Na Mwandishi Wetu

Tanzania inaelekea kufungua ukurasa mpya katika sekta ya madini kufuatia mipango ya kuendeleza uchimbaji wa madini ya niobium katika eneo la Panda Hill, mkoani Mbeya.

Madini haya adimu yana umuhimu mkubwa duniani kutokana na matumizi yake katika kuimarisha chuma, sekta ya anga, pamoja na teknolojia za kisasa.

Akizungumzia maendeleo hayo, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema kuwa mradi huo ni hatua muhimu katika kuiweka Tanzania kwenye ramani ya wazalishaji wa madini ya kimkakati duniani.

Alisema serikali imejipanga kuhakikisha kuwa rasilimali hizo zinaleta manufaa makubwa kwa wananchi kupitia ajira, mapato, na maendeleo ya viwanda.

Kwa upande wake, Patrick Cook, ambaye ni kiongozi wa kampuni ya Peak Rare Earths inayohusika na mradi huo, amesema kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na wadau wa kimataifa unaimarisha uwezekano wa kufanikisha mradi wa Panda Hill.

Alisema mradi huo una uwezo wa kuiweka Tanzania katika nafasi ya nne duniani kwa uzalishaji wa niobium.

Mradi huo unatarajiwa kujumuisha ujenzi wa mgodi, kituo cha uchenjuaji pamoja na kiwanda cha kuzalisha ferroniobium, bidhaa yenye thamani kubwa zaidi sokoni.

Hatua hii inalenga kuongeza thamani ya madini ndani ya nchi badala ya kuyauza ghafi.

Aidha, serikali kwa kushirikiana na wawekezaji inaendelea kukamilisha taratibu muhimu ikiwemo upatikanaji wa umeme, miundombinu, na leseni maalum za uchimbaji ili kuhakikisha mradi unaanza kwa wakati na kwa ufanisi.

Kwa ujumla, mradi wa niobium wa Panda Hill unatarajiwa kuwa chachu ya mageuzi ya kiuchumi nchini, na kuifanya Tanzania kuwa na nafasi ya kipekee katika soko la kimataifa la madini adimu huku ukichochea maendeleo endelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Posted in

Leave a comment