Na Mwandishi Wetu, Nachingwea – Lindi
Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Mohamed Hassan Moyo ameongoza zoezi la ugawaji wa miche zaidi ya elfu sabini ya mikorosho kwa wananchi, ikiwa ni juhudi za kuongeza uzalishaji wa zao la korosho wilayani humo.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo tarehe 23/02/2026, Moyo alisema serikali imeamua kuwapatia wakulima miche hiyo bila malipo ili kupunguza gharama za uzalishaji na kuwawezesha kuongeza kipato chao.
Ameeleza kuwa mpango huo unatekelezwa kwa lengo la kuimarisha sekta ya kilimo na kuinua uchumi wa wananchi.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea, Adinan Mpyagila, ambaye ameshiriki katika zoezi hilo, amesema ugawaji wa miche hiyo ya mikorosho utachochea ongezeko la uzalishaji na kuboresha ubora wa zao la korosho wilayani hapo.
Kwa upande wao, wakulima walishukuru kupata miche hiyo, walisema hapo awali walikuwa wakisubiri kwa muda mrefu kupata mavuno walipopanda miche ya zamani tofauti ni miche mipya waliyopewa ambayo itawawezesha kupata mavuno kwa muda mfupi zaidi.
Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa serikali wa kuendeleza mazao ya kimkakati, ikiwemo korosho, kwa lengo la kuongeza mapato ya wakulima na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.
Leave a comment