
Na Vincent Mpepo
Mtaalamu wa huduma za ushauri wa kitaalamu Innocent Deus amewataka wasomi katika fani za sanaa na sayansi za jamii kudhihirisha mchango wao katika utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii kupitia eneo la ushauri wa kitaalamu.
Aliyasema hayo wakati wa mafunzo ya kitaalamu kwa wanataaluma na waendeshaji katika Kitivo cha Sanaa na Sayansi ya Jamii cha Chuo Kikuu Huria cha Tanzania yaliyofanyika katika Ukumbi wa chuo hicho jijini Dar es salaam.
“Changamoto za kijamii zinahitaji utatuzi kutoka kwa wasomi katika fani hizi na kwamba uwepo wenu utaleta tija ikiwa mtasaidia jamii kukabiliana na changamoto”, alisema Deus.
Akizungumzia uandishi miswada ya kazi za ushauri wa kitaalamu alisema kuna umuhimu wa waandishi kuzingatia masuala kadhaa ikwemo namna ya uandishi, ushawishi na namna ya uwekaji malengo ya mradi na kutojifungia ofisini badala yake kuonesha umahiri wao ili jamii itambue.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Idara ya Sosholojia na Ustawi wa Jamii chuoni hapo, Dkt. Mariana Makuu mafunzo hayo yanalenga kubadili mtazamo wa kufikiri na utendaji kutoka tafiti za kinadharia kwenda kwenye huduma za ushauri wa kitaalamu zenye matokeo halisi kwa jamii.
“Wakati umefika kwa wanataaluma kugeuza maarifa na nadharia wanazozalisha kuwa vitendo vinavyogusa maisha ya wananchi kupitia huduma za ushauri wa kitaalamu,” alisema Dkt. Makuu.
Aidha, aliwahimiza washiriki kuyafuatilia mafunzo hayo kwa umakini ili kupata ujuzi na umahiri utakaowawezesha kushiriki kikamilifu katika utatuzi wa changamoto mbalimbali za kijamii kwa maslahi mapana ya taifa.
Mratibu wa Ushauri wa Kitaalamu na Uhusiano wa Jamii wa Kitivo cha Sanaa na Sayansi za Jamii (FASS), Celia Muyinga alisema mafunzo hayo ni muhimu kwa wafanyakazi wa kitivo hicho ili kuwajengea uwezo na kujiamini katika kutafuta fursa mbalimbali za kazi za huduma za ushauri wa kitaalamu.
“Tathmini za hivi karibuni zinaonesha kuwa ushiriki wa wanataaluma katika Kitivo cha Sanaa na Sayansi za Jamii (FASS), katika uandaaji wa maandiko ya miradi na kushiriki katika zabuni za ushauri wa kitaalamu bado ni mdogo”, alisema Celia.
Alisema hali hiyo inatokana na mtazamo kuwa taratibu za kiufundi ni ngumu, pamoja na ukosefu wa kujiamini katika kushindana kwenye mazingira ya ufadhili yenye ushindani mkubwa.
Alibainisha athari za changamoto hizo kuwa ni kukwamisha kitivo katika kuvutia rasilimali za nje na kutoifikia jamii kwenye huduma za ushauri wa kitaalamu na kutotumika ipasavyo kwa wataalamu waliopo katika kitivo hicho.

Leave a comment