
Na Cartace Ngajiro, Tanga
Katika kuadhimisha siku ya Wanawake Duniani kwa mwaka 2026 watumishi wanawake wa Bandari ya Tanga waliungana na wafanyakazi wanawake wa kutwa wa bandari hiyo kufanya matendo ya huruma.
Wanawake hao wametoa msaada wa mashine za kusaidia upumuaji aina ya “C- PAP Bubble Neonates, Oxygen Flowmeter” pamoja na vifaa mbalimbali katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga -Bombo vyenye thamani ya Shilingi Milioni 5.
Akizungumza baada ya kukabidhi mashine hizo, Afisa Rasilimali Watu Mkuu wa Bandari hiyo Bi. Sharifa Nuhu alisema wamekuwa na utaratibu wa kila mwaka kutumia siku hiyo kufanya matendo ya huruma kwa jamii na mwaka huu wameona wasaidie Hospital ya Rufaa ya Mkoa – Bombo.

“Mwaka huu tumeona tuunge mkono juhudi za serikali katika kuboresha afya za watoto, hivyo tumetoa msaada wa mashine hizo katika wodi ya watoto wachanga katika Hospitali ya Rufaa ya Bombo”, alisema Bi Sharifa.
Akipokea vifaa hivyo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt. Abdi Msangi aliwashukuru watumishi hao kwa msaada walioutoa kwani umetolewa wakati muafaka kutokana na upungufu wa mashine hizo katika wodi ya watoto wachanga wenye matatizo ya upumuaji.
Daktari Bingwa wa Watoto katika Hospitali hiyo, Dkt. Mohamed Salehe alisema kuwa mashine hizo zitasaidia hospitalini hapo ukizingatia ongezeko kubwa la watoto wanaozaliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya upumuaji na kwamba vifaa hivyo vitasaidia kuboresha upatikanaji wa huduma kwa watoto.
Awali wanawake hao waliungana na wanawake wa Mkoa wa Tanga katika maandamano ya kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani Kiwilaya yaliyofanyika katika uwanja wa Shule ya Sekondari ya Usagara, ampabo kauli mbiu ya mwaka 2026 inasema “Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana, Msingi Jumuishi Kufikia Dira 2050”


Leave a comment