• Na Vincent Mpepo, Kwembe

    Wataalamu mbalimbali wanaoishi na kufanya kazi katika Mtaa wa Kwembe Ubungo Jijini Dar es salaam wamebainisha fursa na changamoto mbalimbali za kimaendeleo katika Mtaa huo huku huduma za jamii na miundombinu zikitajwa.

    Hayo yamejitokeza katika mkutano wa kwanza wa serikali ya Mtaa uliofanyika jana katika ofisi za mtaa huo jana huku fursa na changamoto mbalimbali zikitajwa katika kuchochoea au kurudisha nyuma maendeleo ya Mtaa huo.

    Akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kwembe Rajabu Koba alisema ni wakati sasa Wananchi kuamka kuunganisha nguvu zao, kwa kuishauri serikali yao kwa hoja madhubuti ili kwa ushirikiano zifanyiwe kazi kwa manufaa ya Mtaa huo.

    Alitaja vipaumbele vya serikali yake kuwa ni pamoja na ujenzi wa Shule ya Msingi Kwembe ili kupunguza mrudikano wa watoto katika madara yaliyopo ambayo hayatoshi na Kituo cha polisi ili kuimarisha ulinzi na usalama.

    “Vipaumbele vingine ni pamoja na kuimarisha ulinzi na usalama kupitia ulinzi shirikishi, kubadili matumizi ya eneo la soko kuwa machinjio na mnada wa mifugo”, alitaja Koba.

    Aliongeza vipaumbele vingine kuwa ni kukamilisha ujenzi wa ofisi ya serikali ya Mtaa huo na masuala ya urasimishaji ardhi katika Mtaa huo.

    Akizungumzia ajenda ya ulinzi na usalama aliwataka Wananchi kwenye mitaa na zone mbazo bado hazijaanzisha ulinzi shirikishi kufanya hivyo ili kutowapa wezi na wadokozi fursa ya kuwaibia.

    “Ulinzi shirikishi ni kwa ajili ya kuwanyima fursa wezi na wadokozi kujipatia kipato au faida kwa kazi isiyo halali”, alisema Koba.

    Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kwembe, Lwitiko Mwakisole alisema changamoto kubwa inayoikabili shule yake ni uhaba wa madarasa ya kusomea na madawati ambao hauendani na idadi ya wanafunzi waliopo matokeo yake bbadhi ya wanafunzi kulazimika kusomea nje na kukaa chini.

    “Shule ya Msingi Kwembe ina wanafunzi zaidi ya 2000 huku miundombinu ya madarasa tuliyonayo ni 12 tu”, alisema Mwalimu Mwakisole.

    Aliwaasa wazazi kutembelea shule yao ili kujionea uhalisia wa kinachosemwa ili waweze kufanya maamuzi sahihi katika kuboresha miundombinu ya shule hiyo kwa maslahi ya kizazi cha wanakwembe.

    Akizungumzia malezi, Mwakisole alisema kumekuwa na changamoto za malezi katika jamii na familia kutokana na baadhi ya walezi na wazazi kutokubali watoto wao kuadhibiwa suala ambalo linaleta mustakabali mbaya kwa jamii na kizazi cha sasa.

    “Kimsingi, tukubali kuna changamoto za malezi zinazotokana na malezi mabovu katika familia zetu hivyo kusababisha watoto wenye tabia mbaya”, alisema Mwalimu Mwakisole.

    Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Amani, Dkt.Nikodemus Ngwembe aliwataka Wananchi wa mtaa huo na mitaa ya jirani kukitumia kituo hicho ambacho kinapandishwa hadhi na kuwa Kituo cha Afya kutoka Zahanati kwa kuwa mindombinu inaboreshwa ili kuendana na hadhi hiyo.

    “Kwa sasa kituo chetu kimejenga jengo la wazazi kwa gharama ya Tsh milioni 300 ambalo lina vitanda 30 huku vitanda vya chumba cha wazazi ni 10inatoa huduma masaa 24 na ina vitanda 10”, alisema Dkt. Ngwembe.

    Alisema kwa sasa kituo hicho kinaendelea na ujenzi wa wodi ya upasuaji na kwamba kitahudumia kata ya Kwembe na Kibamba huku mashine na mitambo mingine ikiwemo Utra-Sound ikiwa mbioni kuletwa katika kituo hicho ambayo imegharimu Tsh milini 22.

