
Na Cosmas Msuha
Tanzania imepiga hatua muhimu katika sekta ya madini baada ya kusaini makubaliano ya kimkakati na Marekani kwa ajili ya kuendeleza mradi wa madini ya Niobium wa Panda Hill. Hatua hii inalenga kuifanya Mbeya kuwa kitovu cha uzalishaji na usindikaji wa madini hayo adimu duniani.
Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini jijini Mbeya, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, alieleza kuwa mradi huo ni wa kipekee kutokana na umuhimu wa madini ya Niobium, ambayo hayapatikani kwa wingi duniani.
Alisisitiza kuwa Tanzania inalenga kujipatia nafasi ya kipekee katika soko la kimataifa kwa kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa madini hayo.
“Tanzania inalenga kuwa mzalishaji wa nne duniani kwa kuchangia takriban asilimia 4 ya mahitaji ya dunia, ikiwa na uzalishaji unaolengwa kufikia tani 100,000 kwa mwaka,” alisema Mavunde.
Kwa sasa, Brazil inaongoza kwa kuzalisha takriban asilimia 80 ya mahitaji ya dunia, ikifuatiwa na mzalishaji mwingine kutoka Brazil (asilimia 11), huku Canada ikichangia takriban asilimia 6.
Serikali imeeleza kuwa kupitia dira ya maendeleo ya mwaka 2025–2050, inalenga kuhakikisha madini yanachakatwa na kuongezewa thamani ndani ya nchi badala ya kusafirishwa ghafi ili kukuza ajira, kuongeza mapato ya taifa na kujenga viwanda vyenye ushindani wa kimataifa.
Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Panda Hill Tanzania Limited, Dennis Cook, alisema mradi huo umeingia hatua mpya ya utekelezaji baada ya maandalizi ya muda mrefu.

Alisema hatua zinazofuata ni pamoja na kupata Leseni Maalum ya Uchimbaji Madini, kuunganisha mradi na umeme wa gridi ya taifa na kufanya tathmini ya masoko ya bidhaa ya ferroniobium.
“Mradi utahusisha ujenzi wa mgodi wa Niobium, kituo cha uchenjuaji na kiwanda cha kuzalisha ferroniobium”, alisema Cook..
Kupitia mradi huu, Tanzania itakuwa mshiriki wa moja kwa moja katika minyororo ya ugavi ya viwanda vya kimataifa vinavyotumia teknolojia za hali ya juu—hatua inayoweza kubadilisha mwelekeo wa uchumi wa nchi.
Katika hafla hiyo, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Samwel Maneno, pamoja na Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, walitia saini mkataba wa wanahisa kwa niaba ya serikali. Hatua hii imekamilisha rasmi muundo wa ushiriki wa serikali na mfumo wa usimamizi wa mradi.
Mradi wa Niobium wa Panda Hill unaashiria mwanzo wa enzi mpya kwa Tanzania katika sekta ya madini. Ikiwa utatekelezwa kwa ufanisi, unaweza kuiweka nchi katika nafasi ya kipekee duniani na kuifanya kuwa kitovu cha uzalishaji wa madini ya kimkakati yenye thamani kubwa.
Niobium ni madini ya kimkakati yanayotumika kuongeza uimara wa chuma na kutengeneza aloi maalum zenye utendaji wa juu. Madini haya ni muhimu katika ujenzi wa miundombinu mikubwa, sekta ya anga na usafiri na teknolojia za kisasa na viwanda vya hali ya juu na hii inaifanya Niobium kuwa rasilimali yenye thamani kubwa katika uchumi wa kisasa wa dunia.
Leave a comment