Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Rukwa, Jacqueline Mzindakaya akizungumza na baadhi ya vyombo vya habari kuhusu utekelezaji wa bima ya afya kwa wote.

Na Cosmas Msuha

Serikali imepongezwa kwa kuendelea kutekeleza mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, hatua inayolenga kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za afya bila kujali uwezo wake wa kifedha.

Pongezi hizo zimetolewa na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Rukwa, Jacqueline Mzindakaya, wakati akishiriki katika zoezi la kugawa kadi za mfano za bima ya afya kwa walengwa wenye mahitaji maalum, wakiwemo watoto na mama wajawazito.

Katika tukio hilo, Mbunge huyo aligawa kadi 30 za mfano kati ya jumla ya kadi 48,500 zilizotengwa kwa Mkoa wa Rukwa kwa ajili ya kaya zisizo na uwezo.

Akizungumza katika semina iliyowakutanisha walengwa wa kaya maskini pamoja na wadau wa maendeleo mkoani humo, Mzindakaya alisema kuwa mpango huo ni hatua muhimu ya kusaidia wananchi wasio na uwezo kupata huduma za afya bila vikwazo vya kifedha.

Katika hotuba yake, alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutimiza ahadi yake aliyoitoa katika siku 100 za mwanzo wa uongozi wake ya kuhakikisha Watanzania wasiojiweza wanapatiwa bima ya afya bure.

“Mpango huu unalenga kuhakikisha kila Mtanzania anakuwa na uhakika wa kupata matibabu bila kujali hali yake ya kipato,” alisema Mzindakaya.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Mkoa wa Rukwa, Amos Edward, alisema serikali imejipanga kuhakikisha mpango huo unatekelezwa kwa ufanisi ili wananchi waweze kunufaika kikamilifu.

Alisema juhudi zinafanyika kuhakikisha vituo vyote vya afya vinavyotoa huduma chini ya mpango huo vinakuwa na dawa na vifaa tiba vya kutosha.

Aidha, aliwakumbusha watoa huduma katika hospitali kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wananchi wote bila ubaguzi, huku wakizingatia matumizi ya lugha ya staha na kuwahudumia kwa usawa wote wanaofika hospitalini, ikiwemo wanaolipia huduma kwa fedha taslimu.

“Tunatarajia kuwa na vifurushi mbalimbali vitakavyowezesha kila kaya kupata bima itakayowanufaisha katika kupata huduma bora zaidi za afya,” alisema Edward.

Naye Mwenyekiti wa Kata ya Kiwango, Paulin Nikasi, aliipongeza serikali kwa kuanzisha mpango huo na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kujiunga na bima ya afya ili kupata matibabu kwa urahisi.

Alisisitiza umuhimu wa kuwapa kipaumbele makundi maalum kama wazee, mama wajawazito na watoto wanapofika hospitalini ili wapate huduma kwa wakati.

“Ni jambo jema kwa sababu mpango wa bima ya afya kwa wote utamfikia kila Mtanzania. Zamani watu wengi walipoteza maisha kutokana na kushindwa kumudu gharama za matibabu,” alisema Nikasi.

Sambamba na masuala ya afya, semina hiyo pia ilitoa elimu ya ujasiriamali kwa wananchi, ambapo washiriki walipata mafunzo kuhusu fursa za mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri.

Mafunzo hayo yaliwasilishwa na Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, Noela Munis, ikiwa ni sehemu ya jitihada za serikali kuwawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi na kuboresha maisha yao.

Posted in

Leave a comment