    Akizungumzia masuala ya urasimishaji ardhi katika Mtaa huo, Mkandarasi Demetrius Sangu alisema tangu zoezi hilo lianze tayari wameshatambua viwanja 4015 na viwanja vilivyopangwa kwa mujibu wa ramani ya mipango miji ni 6207 wakati viwanja vilivopata namba za ploti ni 2116 wakati ni viawanja 20 pekee ambavyo bado havijapandwa mawe.

    “Changamoto za kuendelea na zoezi hili ikiwemo upandaji wa mawe unatokana na uhaba wa fedha”, alisema Mkandarasi Sangu.

    Aidha, uchunguzi uliofanywa na mwandishi umebani kuwa kuchelewa kwa zoezi la urasimishaji kumetokana na sababu mbalimbali ikiwemo kuzorota kwa uchangiaji wa fedha kwa wananchi kutokana na kukosa hamasa au matamko mbalimbali ya serikali kwa nyakati zilizopita.

  • Na Vincent Mpepo, Kwembe

    Eneo ambalo lililopangwa kutumika kama soko limebadilishwa matumizi na kuwa machinjio na mnada wa mifungo kitu kinachotajwa kitaongeza idadi ya wasafiri kuja na kutoka mtaani hapo na kuchochea maenedeleo ya Mtaa wa Kwembe Ubungo jijini Dar es salaam.

    Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa Mtaa wa Kwembe Rajabu Koba wakati wa mkutano wa wa kwanza wa wananchi uliofanyika jana katika ofisi za mtaa huo ambapo masuala mbalimbali yalijadiliwa huku kubadili matumizi kwa eneo la soko na urasimishaji ardhi zikiwa ni ajenda ambazo zilivuta makini ya wananchi wa mtaa huo.

    Koba alisema maamuzi ya kubadili matumizi ya eneo hilo kuwa machinjio na mnada limefikiwa kufuatia vikao na kamati mbalimbali za mtaa huo na limewasilishwa kwa diwani ili kwenda kwenye ngazi za juu kwa maamuzi zaidi na kwamba tangu lilipofanywa kama soko hakuna kilichofanyika mpaka sasa.

    Alisema maamuzi ya kubadili eneo matumizi limezingatia vitu vingi ikiwemo uboreshaji wa miundombinu ambayo itavutia wafanyabiashara ya usafirishaji kama daladala kuja na kutoka kutokana na abiria wakakaokuja kwa shughuli mbalimbali za kibiashara.

    “Ili kupata abiria wa kutosha lazima kuwe na eneo ambalo litavuta watu kuja na kutoka huku pia miundombinu yetu ikiwa imeboreshwa”, alisema Koba.

    Aidha aliwataka wananchi wa Mtaa huo kuchangamkia fursa za ujasiriamali katika mradi mkubwa unaotarajiwa kuanza hivi karibuni katika eneo la Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kampasi ya Mloganzila.

    “Wanacnhi wa maeneo jirani wajiandae kwa kazi mbalimbali ikiwemo vibarua na ujasiriamali kama mama lishe katika mradi huo”, alisema Koba.

    Alisema fursa hizo ni matokeo ya utekelezaji wa Mradi wa Elimu ya juu kwa Mageuzi ya Kichumi unaofadhiliwa na Benki ya Dunia unahusisha ujenzi wa majengo sita ambapo tayari kandarasi zimekwishatolewa kwa makampuni mawili na utagharimu kiasi cha dola za kimarekani milioni 30.5.

    Mtendaji wa Mtaa huo, Kennedy Kuwendwa alisema Wananchi wa mtaa huo wajenge utaratibu wa kwenda ofisini ili kupata taarifa sahihi na kutoa taarifa mbalimbali kwa kero ili zifanyiwe kazi badala ya kupeana maneno mitaani ambayo wakati mwingine hayana uhakika.

    “Ninawashukuru Wananchi wa mtaa huu na nitoe rai ikiwa kuna jambo hulielewi njoo ofisini utasaidiwa kupata ufumbuzi”, alisema Kennedy.

    Afisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Kwembe, Bi Ramla Mustafa aliwakumbusha wananchi wa mtaa huo kuhusu fursa za mikopo asilimia kumi (10%) ambayo hutolewa na serikali kupitia Halmashauri ya Ubungo kwa wanawake, vijana na wenye ulemavu.

    Vigezo vya kuapata mikopo hiyo ni mtu mwenye umri wa miaka 18 hadi 45 na mwenye Uwezo wa kufanya kazi na kujiingizia kipato, alisema Bi Ramla.

