
Na Mwandishi Wetu
Mtandao wa Polisi Wanawake Mkoa wa Ruvuma (TPF–NET) umeendelea kuonyesha moyo wa kujali jamii baada ya kutembelea na kutoa msaada kwa watoto wenye mahitaji katika Kituo cha kulelea watoto yatima cha Mfaranyaki, kilichopo Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma.
Ziara hiyo iliongozwa na Mwenyekiti wa TPF–NET Mkoa wa Ruvuma, Mrakibu wa Polisi (SP) Atupakisye Mwakasutu, aliyewaongoza polisi wanawake wa mkoa huo kukabidhi msaada wa mahitaji mbalimbali yenye thamani ya Shilingi 800,000 kwa watoto wanaolelewa katika kituo hicho.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, SP Mwakasutu alisema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa wajibu wa Mtandao wa Polisi Wanawake katika kushirikiana na jamii na kuwasaidia watu wenye mahitaji maalum.
“Lengo letu ni kuwashika mkono watoto hawa kwa kuwasaidia mahitaji mbalimbali, lakini pia kuendelea kuwa karibu na jamii inayotuzunguka,” alisema SP Mwakasutu.
Aliongeza kuwa TPF–NET imeamua kufanya hivyo ili kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha huduma kwa jamii, hususan kwa makundi maalumu yanayohitaji msaada.
SP Mwakasutu pia alieleza kuwa Jeshi la Polisi limekuwa na utaratibu wa kutembelea vituo vya kulelea watoto wenye mahitaji maalumu na kutoa misaada mbalimbali, huku akihimiza jamii, taasisi za umma na binafsi kujitokeza kusaidia makundi hayo ili kujenga jamii yenye mshikamano, upendo na kujali.
Mbali na msaada huo, Jeshi la Polisi pia linaendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu lishe bora kwa watoto, malezi bora pamoja na kupinga ukatili wa kijinsia, ili kuongeza uelewa kwa watoto na jamii kwa ujumla.

Kwa upande wake, uongozi wa Kituo cha Mfaranyaki ulilishukuru Jeshi la Polisi kwa msaada huo, ukieleza kuwa umekuwa faraja kubwa kwa watoto wanaolelewa hapo, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea sikukuu za Eid El Fitri na Pasaka.

Leave a comment