

Na Mwandishi Wetu, Nachingwea – Lindi
Chama Kikuu cha Ushirika (RUNALI), kinachojumuisha wilaya za Nachingwea, Ruangwa na Liwale, kimetoa mafunzo kwa viongozi wa vyama vya ushirika vya msingi (AMCOS) kutoka katika wilaya hizo, yakilenga kuongeza ufanisi na kuimarisha mipango ya vyama hivyo.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo jana kwa naiba ya Mkuu wa Mkoa, wilayani Liwale, Mkuu wa Wilaya hiyo, Goodluck Milinga alisema yatachangia kuboresha utendaji na uwajibikaji wa viongozi na wanachama wa vyama vya ushirika.
DC Milinga aliwamewapongeza wanachama wa ushirika kwa juhudi wanazozifanya katika kuendeleza sekta hiyo, huku akisisitiza umuhimu wa matumizi sahihi ya rasilimali fedha ili kuhakikisha maendeleo endelevu yanapatikana.
A;isema mipango bora ni msingi muhimu katika kuelekeza mustakabali wa AMCOS, na kuonya dhidi ya kuchukua madeni yasiyo na tija pamoja na kuepuka migogoro isiyo ya lazima ndani ya vyama.
Kwa upande wake, Mrajisi wa Ushirika Mkoa wa Lindi, Keneth Shemdoe, alisema RUNALI inaendelea kuimarisha sekta ya ushirika kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa hoteli na ukumbi wa kisasa kwa ajili ya mikutano na mafunzo.
Alisema mradi wa ujenzi wa hoteli utachochea ukuaji wa uchumi wa eneo hilo kwa kuongeza fursa za huduma kwa jamii na kuzalisha ajira.
Aidha, alivitaka vyama vya ushirika kuongeza mtaji wa hisa hadi kufikia angalau asilimia 51 ili kuhakikisha wanachama wengi zaidi wanashiriki kikamilifu katika umiliki na uwekezaji.
Naye Mwenyekiti wa RUNALI, Odas Mpunga, alisema ushirika ni biashara, hivyo vyama vinapaswa kuendeshwa kwa misingi ya kibiashara ili kuongeza tija huku akibainisha kuwa baadhi ya vyama tayari vinamiliki mali kama magari ya mizigo, hatua inayoonesha ukuaji wa sekta hiyo.
Kwa upande wao, baadhi ya wawakilishi wa AMCOS wameipongeza RUNALI kwa kuandaa mafunzo hayo kwani yatawasaidia kuboresha utendaji wao, usimamizi wa fedha, na mipango ya maendeleo ya vyama vya vyao.


Leave a comment