
Na Mwandishi Wetu
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imekutana na kuzungumza na wananchi wa Mtaa wa Golani, Kata ya Kimara, Wilaya ya Ubungo kwa lengo la kutatua changamoto ya upatikanaji huduma ya maji katika mtaa huo.
Akizungumza kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano, Bi. Everlasting Lyaro amewatoa hofu wananchi wa Golani kwamba Mamlaka inatambua changamoto ya maji katika mtaa huo na zipo hatua za muda mfupi na mrefu ambazo zinachukuliwa ili kuhakikisha huduma hiyo inapatikana.
“Kwanza tuwaombe radhi wananchi wa hapa Golani kwa changamoto ya maji mnayoipitia, tunatambua maji ni haki ya kila mmoja wetu”, alisema Bi. Everlasting.
Alisema kwa kuanza Mamlaka italeta matenki Matano (05) yenye ujazo wa Lita 10,000 kila moja na kuyajaza maji yatakayouzwa kwa bei elekezi zoezi na zoezi hilo litafanyika kuanzia 15.01.2025 ili kukabiliana na changamoto hiyo kama hatua za awali ambazo ni za muda mfupi.
“Tutaratibu mgao wa maji katika eneo hili ambapo mtapata maji mara tatu kwa wiki, Alhamisi, Jumapili na Jumatatu”, alisema Bi. Evarlasting.
Akizungumzia utatuzi wa changamoto hiyo kwa mpango wa muda mrefu alisema DAWASA itajenga kituo cha kusukuma maji eneo la kwa Mama Stela kitakachosaidia maji kufika sehemu mbalimbali zilizookua hazipati huduma hiyo hapo awali.

Kwa upande wake, Meneja wa Mkoa wa kihuduma DAWASA Kinyerezi, Mhandisi Antony Budaga alisema watumishi hawatakaa ofisi badala yake watatoka kuwafikia wananchi na kuhakikisha yaliyopangwa katika kikao hicho yanatekelezwa.

Mkazi wa Golani, Rajabu Said ameshukuru jitihada zinazofanyika kuhakikisha changamoto ya maji mtaani hapo inakwisha kwamba wananchi wanapata matumaini ya upatikanaji wa huduma ya maji amabayo itawaondolea kero ya ununuzi wa maji kwa watoa huduma binafsi inayowagharimu fedha nyingi.

Leave a comment