Na Mwandishi Wetu, Nachingwea
Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea Mohamedi Hassani Moyo amewataka madiwani wa Halmashauri za Ruangwa na Mtama kutimiza wajibu wao wa kuwatumikia wananchi na kufuata kanununi na taratibu za uongozi.
Moyo alisema hayo wakati akifungua mafunzo elekezi yenye lengo la kuwajengea uwezo katika Nyanja za uongozi, usimamizi na uwajibikaji katika kuwatumikia wananchi waliowachagua.
Alisema mafanikio ya halmashauri hizo yanategemea ushirikiano wa madiwani, wataalamu na wananchi na kuwasihi kutoingiza maamuzi binafsi na badala yake kuhakikisha wanadhibiti mianya ya rushwa na kutanguliza mbele maslahi ya umma.
“Jukumu lenu kubwa ni kudumisha amani, uzalendo, umoja, na uwajibikaji kwasababu ndio yanayochochea maendeleo”, alisema Moyo.
Aidha, aliwataka madiwani kutambua walichukua fomu na kugombea nafasi hizo kwa ajili ya kutumikia wananchi na si vinginevyo, hivyo aliwakumbusha kuacha alama katika uongozi wao ili wakumbukwe kwa mema.
Aliwataka kuepuka chuki kati yao na wataalamu pamoja na wananchi na badala yake kwenda kusimamia fedha za serikali zinazoletwa katika halmashauri ili ziweze kuleta maendeleo kwa wananchi.
Leave a comment