Na Yusra Temba

Wahudumu wa afya 58 wamehitimu mafunzo ya muda mfupi ya kipimo cha moyo kwa kutumia teknolojia ya Echo (Echocardiography), katika mahafali yaliyofanyika Ijumaa, tarehe 27 Machi, jijini Dar es Salaam.

Mafunzo hayo yameandaliwa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili kwa kushirikiana na Hospitali ya Taifa Muhimbili pamoja na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete. Programu hiyo imelenga kuimarisha ujuzi na weledi wa wahudumu wa afya katika uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mgeni rasmi ambaye ni Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Appolinary Kamuhabwa, aliwapongeza wahitimu kwa kujituma kwao na kusisitiza umuhimu wa kutumia maarifa waliopata kuboresha huduma za afya kwa wananchi.

Kwa upande wake, Mratibu Mkuu wa mafunzo hayo, Profesa Pilly Chillo, alisema mafunzo hayo yameandaliwa kwa kuzingatia mahitaji halisi ya sekta ya afya.

Alisema dhamira ya chuo ni kuendelea kutoa mafunzo bora yatakayochangia kuinua viwango vya huduma za afya nchini.

Mahafali hayo yalifanyika katika viunga vya chuo hicho, yakihitimisha rasmi programu iliyolenga kujenga uwezo wa wataalamu wa afya. Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa chuo, wakufunzi pamoja na wahitimu wenyewe.

Katika hotuba mbalimbali, umuhimu wa kujifunza na kuzingatia maadili ya taaluma ya afya vilisisitizwa kama nguzo muhimu katika kuboresha huduma kwa jamii.

Posted in

Leave a comment