
Na Mwandishi Wetu, Nachingwea – Lindi
Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea imetoa mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, sambamba na kukabidhi vifaa mbalimbali ikiwemo matrekta, maguta, magari madogo ya mizigo na pikipiki kwa wanufaika wa mpango huo.
Makabidhiano hayo yaliongozwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Nachingwea, Ramadhani Maiga jana katika viwanja vya Halmashauri hiyo ambapo jumla ya mikopo hiyo ina thamani ya zaidi ya shilingi milioni 570.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Maiga aliipongeza serikali kwa kuendelea kuwezesha upatikanaji wa mikopo hiyo inayolenga kuwainua kiuchumi wananchi na kukuza shughuli za ujasiriamali.
Aidha, aliwataka wanufaika kuvitunza vifaa walivyokabidhiwa pamoja na kuhakikisha wanarejesha mikopo hiyo kwa wakati ili kutoa fursa kwa vikundi vingine kunufaika na mpango huo.
Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea, Stella Kategile, aliwahimiza wananchi kuchangamkia fursa ya mikopo hiyo.

“Ni muhimu kwa wanufaika kuzingatia maandiko ya miradi mliyoainisha na kwamba muiweze kutimiza malengo na kurejesha kwa wakati”, alisema Bi.Stella.
Baadhi ya wanufaika wa mikopo hiyo waliishukuru serikali kwa kutenga fedha hizo na kwamba vikundi vyao vitaendelea kuzitumia kwa ufanisi ili kujikwamua kiuchumi na kuongeza uzalishaji katika shughuli zao.


Leave a comment