Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Ilala, Mrakibu Mwandamizi wa Jeshi la Polisi (SSP) Salum Morimori, amewataka wamiliki wa magari ya kusafirisha wanafunzi kuhakikisha wanaajiri madereva wenye sifa stahiki ili kuimarisha usalama wa watoto barabarani.

Akizungumza hivi karibuni katika viwanja vya Shule ya Msingi Olimpio wakati wa zoezi la ukaguzi wa mabasi ya shule, Morimori alisema ni muhimu kwa wamiliki kufuata taratibu za kisheria wanapoajiri madereva.

Ukaguzi huo ulifanywa na Jeshi la Polisi kwa lengo la kuhakikisha magari hayo yanakidhi viwango vinavyotakiwa kwa usafirishaji wa wanafunzi.

“Ni lazima mmiliki ahakikishe dereva anayeajiriwa ana leseni halali, angalau ya daraja C au C1, pamoja na kukidhi vigezo vingine vya kisheria,” alisisitiza Morimori.

Aliongeza kuwa pamoja na sifa za dereva, wamiliki wanapaswa kuhifadhi kumbukumbu muhimu za madereva wao na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa magari yao ili kuepusha udanganyifu na kuwawajibisha wahusika pale matatizo yanapotokea.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Ilala, SSP Sarah Bundala, aliwataka madereva kuwa makini na maudhui wanayowawekea wanafunzi wanapokuwa safarini na kuwataka kuchagua maudhui yenye maadili mema na kuepuka nyimbo au vipindi vinavyoweza kuathiri tabia za watoto.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Shule ya Upanga, Abel Kasabalala, alilishukuru Jeshi la Polisi kwa kuitikia mwaliko wao na kufanya ukaguzi huo kwa kuwa imewasaidia kubaini hali halisi ya magari yao ili waweze kuchukua hatua stahiki kuboresha huduma ya usafiri kwa wanafunzi.

Ukaguzi huo ni sehemu ya jitihada za kuimarisha usalama wa wanafunzi na kuhakikisha wanapata usafiri salama na wenye kuzingatia sheria za barabarani.

Posted in

Leave a comment