Na Cosmas Msuha

Katika juhudi za kupunguza ajali za barabarani zinazohusiana na kazi, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) umesaini makubaliano ya ushirikiano na Chuo cha Usafirishaji cha Taifa (NIT) jijini Dar es Salaam.

Ushirikiano huo unalenga kuimarisha usalama barabarani na kupunguza athari zake kwa wafanyakazi pamoja na uchumi wa taifa.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma, alibainisha kuwa sehemu kubwa ya madai ya fidia yanayotolewa na mfuko huo yanatokana na ajali za barabarani.

“Sehemu kubwa ya madai ya fidia tunayopokea yanatokana na ajali za barabarani, hususan kwa madereva na wafanyakazi wanaotumia usafiri kwenda na kutoka kazini”, alisema Dkt.Mduma.

Alisema kupitia makubaliano hayo, taasisi hizo mbili zitashirikiana katika maeneo muhimu ikiwemo utoaji wa mafunzo, elimu ya usalama barabarani, kufanya tafiti, kubadilishana taarifa pamoja na kujengeana uwezo wa kitaalamu.

“Ushirikiano huu utasaidia kuongeza uelewa na uwezo wa kitaalamu katika kukabiliana na ajali za barabarani nchini”, alisema Dkt.Mduma.

Kwa upande wake, Mkuu wa NIT, Dkt. Prosper Mgaya, alisema ushirikiano huo unaashiria hatua muhimu katika kupunguza ajali za barabarani ambazo zimeendelea kuwa tatizo kubwa nchini.

“Hii ni hatua muhimu katika juhudi za pamoja za kukabiliana na changamoto ya ajali za barabarani”, alisema Dkt.Mgaya.

Alirejea takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinazoonesha kuwa takribani watu milioni 1.19 hupoteza maisha kila mwaka duniani kutokana na ajali za barabarani huku akifafanua zaidi kuwa nchi zinazoendelea kama Tanzania, ajali hizi husababisha hasara ya kati ya asilimia 3 hadi 5 ya Pato la Taifa kutokana na kupotea kwa nguvu kazi na gharama nyingine za kiuchumi.

Kwa ujumla, ushirikiano huo unatarajiwa kusaidia kupunguza ajali za barabarani, kulinda maisha ya wafanyakazi, kuimarisha nguvu kazi ya taifa na kuboresha ustawi wa jamii kwa ujumla.

Posted in

Leave a comment