Na Mwandishi Wetu, Ruvuma

Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma linamshikilia mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Michael Ngonyani (38), mkazi wa Mtyangimbole, kwa tuhuma za kujihusisha na uhalifu mbalimbali ikiwemo wizi wa magari katika Mkoa wa Mbeya.

Akizungumza kuhusu tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Marco Chilya, alisema kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa Machi 31, 2026 katika kijiji cha Mtyangimbole, Halmashauri ya Madaba.

Kwa mujibu wa Kamanda Chilya, baada ya kufanyika upekuzi katika makazi ya mtuhumiwa, polisi walifanikiwa kukamata mali mbalimbali zinazodhaniwa kuwa za wizi.

Miongoni mwa mali hizo ni gari aina ya Toyota IST lenye namba za usajili T 829 DYH, leseni nne za udereva zenye majina tofauti, pamoja na vifaa vya kielektroniki ikiwemo sound bar aina ya Skywood, runinga mbili zenye ukubwa wa inchi 65 na 55, pamoja na pampu ya maji.

Aidha, katika upekuzi huo, mtuhumiwa alikutwa na sare za vyombo vya ulinzi na usalama, zikiwemo sare za Jeshi la Polisi (kaki) jozi moja, pamoja na sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambazo ni suruali moja na fulana moja.

Kamanda Chilya alieleza kuwa inaaminika mtuhumiwa huyo alikuwa akitumia sare hizo kujifanya askari ili kurahisisha kutekeleza vitendo vya uhalifu katika maeneo mbalimbali.

Aliongeza kuwa uchunguzi bado unaendelea ili kubaini namna mtuhumiwa alivyoweza kupata sare hizo na mtandao wake wa uhalifu, kabla ya kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Posted in

Leave a comment