Na Issa Mwadangala

Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe limetoa taarifa ya matukio mawili ambapo katika tukio moja limeripoti kifo cha Feriki Kareai (54) Mkulima, Mkazi wa Kijiji cha Lukululu Wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe, amabaye alikutwa amefariki dunia huku mwili wake ukiwa umefukiwa na kifusi pembeni mwa Mto Itemba.

Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi Mkoni humo, kifo hicho kilichotokea tarehe 01 Februari, 2026 saa 07:00 mchana katika maeneo ya Mto Itemba, Kijiji cha Lukululu, Kata ya Mlangali, Tarafa ya Iyula, Wilaya ya Mbozi, Mkoa wa Songwe.


Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa chanzo cha kifo ni marehemu kufukiwa na kifusi alipokuwa  anachimba madini aina ya dhahabu, hali iliyopelekea kifusi hicho kuporomoka na kumfukia  Hivyo kusababisha kifo chake.

Na katika hatua nyingine, jeshi  hilo limetoa taarifa ya tukio la uhalifu lililotokea tarehe 04 Februari, 2026 saa 04:00 asubuhi, katika eneo la Kisimani, Mtaa wa Unyamwanga, Kata ya Tunduma, Wilaya ya Momba, Mkoa wa Songwe.

Katika tukio hilo, Yengo Mwapina Mkazi wa Sogea Wilaya ya Momba Mkoani Songwe, alishambuliwa na watu watatu wasiojulikana akiwa njiani akitoka Benki ya NBC Tunduma.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, washambuliaji hao walimfyatulia risasi na kumsababishia jeraha kiunoni upande wa kushoto na kumnyang’anya fedha taslimu kiasi cha Shilingi Milioni Hamsini na Nne (54,000,000) za kitanzania.

Muhanga alikimbizwa katika Kituo cha Afya Tunduma ambapo alipatiwa matibabu ya awali na baadaye alihamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Songwe kwa ajili ya matibabu zaidi.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe linaendelea na uchunguzi wa kina sambamba na msako mkali ili kuwabaini na kuwakamata watuhumiwa wa tukio hilo na kuwafikisha Mahakamani kwa hatua zaidi.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe linatoa wito kwa wananchi kutojihusisha na shughuli za uchimbaji wa madini kiholela na bila kufuata taratibu za usalama na linawaomba wananchi kutoa taarifa zitakazosaidia kufanikisha kuwakamata watuhumiwa waliohusika katika tukio la unyang’anyi kwa kutumia silaha.

Posted in

Leave a comment