
Na Mwandishi Wetu
Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita limewataka viongozi wa makundi ya mitandao ya kijamii, hususan WhatsApp, kudhibiti usambazaji wa taarifa za uchochezi, uvunjifu wa amani.
Wito huo umetolewa Desemba 8, 2025 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, SACP Safia Jongo, alipoungana na Mtandao wa Polisi Wanawake Tanzania (TPF-Net) mkoani humo kutoa msaada katika Kituo cha Afya Nyankumbu ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga ukatili wa kijinsia.
Kamanda Jongo alisema mitandao ya kijamii, hususan makundi ya WhatsApp, isiruhusiwe kuwa majukwaa ya kusambaza chuki, vitisho, taarifa za upotoshaji na unyanyasaji wa kidijitali dhidi ya wanawake na wasichana.
Alisema wasimamizi wa makundi ya WhatsApp na watumiaji wa mitandao ya kijamii wanayo nafasi kubwa ya kudhibiti maudhui yanayokiuka maadili, sheria na kuchochea uvunjifu wa amani.
“Ni wajibu wao kuhakikisha mitandao haigeuki kuwa chanzo cha uhalifu na ukatili wa kijinsia,” alisema Kamanda Jongo.
Alizungumzia Mtandao wa TPF-Net unaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kupambana na ukatili unaotekelezwa kupitia majukwaa ya kidijitali, sambamba na kuhamasisha wananchi kutoa taarifa mapema wanapobaini au kukumbana na vitendo vya ukatili.
Aidha, amewataka wananchi kuepuka vitendo vya vurugu, uhalifu na uvunjifu wa amani, huku akisisitiza umuhimu wa kukomesha vitendo vyote vya ukatili, hususan unaofanywa mtandaoni dhidi ya wanawake na wasichana.

Leave a comment