    Mkutano huo ulikuwa na ajenda nyingine ikiwemo ujenzi wa Shule ya Msingi Kwembe, Ujenzi wa Kituo cha Polisi, Suala la Ulinzi Shirikishi na umaliziaji wa ofisi ya mtaa huo.

    Hata hivyo uchunguzi wa mwandishi umebaini kutokuwepo kwa hamasa ya kutosha ya Wananchi kushiriki katika mikutano ya mtaa huo suala linalotajwa limetokana na taarifa kutowafikia Wananchi.

  • Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga akiteta jambo na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) Mhandisi. Charles Sangweni (kushoto). Kulia ni Katibu wa Baraza Baraza la Wafanyakazi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli ( PURA) Ebeneza Mollel wakati wa Kikao cha Baraza hilo kilichofanyika hivi karibuni mkoani Morogoro.

    Morogoro

    Serikali imeitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) kuendelea kuvutia  uwekezaji katika vitalu vilivyo wazi vya mafuta na gesi asilia ili kuongeza kiasi cha nishati hiyo nchini.

    Kauli hiyo ilitolewa mwanzoni mwa wiki na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga wilayani Morogoro, Mkoa wa Morogoro wakati akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) kilicholenga kujadili  mipango na bajeti ya taasisi hiyo kwa mwaka  wa fedha 2025/26.

    Alisema mamlaka hiyo ikifanikiwa kuvutia wawekezaji wa utafutaji wa mafuta na gesi nchi itaongeza ugunduzi wa rasilimali hiyo muhimu ikiwa ni pamoja na kufikia futi za ujazo wa gesi  inayopatikana nchini.

    “Mkiendelea kuvutia uwekezaji kupitia Duru ya Tano ya kunadi vitalu itakayozinduliwa mwezi Machi mwaka huu pamoja na faida zilizopo mtakuwa mmeendeleza jitihada za serikali kuifungua Tanzania kiuchumi na kuvutia uwekezaji zaidi”, Alisema Kapinga.

    Alisema wizara inatambua umuhimu wa tukio la Duru ya Tano ya kunadi vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini pamoja na kutambua kazi kubwa ambayo imekwishafanyika kuelekea uzinduzi wa tukio hilo muhimu.

    “Kwa muda mrefu tumekuwa tukizungumzia ugunduzi wa futi za ujazo trilioni 57.54 pekee wakati umefika ili kuongeza ugunduzi wa rasilimali hii muhimu kwa maendeleo ya Taifa”,Alisema Kapinga

    Aidha, aliupongeza uongozi wa uongozi wa PURA kwa kuendelea kuwashirikisha watumishi wake katika kujadili, kupanga na kupitisha mipango na bajeti ya taasisi hiyo kwa uwazi kupitia baraza hilo ikiwa ni utekelezaji wa Sheria ya Majadiliano ya Pamoja katika Utumishi wa Umma.

    Alisema kufanyika kwa vikao hivyo ni ishara tosha ya utawala bora mahala pa kazi kwa kuwa watumishi wanapata fursa ya kuchangia mawazo yao kuhusu uendeshaji wa taasisi hivyo kuendelea kuwa ni sehemu muhimu ya taasisi.

    Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) Mhandisi. Charles Sangweni, alisema duru ya tano (5) ya kunadi vitalu vya utafutaji wa mafuta na

    gesi asilia nchini inatarajiwa kuzinduliwa mwezi Machi, 2025 Jijini Dares salaam wakati wa Kongamano na Maonesho ya Petroli ya Nchi Wanachama wa Afrika Mashariki (EAPCE’25).

    Alisema PURA itaendelea kusimamia na kudhibiti shughuli za utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa gesi asilia katika vitalu mbalimbali nchini ili kuhakikisha watanzania wazawa wanashirikishwa kikamilfu kwenye miradi mbalimbali ya mkondo wa juu wa petroli nchini.

    Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga (katikati) katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli( PURA) wakati wa Kikao cha Baraza hilo kilichofanyika Tarehe 18 na 19 Februari 2025, mkoani Morogoro. Kushoto Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) Mhandisi. Charles Sangweni.

  • Mwalimu Bupe Mwabenga akifundisha  wakati ibada ya Jumapili katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Mtaa wa Kwembe jijijini Dar es salaam

    Na Vincent Mpepo, Kwembe

    Wanandoa wamekumbushwa kuishi kwa kadiri ya mpango wa maagizo ya Mungu ili kuepuka migogoro inayotokana na mwingiliano wa majukumu kati yao.

