
Na Cosmas Msuha
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, amewataka wanahabari wanawake nchini kushirikiana kwa karibu na jamii ili kusaidia kuinua sauti ya mwanamke kupitia vyombo vya habari.
Akizungumza katika Kongamano la “Malkia wa Habari” lililofanyika Machi 28, 2026 katika Ukumbi wa Hoteli ya Rungwe, Sinza jijini Dar es Salaam, Kairuki alisisitiza kuwa mchango wa wanahabari wanawake ni muhimu sana katika kushughulikia changamoto mbalimbali za kijamii, hususan zinazowahusu wanawake.
Alieleza kuwa kalamu za wanahabari zina nguvu kubwa na zinaweza kuwa daraja la kuunganisha wananchi na serikali katika kutatua matatizo yaliyopo kwenye jamii.
“Zipo fursa nyingi katika tasnia ya habari na mawasiliano, hivyo wanawake mnapaswa kuzichangamkia. Serikali ipo tayari kutoa ushirikiano,” alisema Kairuki.
Aidha, aliwahimiza wanahabari wanawake kusimamia kikamilifu vikundi na vyama wanavyoanzisha ili viweze kuleta matokeo chanya, pamoja na kujenga umoja utakaowezesha kutambulika rasmi na serikali.
Kwa upande wake, Mratibu wa kongamano hilo, Penina Malundo, alisema lengo la mkutano huo ni kujadili changamoto zinazowakabili wanahabari wanawake, kuimarisha ushirikiano wa kijamii, na kuinua sauti ya wanawake kupitia vyombo vya habari.
Naye Mhariri wa Habari za Siasa wa gazeti la Mwananchi, Lilian Timbuka, aliwataka wanahabari wanawake kuwa na juhudi binafsi katika kutafuta maarifa badala ya kusubiri mafunzo rasmi pekee.
Kwa upande mwingine, mmoja wa wahariri wa Clouds Media, Joyce Shebe, aliwashauri wanawake kujifunza mbinu mbalimbali za kukabiliana na taarifa hasi zinazosambaa mitandaoni.
Naye Mhariri wa Habari wa gazeti la Tanzania Leo, Marry Geofrey, alisema kongamano hilo limewapa fursa wanahabari wanawake kujadili na kueleza changamoto zao wazi, pamoja na kubadilishana uzoefu.
Kwa ujumla, kongamano hilo limeonyesha umuhimu wa mshikamano miongoni mwa wanahabari wanawake katika kuleta mabadiliko chanya ndani ya tasnia ya habari na jamii kwa ujumla.
Top of Form
Leave a comment