Na Mwandishi Wetu

Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew, amemuagiza Mkandarasi Kampuni ya Afcons ya India kuzingatia maelekezo ya serikali kuhusu viwango vipya vya mishahara kwa wafanyakazi wa ngazi za chini, vinavyotaka kulipwa shilingi 16,500 kwa siku sawa na shilingi 515,000 kwa mwezi.

Agizo hilo amelitoa leo wakati wa ukaguzi wa Mradi wa Maji wa Miji 28 katika mji wa Kayanga, wilayani Karagwe, baada ya kubaini kuwa mkandarasi huyo anawalipa vibarua shilingi 12,500 kwa siku, kinyume na maelekezo ya serikali.

Alisema serikali ilielekeza viwango hivyo vipya vya mishahara kuanza kutumika Januari Mosi mwaka huu, na kusisitiza kuwa malipo hayo yaanze mara moja pamoja na kusainiwa kwa mikataba mipya inayoendana na mabadiliko hayo.

“Nakuelekeza kuwasilisha nakala za mikataba hiyo mipya katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na kwa viongozi wa sekta ya maji katika mkoa husika”, alisema Kundo.

Sanjali na hilo, alionesha kutoridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo, ambao awali ulipangwa kukamilika Desemba 2025 kabla ya kuongezewa muda hadi Septemba mwaka huu.

Kutokana na hali hiyo, amemuagiza Mkuu wa Wilaya kwa kushirikiana na viongozi wa sekta ya maji mkoani kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini iwapo vifaa vya utekelezaji wa mradi vimeagizwa na kama mpango kazi uliopo unatekelezeka kwa muda uliopangwa.

Alisema Wizara ya Maji haitavumilia uzembe wa mkandarasi wakati wananchi wakiendelea kupata changamoto ya huduma ya maji safi na salama.

Mradi huo wa Maji wa Miji 28 wa Kayanga, unagharimu kiasi cha shilingi bilioni 64.32 na unatarajiwa kuwanufaisha wakazi 352,790, na mpaka sasa umefikia asilimia 70 ya utekelezaji.

Posted in

Leave a comment