    Wito huo umetolewa Jumapili  na Mwalimu Bupe Mwabenga wakati akifundisha katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Mtaa wa Kwembe na kubainisha kuwa sababu mojawapo ya migogoro katika ndoa ni kwa baadhi ya wanandoa kutoishi kwa utaratibu uliowekwa na Mungu.

    Alisema si vibaya kwa wanandoa kuamua kusaidiana majukumu lakini kusaidiana huko kuwe katika utaratibu ambao unatambua haki na wajibu wa kila mwanandoa ili kupata tafsiri sahihi ya anayesaidia na anayesaidiwa.

    “Wanawake wamejengewa uwezo, wamewezeshwa na wanatambua haki zao hatahivyo bado haiwapi nafasi ya kuwa wanaume”, alisema Mwalimu Mwabenga.

    Aliikumbusha jamii kuwa makini na mafundisho ya mitandaoni kuhusu masuala ya ndoa kwani siyo kila maudhui yanalenga ustawi wa ndoa badala yake ni upotoshaji ambao matokeo yake ni kuwa na ndoa zenye migogoro ambayo inazorotesha ustawi wa taasisi muhimu ya ndoa.

    Akizungumzia malezi ya watoto ambao kila familia inajaaliwa alisema huwa wanakuja na changamoto hivyo aliwataka wazazi na walezi kutokawakatia tamaa watoto wao kwa kuwa watoto hao wamebeba kusudi la Mungu.

    “Malezi ya watoto huwa yanaambatana na changamoto mbalimbali katika hatua za malezi tangu utoto hadi utu uzima”, alisema Mwalimu Mwabenga.

    Mwinjilisti Kiongozi wa Mtaa huo, Emeline Mzava aliwajulisha washarika kuhusu ujio wa vijana zaidi ya mia mbili (200) ambao walikuja siku hiyo kwa ajili ya mkutano kwa ajili ya mipango yao ya shughuli za vijana.

    “Niliipokea taarifa ya mkutano huo kwa kwa shukrani japo nlijiuliza ikiwa Kwembe imeonwa kuwa yaweza kuwa mwenyeji wa mkutano mkubwa kama huo”, alisema Mwinjilisti Mzava.

    Mwenyekiti wa Kwaya Kuu ya Mtaa huo, Jonas Mnkeni aliwajulisha washarika wa mtaa huo kuhusu uzinduzi wa albamu ya kwanza ya picha mjongeo (video) ambao unatarajiwa kufanyika Jumapili ya Tarehe 23 Februari 2024.

    “Ninaomba washarika mtuunge mkono ili kuendeleza kuitangaza injili kupitia albamu hii ya kwanza ya toleo la video”,alisema Mnkeni.  

    Sehemu ya jengo la Kanisa Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Mtaa wa Kwembe ambalo linaendelea kujengwa, (Picha zote na Michael Mwambage).

  • Na Vincent Mpepo, Kwembe

    Vijana wa kike na kiume nchini wametakiwa kujishughulisha na kuzalisha kipato kitakachowasidia hata kama hawakupata ajira kwenye mifumo rasmi iwe serikalini au sekta binafsi.

    Wito huo umetolewa na Mwalimu Bupe Mwabenga wakati akihubiri katika ibada siku ya Jumapili katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Mtaa wa Kwembe na kusisitiza kuwa bado wana wajibu kama wanajamii kujibiidisha ili kufikia maono ya ndoto zao.

    Alisema kufanya kazi na kuzalisha baada ya kuhitimu masomo kutawasaidia kuepuka utegemezi kwa wazazi na walezi ambao wamejitoa kuwafikisha hatua hiyo.

    Alisema vijana wanatakiwa kujisimamia katika maisha na kuwakumbusha kujenga mahusiano mema na Mungu na wanajamii wanaowazunguka.

    Aidha,aliwapongeza washarika wa Mtaa huo kwa ujenzi wa nyumba ya Mungu huku akitanabaisha kuwa ujenzi siyo rahisi na kuwatia moyo kwa kuwa wanafanya jambo jema machoni pa Mungu.

    “Kujenga siyo rahisi iwe kwenye ngazi ya familia au taasisi”, alisema Mwalimu Mwabenga.

    Mwinjiisti Kiongozi wa Mtaa huo, Emeline Mzava alimshukuru Mwalimu Mwabenga mafundisho mazuri kwa kuwa kilichofundishwa kimegusa maeneo mengi na kwa washarika wa rika zote kiasi kwamba kila aliyehudhuria amepata kwa sehemu yake.

