Na Farida Mkumba, Dodoma

Hospitali ya Afya ya Akili ya Taifa Mirembe imeombwa kuimarisha ushirikiano na taasisi binafsi ili kuwezesha tathmini ya watoto wenye usonji kufanyika kila robo mwaka, hatua itakayosaidia kuboresha huduma za matibabu na ufuatiliaji wa karibu.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Msaidizi wa Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza, Dkt. Omary Ubuguyu, kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Usonji Duniani yaliyofanyika leo katika Hospitali ya Mirembe mkoani Dodoma.

Dkt. Ubuguyu aliipongeza hospitali hiyo kwa juhudi zake katika kutoa huduma kwa watoto wenye changamoto ya usonji, na kusisitiza umuhimu wa kuendelea kushirikiana na taasisi binafsi ikiwemo shule maalum ili kuboresha zaidi huduma hizo kwa jamii.

Alieleza kuwa ushirikiano huo utaiwezesha Mirembe kutoa huduma bora zaidi na kuwasaidia watoto wenye usonji kupata matibabu sahihi kwa wakati.

Kwa upande wake, Afisa Elimu Maalum wa Jiji la Dodoma, Issa Kambi, alisema halmashauri inaendelea kuwabaini watoto wenye usonji ili kuwaingiza katika mfumo wa bima ya afya kwa wote, hatua itakayorahisisha upatikanaji wa huduma za matibabu.

Aliongeza kuwa lengo ni kuhakikisha watoto hao wanapata huduma bora za afya pamoja na elimu inayokidhi mahitaji yao.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Mirembe, Dkt. Godwin Mwisomba, alisema hospitali hiyo inaendelea kushirikiana kwa karibu na jamii ili kukuza uelewa, kuonesha upendo na kuhakikisha huduma bora za afya ya akili zinawafikia wananchi wengi zaidi.

Maadhimisho hayo yalifanyika katika Hospitali ya Mirembe, Dodoma, yakiwa na lengo la kuongeza uelewa wa jamii kuhusu usonji na kuhamasisha mazingira jumuishi kwa watu wenye hali hiyo.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni: “Weka Tumaini Usoni Mwao, Furahia Utofauti.”

Posted in

Leave a comment