
Na Cosmas Msuha
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Balozi Dkt. Bashiru Ally amefanya ziara mkoani Geita na kugagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya Soko la Kimataifa Samaki la Chato na kumtaka mkandarasi kukamilisha ujenzi wa mtambo wa kukaushia dagaa kabla ya mwezi April mwaka huu.
Dkt. Bashiru alitoa maagizo hayo Februari 28, 2026 baada ya kukagua ujenzi wa miundombinu ya soko hilo ambapo ameonesha kutoridhishwa na kasi ya kazi zinazofanywa na mkandarasi huyo licha ya changamoto za malipo zinazomkabiri.A
Aliagiza kufanyika tathmini mpya ya gharama za mtambo huo ili upatikane kwa haraka ambapo kukamilika kwa ujenzi huo kutachangia upatikanaji wa ajira kwa makundi mbali mbali ya vijana katika soko hilo.
“Nataka kazi ifanyike kwa kasi na Jumatatu barua iwe imejibiwa na mpaka Jumatano mkandarasi awe ameipata na mimi nipate nakala”, alisema Dkt. Bashiru
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Miundombinu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mhandisi George Kwandu alisema kuchelewa kwa malipo kwa mkandarasi kulitokana na changamoto kadhaa ambazo zilisababisha mkandarasi kushindwa kununua mtambo kwa wakati hatahivyo wamejipanga kujadiliana na kuzifanyia kazi ili kuharakisha malipo hayo.
Sanjali na maagizo hayo, Dkt. Bashiru amemtaka mkandarasi huyo kushirikiana na taasisi nyingine katika uimarishaji wa miundombinu na huduma za kijamii ikiwemo miundombinu ya maji, umeme, barabara ili soko hilo litambuliwe kimataifa na kuanza kufanya kazi kwa manufaa ya wananchi.

Leave a comment