    Aidha, aliwakumbusha washarika kuhusu harambee ya kuchangia kituo cha Udiakonia cha watoto wenye mahitaji maalumu ambacho kitahamishwa kutoka Kijichi Kwenda Kitopeni-Bagamoyo kutokana na changamoto za kimazingira mahali kiliposasa.

    “Tuhusike kwenye harambee hii kama sehemu ya kumshukuru Mungu kwa kutujalia Watoto”, alisema Mwinjisti Mzava.

    Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa Mtaa huo, Exaud Mchome aliwashukuru washarika kwa kuendelea kuchangia ujenzi wa kanisa huku akiwataka kutokata tamaa na kazi hiyo.

    Alisema kazi inayofuata ni kutengeza mifumo ya uwekaji paa ambapo kuna uhitaji wa matofali ya kawaida 5,000,  ya ruva 1500 na mifuko ya saruji ipatayo 1,500.

  • Na Tabia Ally, DSM

    Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) itashirikiana na Jeshi la Polisi Tanzania katika utekelezaji wa mikakati ya kuimarisha usalama barabarani ili kupunguza ajali.

    Hayo yamebainika wakati wa ziara ya Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania, Kamanda SACP William Mkonda katika Ofisi za Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) zilizopo Mtendeni, Dar es Salaam mwanzoni mwa wiki hii.

    Kamanda SACP William Mkonda alisema lengo la ziara hiyo kujadili na kuweka mikakati ya ushirikiano kati ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) na Jeshi la Polisi Tanzania ikiwa ni maandalizi ya Kikao Kazi cha Makamanda wa Polisi wa Usalama Barabarani wa Mikoa na Wilaya kinachotarajiwa kufanyika jijini Dodoma Februari 2025.

    “Kikao hicho kinalenga kuweka mikakati madhubuti ya kupunguza ajali za barabarani na madhara yake kwa watumiaji wa barabara”, alisema Kamanda SACP Mkonda.

    Alisema kuna umuhimu wa elimu ya bima kwa makamanda wa polisi wa usalama barabarani wa wilaya na mikoa hususani katika uhakiki wa bima kupitia mifumo rasmi.

    Kamishna wa Bima Tanzania, Dkt. Baghayo Saqware alisema hatua ya kuunganisha mifumo ya TIRA na Polisi itasaidia upatikanaji wa taarifa za ajali mara zinapotokea.

    “Hatua hii inalenga kuhakikisha waathirika wa ajali wanapata fidia zao kwa haraka, kwani taarifa za ajali zitasomwa moja kwa moja na kampuni za bima kupitia mfumo wa TIRA”, alisema Kamishna Dkt.  Saqware.

    Mkutano makamanda wa Polisi wa Usalama Barabarani wa mikoa na wilaya utafanyika jijini Dodoma wiki ya tatu ya Mwezi Februari 2025 huku Mkuu wa Mkoa huo, Bi. Rose Senyamule anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi.

  • Na Martha Joachim,Tanga

    Kamati ya Kudumu ya Baraza la Wawakilishi, Mawasiliano, Ardhi na Nishati Zanzibar, imelipongeza Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kwa utendaji kazi madhubuti katika usimamizi wa sheria na kanuni za usalama, ulinzi na utunzaji mazingira  wa usafiri majini.

    Pongezi hizo zimetolewa hivi karibuni na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Yahya Rashid Abdulla, walipotembelea Ofisi za TASAC mkoani Tanga na kufanya kikao na watumishi wa TASAC pamoja na watumishi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA).

    “Tumefurahishwa na utendaji kazi mzuri wa TASAC katika udhibiti na usimamizi wa safari kwa njia ya maji hasa katika Bandari ya Tanga”, alisema Mhe. Abdulla

    Alisema usimamizi mzuri umesaidia kurahisisha usafiri kati ya Tanzania Bara na Visiwani kwa eneo la mwambao ambalo lilikua na changamoto kubwa ya usafiri kwa njia ya maji.

    Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu TASAC, Meneja Mafunzo na Utoaji vyeti Mhandisi Lameck Sondo ameishukuru Kamati hiyo na kuahidi kuendeleza weledi, ufanisi na ushirikiano na taasisi nyingine katika kudhibiti na kusimamia shughuli za usafiri majini kwa maslahi mapana ya Taifa.

