Na Athuman Kajembe, Nachingwea

Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, mkoani Lindi, Mohamed Hassan Moyo, ameonesha kukerwa baada ya kubaini ujenzi wa Kituo cha Afya cha Nammanga, Kata ya Ruponda, unaendelea bila kufuata Hati ya Makadilio Kiasi cha Kazi (BOQ) kama ilivyoainishwa na serikali.

Akiwa katika ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi huo, DC Moyo alisema serikali haiwezi kuvumilia wataalamu wanaojenga majengo ya umma bila kuzingatia taratibu, kanuni na viwango vilivyowekwa.

“Leo hii jamvi linafunikwa bila utaratibu, nondo za mita nane zinatumika badala ya nondo za mita 12 na mbao zinazotumika kujenga majengo mawili si zile zilizo kwenye BOQ, hili ni kosa kubwa,” alisema DC Moyo.

Alisema kitendo hicho kinaashiria matumizi mabaya ya fedha za umma na ujenzi wa miundombinu isiyokidhi viwango vya ubora.

“Naagiza TAKUKURU kuwakamata na kuwafikisha mahakamani wahandisi wote wanaohusika ili kujibu kwa nini wanajenga chini ya kiwango na kutumia vifaa visivyoidhinishwa”, alisema DC Moyo.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea ambaye pia ni Afisa Mipango, Joshua Mnyang’ali, alikiri kuwepo kwa makosa katika ujenzi huo na kumuomba DC Moyo msamaha mbele ya hadhira.

Hata hivyo, DC Moyo alisisitiza kuwa suala hilo litashughulikiwa kikamilifu kupitia ofisi za TAKUKURU ili kuhakikisha haki inatendeka na fedha za serikali hazipotei.

Inakumbukwa kuwa mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Nammanga umetengewa zaidi ya milioni 200 hadi kufikia Februari 2026, kiasi kinachotarajiwa kukamilisha ujenzi huo kwa viwango vinavyokubalika.

Posted in

Leave a comment