
Na Tabia Mchakama, Zanzibar
Serikali imeitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) kuendelea kusimamia kikamilifu upatikanaji wa huduma za bima nchini hususani zinazowahusu wageni kutoka nje ili kuboresha huduma hiyo na kuendelea kuvutia wawekezaji, watalii na wafanyabiashara kwa maslahi ya taifa.
Maelekekezo hayo yalitolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Balozi Mahmoud Thabiti Kombo alipotembelea banda la mamlaka hiyo katika Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Zanzibar (ZITF) kuelekea Maadhimisho ya 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Katika ziara hiyo, Waziri Kombo alipata fursa ya kuelimishwa kuhusu majukumu ya TIRA katika kusimamia na kuendeleza sekta ya bima, hususan katika kuhakikisha ulinzi wa maslahi ya wageni kutoka nje wanaoingia Tanzania kwa madhumuni ya utalii, biashara na shughuli nyingine.

Alisema kuna umuhimu wa kuwepo kwa mifumo madhubuti ya bima kwa wageni ili kulinda usalama wao, kuongeza imani ya wawekezaji na watalii, pamoja na kuimarisha taswira ya Tanzania kimataifa kama nchi salama na yenye mazingira rafiki ya uwekezaji na utalii.
Aidha, alielekeza wadau wa bima kushirikiana kwa karibu na taasisi nyingine za serikali zinazohusika na masuala ya uhamiaji, utalii na afya hasa wizara yake ili kuhakikisha bidhaa za bima kwa wageni zinaeleweka, zinapatikana kwa urahisi na zinakidhi mahitaji halisi ya soko la kimataifa.
Kwa upande wake, Meneja wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Kanda ya Unguja, Kurenje Mbura alimhakikishia Waziri Kombo kuwa mamlaka itaendelea kusimamia sekta ya bima kwa weledi na kushirikiana na wadau wote ili kuboresha huduma za bima kwa wageni wa nje na mizigo inayoagizwa kutoka nje jambo litakalosaidia kukuza sekta ya utalii, biashara na uchumi wa taifa kwa ujumla.
Maonesho hayo kuelekea Maadhimisho ya miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar, yalianza Tarehe 29/12/2025 na yanatarajiwa kumalizika tarehe 16/01/2026 katika Viwanja vya Nyamanzi Dimani Zanzibar.


Leave a comment