Na Vincent Mpepo

Makundi sogozi ya mitandao ya kijamii kama WhatsApp, Telegramu ni matokeo ya maendeleo ya sayansi, teknolojia ya habari na mawasiliano na yamekuwa ni njia rahisi na yenye nguvu ya kuwasiliana na kushirikiana.

Ikumbukwe kuwa matumizi ya makundi haya huwa na taratibu zinazoongoza uendeshaji wake na wakati mwingine yanapaswa kuwekewa vigezo au masharti lakini muhimu zaidi ni kuzingatia madhumuni ya kimawasiliano bila kuathiri shughuli za msingi za jumuiya ya watu wa kundi husika.

Kwa mfano makundi ya taasisi binafsi kama shule za msingi na sekondari hususani binafsi huwa wanatoa maharti na wakati mwingine kuwa na viongozi wachache (admin) wenye ruhusa ya kushirikisha au kutoa taarifa ya jambo lolote kulingana na taasisi husika ikiwemo matangazo kuhusu shughuli za msingi za taasisi husika.

Kwa mfano wa taasisi za elimu nilizotaja hapo juu ambazo ni shule binafsi zinatumia makundi sogozi ili kutoa taarifa kuhusu mambo kadha wa kadha ikiwemo kuwakumbusha wazazi au walezi masuala ya ulipaji ada, usafiri wa watoto kwa shule zenye mabasi na taarifa nyingine muhimu. Wao wapo kibiashara na wanalinda taswira, hadhi na utambulisho wa taasisi zao.

Kwa kundi au makundi ya mitandao ya kijamii ya taasisi za kidini ikiwemo makanisa au taasisi za elimu za kikanisa mambo hayana tofauti sana.

Kwa aina ya makundi katika muktadha wa dini mambo ya msingi yanayozingatiwa ni masuala ya kidini na taarifa kuhusu taratibu zao kama vile kuimarisha Imani, maadili mema, misaada ya kijamii lakini pia kujenga umoja na mshikamano miongoni mwa waumini.

Katika majukumu ya ujumla makundi sogozi yanakusudiwa kuwa njia kuu ya mawasiliano, husaidia uratibu wa shughuli za kiofisi na utoaji wa taarifa na matukio pamoja na uwasilishaji wa mipango mbalimbali.

Hatahivyo, wahusika wanapaswa kuzingatia maudhui yasiende nje na lengo mama. Sanjali na hilo, jamii ya watu katika makundi haya siyo tu wakristo wanaotegemea neno la Mungu pekee, ni sehemu ya jamii yenye mipango na shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.

Kwa minajiri hiyo, ni muhimu kuwa tayari na kukubali faida ya uwepo pamoja kuwa ni fursa inayoweza kutumika kwa matokeo chanya kwa wahusika kuweka na kushirikishana fursa walizonazo ili kuapata wateja miongoni mwao au hata nje ya wao lakini kupitia wao.

Sidhani kama ni dhambi mtu kutoa taarifa ya biashara yake, au aina fulani ya shughuli inayoweza kumsaidia kupata kipato.

Vinginevyo hatuwezi kuliishi neno la Mungu ikiwa tutajitenga na shughuli za kimwili ambazo zinasaidia ustawi wa mwanajamii husika katika kundi.

Tukizungumzia dhana ya upatikanaji wa bidhaa au huduma na usambazaji naweza kuwa msharika wa kundi fulani ambalo lina washarika taja idadi yoyote na wanaweza kuwa ni miongoni mwa wahitaji wa huduma au bidhaa za msharika mwenzao lakini anawapaje taarifa kuhusu huduma zake?

Maudhui haya yanarandana na maoni yaliyotolewa na viongozi mbalimbali wa dini waliohojiwa na mwandishi juu ya matumizi ya makundi sogozi katika jamii. Viongozi hao wa dini walikuwa na maoni tofauti kuhusu jambo hili.

Mchungaji Kiongozi wa Kanisa Kuu la Kiinjili Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Dodoma, Daniel Sailowa anasema makundi haya ya WhatsApp ni muhimu kwa kuwa yanawaleta waumini wote na yanasaidia katika upokeaji wa taarifa zinazohitaji utekelezaji wa masuala mbalimbali ndani ya kanisa.

“Siyo ya kutoa na kupokea bali ni ya kupokea na kutekeleza, ndiyo maana yana viongozi wasimamizi (admin) wachache walioruhusiwa kushirikisha taarifa”, alisema Mchungaji Sailowa.

Alisema kutokana na kuwapa fursa wasimamizi wachache kushirikisha taarifa wamejitenga na changamoto ya kila mmoja kutoa taarifa na kuna taarifa zinaleta shida mpaka kutafuta ufumbuzi wake tayari kuna athari hivyo ni muhimu kuwa na vizuizi.

Mchungaji Sailowa anashauri kuwepo na makundi mengine madogomadogo yanaweza kuwa ya vijana, akina mama au akina baba ambayo yanaweza kutumika kwa taarifa nyingine na kuacha kundi kubwa kuhusika na dhima kuu za kikanisa.

Kwa upande wake, Mhadhiri Mwanadamizi wa Masuala ya Mawasiliano, Dr. Francis Ng’atigwa anasema masuala ya matangazo ya biashara katika makundi ya WhatsApp ya watu wa kanisa au jamii yoyote yanapaswa kuwa na makubaliano na uelewa na sheria za mitandao.

Wakati mwingine makubaliano ndiyo yaongoze namna ya kuwasilisha matangazo na labda wakati mwingine wangine wasiwe tu wakali sana, anasema Dr. Ngatigwa.

Mwandishi anaona kuwa kwa hali halisi na namna jamii ya sasa ilivyo na teknolojia ilipofikia hatuwezi kujitenga na masuala ya kijamii au kimwili hata kama waumini tulio kiroho. Kuna namna maisha yetu ya kiroho yanahusiana na ya kimwili.

Makundi ya WhatsApp ya kidini ni njia rahisi ya kuimarisha imani, kujifunza, na kusaidiana kiroho, lakini yanahitaji matumizi ya hekima ili yawe na manufaa kwa kila mtu ndani ya kundi husika. Zaidi yanapaswa kutmika kwa nidhamu na uwajibikaji ili kuepuka usumbufu au taarifa zisizo sahihi.

Posted in

Leave a comment