
Na Alvar Mwakyusa
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetangaza mwelekeo wa mvua za msimu wa Masika kwa mwaka 2026, ikieleza kuwa baadhi ya maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani, huku maeneo mengine yakitarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Februari 5, 2026, mvua za Masika zinazotarajiwa kuanza mwezi Machi hadi Mei zitahusisha zaidi ukanda wa Ziwa Victoria, Nyanda za juu Kaskazini Mashariki, Pwani ya Kaskazini pamoja na Kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.
TMA imeeleza kuwa ongezeko la mvua linatarajiwa zaidi mwezi Aprili, hali inayoweza kuambatana na athari mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Akizungumza wakati wa kutangaza mwelekeo huo, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Ladislaus Chang’a, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), alisema ni muhimu kwa jamii kutumia taarifa za utabiri wa hali ya hewa katika kupanga na kutekeleza shughuli zao za kila siku.
Alisema mvua hizo, pamoja na faida zake katika sekta mbalimbali, zinaweza pia kusababisha changamoto ikiwemo mafuriko, uharibifu wa miundombinu na uchafuzi wa vyanzo vya maji endapo tahadhari hazitazingatiwa kwa wakati.
Alisisitiza umuhimu wa wananchi na wadau wa sekta mbalimbali kuendelea kufuatilia utabiri wa kila siku na tahadhari rasmi zinazotolewa na TMA.
Katika ukanda wa Ziwa Victoria, mvua za wastani hadi juu ya wastani zinatarajiwa katika mikoa ya Kagera na Geita pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma, huku mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Mara na Simiyu ikitarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani.
Kwa upande wa pwani ya kaskazini ikiwemo Dar es Salaam, Tanga, Pwani na visiwa vya Unguja na Pemba, mvua za wastani hadi juu ya wastani zinatarajiwa kuanza mapema mwezi Machi na kuisha mwishoni mwa Mei au mwanzoni mwa Juni.
Nyanda za juu Kaskazini Mashariki zinazojumuisha mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro zinatarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani, huku mvua hizo zikitarajiwa kuanza katikati ya mwezi Machi na kuisha mwishoni mwa Mei.
TMA imeonya kuwa, licha ya mwelekeo wa jumla wa mvua, matukio ya vipindi vya mvua kubwa yanaweza kujitokeza hata katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua chache, hali inayoweza kuongeza hatari ya mafuriko, uharibifu wa mali na kuibuka kwa magonjwa yanayotokana na uchafuzi wa maji.
Wadau wa sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, mifugo, afya, usafiri, ujenzi na menejimenti za maafa wametakiwa kuzingatia taarifa hizi katika kupanga na kutekeleza shughuli zao, huku wananchi wakihimizwa kuendelea kufuatilia taarifa rasmi za hali ya hewa zinazotolewa na TMA.
Leave a comment