Na Mwandishi Wetu, Pwani

Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia kutoka Mkoa wa Pwani, wakiongozwa na Sajini Taji Wandwi Patrick, wametoa msaada kwa watoto wanaolelewa katika Kituo cha kulea wahitaji cha Buloma kilichopo Wilaya ya Kibaha, Mkoa wa Pwani.

Tukio hilo limefanyika leo ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa matendo ya huruma kwa jamii, hususan katika kipindi hiki kinachoelekea kwenye sikukuu za Eid na Pasaka ili kurudisha kwa jamii, kuonesha upendo, na kuleta faraja kwa watoto wahitaji.

Katika zoezi hilo, askari hao walikabidhi bidhaa mbalimbali muhimu za matumizi ya kila siku kwa watoto hao ikijumuisha unga wa sembe, wa ngano, sukari, chumvi, mafuta ya kula na ya kupaka.

Bidhaa nyingine zilizokabidhiwa ni sabuni, taulo za kike, mchele, biskuti, sharubati, maji ya kunywa, nguo na viatu pamoja na na fedha taslimu

Msaada huu unatarajiwa kusaidia kuboresha hali ya maisha ya watoto hao na kukidhi baadhi ya mahitaji yao ya msingi.

Akizungumza wakati wa kupokea msaada huo, mlezi wa kituo hicho, Baraka Kyando, alilishukuru Jeshi la Polisi pamoja na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani kwa kuruhusu askari kushiriki katika tendo hilo la huruma.

Alisema msaada huo ni muhimu sana kwa kituo hicho na kwamba utasaidia kukidhi mahitaji ya watoto wanaolelewa hapo.

“Hili ni jambo jema na la kupongezwa na tunawashukuru sana kwa upendo wao, na tunawaombea baraka zaidi ili waendelee kusaidia wengine”, alisema Kyando.

Tendo hili linaonesha umuhimu wa ushirikiano kati ya vyombo vya usalama na jamii, na nafasi yao katika kusaidia makundi yenye uhitaji maalum na unatajwa kama mfano mzuri wa kuigwa unaohamasisha mshikamano, upendo, na uwajibikaji wa kijamii.

Kadri jamii inavyoelekea kwenye sikukuu, matendo kama haya yanakumbusha umuhimu wa kushirikiana na kuwajali wale wanaohitaji msaada zaidi.

Posted in

Leave a comment