Na OWM (KAM) – DODOMA

Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) umepongezwa kwa hatua kubwa ilizochukua katika kuboresha upatikanaji wa huduma kwa wananchi, hususan utoaji wa fidia kwa wafanyakazi wanaokumbana na madhila ya ajali ama ugonjwa unaotokana na kazi.

Pongezi hizo zimetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Sangu jana jijini Dodoma wakati wa ziara yake katika Ofisi za Makao Makuu ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) alipokutana na menejimenti na baadhi ya watumishi wa WCF kwa lengo la kujua majukumu ya Mfuko huo sambamba na kutoa maelekezo ya kiutendaji yanayolenga kuongeza tija na ufanisi.

Sangu alisema huduma hizo bora zimechangia kuimarisha imani ya wananchi kwa mfuko, ambapo wafanyakazi wanaopatwa na majanga kutokana na kazi wamekuwa wakipatiwa huduma kwa wakati na kwa kiwango kinachostahili hivyo kuongeza ufanisi na kupunguza usumbufu kwa wafanyakazi,

Katika hatua nyingine, Waziri Sangu ameitaka Menejimenti ya WCF kuendeleza ubunifu katika utekelezaji wa majukumu yao, ikiwemo kuongeza nguvu ya mifumo mipya ya kidijitali inayoboresha mbinu za utoaji huduma kwa wakati na ufanisi zaidi ili kufikia wananchi kwa haraka.

Awali, akizungumza, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Rahma Kisuo, amehamasisha Menejimenti ya Mfuko huo kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu majukumu na huduma zinazotolewa na Mfuko, ili kuongeza uelewa kwa waajiri wengi zaidi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa WCF Dkt. John Mduma alisema WCF imejipanga kuendelea kuboresha mifumo ya utoaji huduma ili kuhakikisha madai ya fidia yanashughulikiwa kwa wakati, uwazi na ufanisi zaidi.

Posted in

Leave a comment