
Na Vincent Mpepo
Wanataaluma katika taasisi za elimu ya juu nchini wametakiwa kufanya tafiti zenye kuleta matokeo chanya, ikiwemo kutatua changamoto mbalimbali za kijamii na kubadili maisha ya wananchi, badala ya kuzihifadhi kabatini mara baada ya kuhitimu.
Wito huo umetolewa na washiriki wa mafunzo ya ushauri wa kitaalamu ya siku mbili yaliyoanza leo katika Ukumbi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), jijini Dar es Salaam. Mafunzo hayo yamewakutanisha wanataaluma na waendeshaji kutoka Kitivo cha Sanaa na Sayansi za Jamii pamoja na vitivo vingine vya chuo hicho.
Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mtiva wa Kitivo cha Sanaa na Sayansi za Jamii, Mkuu wa Idara ya Sosholojia na Ustawi wa Jamii, Dkt. Mariana Makuu, alisema kuwa wakati umefika kwa wanataaluma kugeuza nadharia kuwa vitendo ili kutatua changamoto za kijamii, kiuchumi na kiutamaduni.
“Mafunzo haya yanalenga kubadili mtazamo wa kufikiri na utendaji kutoka tafiti za kinadharia pekee kwenda kwenye tafiti zenye matokeo halisi,” alisema Dkt. Makuu.
Aliongeza kuwa matarajio ya kitivo ni kuona mafunzo hayo yakileta matokeo chanya kwa washiriki mmoja mmoja na kwa taasisi kwa ujumla, ikiwa ni pamoja na kuchochea umahiri katika kazi za ushauri wa kitaalamu.
Aidha, aliwahimiza washiriki kufuatilia mafunzo hayo kwa makini ili kupata ujuzi utakaosaidia kuongeza uelewa na mchango wao katika eneo la ushauri wa kitaalamu kwa ajili ya utatuzi wa changamoto mbalimbali za jamii kwa maslahi mapana ya taifa.
Kwa upande wake, mwezeshaji wa mafunzo hayo, Innocent Deus, alisema kuwa wasomi, wanataaluma na watafiti wanapaswa kuwa na mawazo bunifu yatakayosaidia kutatua changamoto za jamii kupitia tafiti wanazozifanya, ili kuhalalisha uwepo na mchango wao katika jamii.

Akizungumzia masuala ya ushauri wa kitaalamu, alisema ni muhimu kwa watafiti na wataalamu kuanza kushirikiana na taasisi zenye uzoefu katika fani husika ili kujijenga kitaaluma, kutengeneza taswira chanya na kuvutia wadau mbalimbali wa kushirikiana nao siku zijazo.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa kazi za ushauri wa kitaalamu na tafiti katika taasisi za elimu ya juu zinapaswa kujumuishwa katika mipango mkakati ya taasisi husika ili kuwepo na mifumo ya kupima na kutathmini utekelezaji wake.
Akichangia mada katika mjadala wa siku ya kwanza ya mafunzo hayo, Dkt. Janeth Laurean kutoka Idara ya Uchumi na Maendeleo ya Uchumi wa Jamii chuoni hapo, alishauri kuwepo kwa utaratibu wa kuwatambua na kuwathamini wanataaluma watakaobuni miradi na tafiti zitakazoingizia chuo mapato, jambo litakalowahamasisha wengine kushiriki katika kazi hizo.
Wakati mjadala huo ukiibua changamoto mbalimbali katika mfumo wa elimu na tafiti zinazofanyika bila kuzaa majibu ya moja kwa moja kwa jamii, ilibainika kuwa bado mtazamo wa baadhi ya wanafunzi na wasomi ni kuhitimu na kuvaa joho la mahafali, badala ya kuona elimu na tafiti kama nyenzo ya kuleta mabadiliko ya kweli katika jamii.


Leave a comment