Mwezeshaji kutoka Umoja wa Maabara Tanzania, Kezia Mbwambo akifafanua jambo kuhusu mifumo ya ubora kwa wataalam wa maabara kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwenye mafunzo yanayoendelea kufanyika katika ukumbi wa Chuo cha Ustawi wa Jamii jijini Dar es Salaam.

Na Okello Thomas

Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imetoa mafunzo ya utekelezaji wa ISO/IEC 17025:2017 kwa wataalamu wa maabara ili kuongeza umahiri katika utendaji wa kila siku katika maabara.

Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo yaliyofanyika mwishoni mwa wiki kwenye ukumbi wa Chuo cha Ustawi wa Jamii, Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko amesema Kiwango cha ISO/IEC 17025:2017 kinaipa maabara uwezo wa kuonesha umahiri katika kufanya uchunguzi na kutoa matokeo yanayotambulika na kukubalika kitaifa na kimataifa

“Utekelezaji wa kiwango hicho si hitaji la ithibati pekee, bali ni nyenzo muhimu ya kuimarisha ubora, uaminifu na ushindani wa huduma za maabara”, alisema Dkt. Mafumiko.

Alisema maabara kupata ithibati na kuitekeleza kwa vitendo yatatoa sifa njema si tu kwa mamlaka bali pia kwa taifa kwa ujumla.

“Nitumie fursa hii kusisitiza kwamba juhudi na uwajibikaji wenu ndiyo msingi wa mafanikio ya ithibati katika mamlaka”, alisema Dkt. Mafumiko.

Alisema mamlaka itaendelea kutoa rasilimali zinazohitajika kwa ajili ya utekelezaji wa mfumo wa usimamizi wa ubora ulioanzishwa kulingana na mahitaji ya viwango vya ubora wa kimataifa (ISO).

Mwezeshaji kutoka Umoja wa Maabara, Bi. Kezia Mbwambo alisema kuwa Kiwango cha ISO/IEC 17025:2017 ni mfumo wa usimamizi uliotengenezwa na Shirika la Viwango vya Kimataifa (ISO) linalolenga seti ya mahitaji ambayo taasisi au shirika linapaswa kufikia katika mfumo wa ubora ili kupata hati ya ISO.

Naye Riphat Lusingo ameishukuru mamlaka kwa kuwezesha mafunzo hayo na kuahidi kwa niaba ya wataalamu wengine wa maabara kuendelea kujituma katika kutekeleza mifumo ya ubora kwa kuzingatia matakwa ya viwango vya kimataifa vya maabara kwa kufuata taratibu na miongozo husika.

Wataalam wa Maabara kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) wakifuatilia mafunzo ya Mifumo ya Ubora ISO/IEC 17025:2017.

Mtaalam wa Maabara, Judith Swai (kushoto) akimuuliza swali mwezeshaji wa mafunzo kutoka Umoja wa Maabara Tanzania, Kezia Mbwambo.

Posted in

Leave a comment