho ya mwaka huu yamewakutanisha walimu, wahadhiri na wanafunzi wa Kifaransa kutoka Tanzania Bara na Visiwani, yakionyesha kwa mara nyingine kuwa lugha hiyo ina mvuto wa kipekee katika muziki na hivyo kuwa rahisi kufundisha na kujifunza.


Sehemu ya washiriki wa maadhimisho ya Siku ya Walimu wa Kifaransa Duniani wakifuatilia mijadala hapo jana katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari Azania. (Picha na Vincent Mpepo).
Leave a comment