
Na Mwandishi wetu, Nachingwea
Mbunge wa Jimbo la Nachingwea Fadhili Liwaka ameahidi kuwalipia bodaboda zaidi 300 shilingi Elfu tano (5000) kwa Kila bodaboda atakayekwenda kununua kofia ngumu kwenye duka maalum alilolipendekeza.
Akizungumza katika kikao kazi na bodaboda hao hivi karibuni, Mbunge Liwaka alisema kuwa ameamua kuwaunga mkono kwa kiasi hicho cha fedha kwa lengo kuwaondolea adha ya kukamatwa na polisi wa barabarani pamoja kujikinga na ajali za barabarani.
“Napokea simu kutoka kwa bodaboda juu ya kukamatwa na polisi wa barabarani kwa kosa la kutokuwa na kofia ngumu hivyo kama Mbunge wenu nimeamua kuwachangia kiasi hicho ili kila mmoja wenu aweze kulimiki kofia ngumu yake”, alisema Mbunge Liwaka.
Aidha aliliomba Jeshi la Polisi wilaya ya Nachingwea kuwapa muda mfupi ili kila bodaboda aweze kununua kofia ngumu kwa ofa aliyoitoa ya kuwachangia kiasi tajwa.

Kwa upande wake, mmoja wa waendesha bodaboda Wilaya ya Nachingwea, Mohamed Rashidi alimshukuru Mbunge kwa ahadi hiyo ya fedha ambayo itawawezesha bodaboda kupata kofia ngumu na wapo tayari kumuunga mkono kwa kununua kofia hizo kama alivyo waelekeza.


Leave a comment