    Mhandisi Sondo alisema Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limeendelea na utekelezaji wa mradi wa uboreshaji wa usalama wa usafiri katika Ziwa Victoria  ambao ni mradi unaoshirikisha nchi za Uganda na Tanzania katika kanda ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

    Aidha, ameeleza kuwa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) imefanikiwa katika ukaguzi wa meli za kigeni pamoja na kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa watumishi ili kuwajengea uwezo katika kutekeleza majukumu hayo kwa weledi.

    Kamati ya Kudumu ya Baraza la Wawakilishi, Mawasiliano, Ardhi na Nishati Zanzibar ilifanya ziara hiyo mwanzoni mwa wiki hii ili kujifunza utendaji kazi na kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) na TPA mkoani Tanga ikiwemo Bandari za Tanga, Pangani na Kipumbwi.

  • Na Ruth Kyelula, Mbulu

    Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Joseph Mandoo amewataka madiwani na  wakuu wa idara kushirikiana ili kuhakikisha wanafunzi wanaripoti shule kabla ya muda uliopangwa kuisha.

    Mandoo aliyasema hayo wakati akifungua baraza la madiwani katika robo ya pili ya Octoba-Desemba 2024/2025 iliyofanyika hivi karibuni kwenye ukumbi wa halmashauri ya Wilaya hiyo huku akitanabaisha kuwa serikali hutumia fedha nyingi katika kuboresha miundombunu ya shule huku idadi ya wanaosoma ni chache.

    “Wanafunzi wote waliofaulu Kwenda kidato cha kwanza wahimizwe Kwenda shule”, alisema Mandoo

     Aliwataka maafisa elimu na watendaji wa kata na vijiji kushirikiana ili kufanikisha jambo hilo.

    Aidha, aliwakumbusha watumishi hao kujitathimini na kujua sababu zinazochangia shule za msingi za umma kutofanya vizuri katika mitihani ya taifa hivyo kuja na mikakati madhubuti ili kunusuru hali hiyo.

    Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Abubakar Kuuli alisema uandikishaji wa wanafunzi wa elimu msingi na wanafunzi wa sekondari wanaoripoti bado hauridhishi licha ya kuwashirikisha watendaji wa kata kwenye zoezi hilo.

    “Hadi sasa ni asilimia 51 ya wanafunzi wa elimu msingi ndio wameandikishwa huku asimilia 52 ndio wameripoti shule kwa upande wa sekondari.

    Akitoa ripoti ya ufaulu kwa matokeo ya kidato cha nne kwa mwaka 2024 alisema ufaulu umefika asilimia 98.7 ambapo umeongezeka kwa asilimia 3.7 kutoka matokeo ya mwaka 2023.

    Kwa upande wake, Mbunge wa Mbulu Vijijini, Flatei Massay aliwapongeza madiwani na wakuu wa idara wote kwa kazi kubwa kufuatia ufaulu huo.

    Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbulu, Paulo Bura aliutaka uongozi wa  Halmashauri kuhakikisha wanafunzi wanaripoti mapema katika Shule ya Sekondari ya Eshkesh huku pia akitoa makataa ya kuripoti kuwa March 31, 2025.

    Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Mbulu, Melkiadi Nar aliwashukuru viongozi kwa kazi kubwa  wanayofanya huku pia akitoa rai ya kuongezwa kwa shule za sekondari za kidato cha tano (5) na cha sita(6).

  • Na Cartace Ngajiro, Tanga

    Serikali imepongezwa kwa kuendelea kuboresha bandari nchini na kuziwezesha kukusanya baadhi ya mapato “Wharfage” jambo ambalo limeongeza ufanisi  katika utendaji.

    Pongezi hizo zilitolewa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Uchukuzi Ludovick Nduhiye hivi karibuni wakati ziara yake katika bandari ya Tanga kujiuonea utendaji kazi wa bandari hiyo.

    Akipokea taarifa ya mradi wa maboresho yaliyofanyika katika bandari hiyo Nduhiye alisifu  mfumo mzima wa utendaji kazi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania ambao umesaidia ongezeko la makusanyo ya mapato bandarini hapo.

    “Kukua kwa mzigo toka shehena tani 750,000 hadi tani 3,000,000 kwa mwaka inaonyesha kwa kiasi gani maboresho hayo yamezaa matunda matunda”. Alisema Nduhiye

    Kwa upande wake, Meneja wa Bandari ya Tanga, Masoud Mrisha alisema kukamilika kwa mradi huo kumeleta ufanisi, tija na faida  ikiwemo uharaka katika kuhudumia Meli ongenzeko la idadi ya meli, na kupungua kwa gharama za uendeshaji.