
Na Mwandishi wetu,Nachingwea-Lindi
Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Mohamed Hassan Moyo, ameipongeza Kamati ya Lishe ya Wilaya pamoja na Maafisa Lishe kwa kufanya vizuri katika utekelezaji wa masuala ya lishe wilayani humo.
Moyo alitoa pongezi hizo jana wakati wa kikao cha tathmini ya Mkataba wa Lishe kwa robo ya pili ya mwaka wa fedha 2025/2026.
Aliwataka wataalamu wa lishe pamoja na maafisa watendaji wa Kata kuongeza bidii katika kazi zao ili kudumisha na kuendeleza mafanikio yaliyopatikana katika masuala ya lishe.
Alisisitiza kuwa ajenda ya lishe inapaswa kupewa kipaumbele na kuwa ajenda ya kudumu katika vikao mbalimbali vya maendeleo.
Moyo aliwataka watendaji kuhamasisha wanaume kushiriki katika siku ya maadhimisho ya Lishe ya Kijiji (SALIK), akieleza kuwa suala la lishe linamhusu kila mwananchi na si kundi maalumu pekee katika jamii.
Alisema kuna umuhimu wa kila mwanajamii kushiriki na kupata elimu ya lishe, akibainisha kuwa lishe bora ni jambo la muda mrefu na lenye umuhimu kwa afya ya jamii.
Vilevile, alimuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea kuandaa kikao maalumu kitakachowakutanisha viongozi wa dini na mila ili kuhamasisha wananchi kuondoa imani potofu kuhusu masuala ya lishe.
Kupitia kikao hicho, Moyo aliitaka jamii kuacha imani potofu kuhusu matumizi ya unga uliorutubishwa na badala yake kuutumia kwa manufaa ya afya zao kwa kuzingatia elimu wanayopewa na wataalamu.
Akizungumzia utoaji wa chakula shuleni, alisema bado hauwezi kuitwa lishe bora na kwamba unapaswa kuendelea kutolewa mara kwa mara kwa wananchi katika kuboresha afya zao.

Leave a comment