
Na Mwandishi Wetu, Ruvuma
Mahakama ya Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma imemhukumu kijana mmoja mwenye umri wa miaka 20, James Hashimu Chingwaru, kifungo cha miaka 30 jela baada ya kupatikana na hatia ya kujaribu kumbaka bibi mwenye umri wa miaka 75.
Hukumu hiyo ilisomwa tarehe 16 Machi 2026 na Hakimu Mkazi Mfawidhi, F.M. Philip, katika Mahakama ya Wilaya ya Tunduru, baada ya ushahidi uliowasilishwa mahakamani kuthibitisha kosa hilo.
Kwa mujibu wa taarifa za mahakama, tukio hilo lilitokea tarehe 14 Desemba 2025 katika Kitongoji cha Nyerere, Kijiji cha Mtina, wilayani Tunduru. Baada ya tukio hilo, mtuhumiwa alikamatwa na kufikishwa mahakamani Januari 13, 2026 kwa hatua za kisheria.
Mshtakiwa huyo alipatikana na hataia chini ya kifungu cha 132(1) na 132(2)(a) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 (marejeo ya mwaka 2022), kinachohusiana na makosa ya kingono.
Mahakama ilisisitiza kuwa adhabu hiyo inalenga kutoa fundisho kwa jamii na kukomesha vitendo vya ukatili wa kijinsia, hasa dhidi ya watu walio katika mazingira hatarishi kama wazee
Leave a comment