Na Mwandishi Wetu, Nachingwea
Chama Kikuu cha Ushirika RUNALI kinachohusisha wilaya za Nachingwea, Ruangwa na Liwale kimefanya kikao na wadau mbalimbali wa kampuni za usafirishaji ikiwa ni maandalizi ya kuelekea msimu mpya wa mazao wa mwaka 2026/2027.
Kikao hicho kilifanyika hivi karibuni katika ofisi za RUNALI zilizopo wilayani Nachingwea, ambapo viongozi wa chama hicho na wawakilishi wa kampuni za usafirishaji walijadili masuala mbalimbali yanayohusu usafirishaji wa mazao wakati wa msimu wa mavuno.
Akizungumza katika kikao hicho, Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika RUNALI, Jahida Hassan, alisema lengo la kikao hicho ni kufanya mazungumzo na wadau wa sekta ya usafirishaji, ikiwa ni sehemu ya utaratibu ambao chama hicho kimejiwekea kuelekea Mkutano Mkuu wa chama.
Alisema kupitia majadiliano hayo, RUNALI inalenga kusikiliza changamoto na maoni ya wadau ili kuboresha utendaji kazi, hususan katika sekta ya usafirishaji wa mazao wakati wa msimu wa mavuno.
Kwa upande wake, mmoja wa wadau wa kampuni za usafirishaji, Selemani Ramadhani Mukili, alisema wanaendelea kuvutiwa kufanya kazi na RUNALI kutokana na ushirikiano mzuri uliopo kati yao.
Alisema RUNALI imekuwa ikifanya malipo kwa wakati jambo ambalo limechangia kuongeza imani kwa kampuni za usafirishaji kuendelea kushirikiana na chama hicho.
Alisema kampuni zao zimejiandaa kikamilifu kwa msimu wa mazao wa mwaka 2026/2027 na ziko tayari kutoa huduma ya usafirishaji kwa weledi na ufanisi mkubwa ili kuhakikisha mazao yanafika kwa wakati katika maeneo husika.
Kwa mujibu wa uongozi wa RUNALI kikao hicho ni sehemu ya maandalizi ya kuhakikisha msimu wa mazao wa mwaka 2026/2027 unafanikiwa kupitia ushirikiano mzuri kati ya chama hicho na wadau wa sekta ya usafirishaji.
Leave a comment