• Na Mwandishi wetu, Nachingwea

    Mbunge wa Jimbo la Nachingwea Fadhili Liwaka ameahidi kuwalipia bodaboda zaidi 300 shilingi Elfu tano (5000) kwa Kila bodaboda atakayekwenda kununua kofia ngumu kwenye duka maalum alilolipendekeza.

    Akizungumza katika kikao kazi na bodaboda hao hivi karibuni, Mbunge Liwaka alisema kuwa ameamua kuwaunga mkono kwa kiasi hicho cha fedha kwa lengo kuwaondolea adha ya kukamatwa na polisi wa barabarani pamoja kujikinga na ajali za barabarani.

    “Napokea simu kutoka kwa bodaboda juu ya kukamatwa na polisi wa barabarani kwa kosa la kutokuwa na kofia ngumu hivyo kama Mbunge wenu nimeamua kuwachangia kiasi hicho ili kila mmoja wenu aweze kulimiki kofia ngumu yake”, alisema Mbunge Liwaka.

    Aidha aliliomba Jeshi la Polisi wilaya ya Nachingwea kuwapa muda mfupi ili kila bodaboda aweze kununua kofia ngumu kwa ofa aliyoitoa ya kuwachangia kiasi tajwa.

    Kwa upande wake, mmoja wa waendesha bodaboda Wilaya ya Nachingwea, Mohamed Rashidi alimshukuru Mbunge kwa ahadi hiyo ya fedha ambayo itawawezesha bodaboda kupata kofia ngumu na  wapo tayari kumuunga mkono kwa kununua kofia hizo kama alivyo waelekeza.

  • Na Athuman Kajembe, Nachingwea

    Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, mkoani Lindi, Mohamed Hassan Moyo, ameonesha kukerwa baada ya kubaini ujenzi wa Kituo cha Afya cha Nammanga, Kata ya Ruponda, unaendelea bila kufuata Hati ya Makadilio Kiasi cha Kazi (BOQ) kama ilivyoainishwa na serikali.

    Akiwa katika ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi huo, DC Moyo alisema serikali haiwezi kuvumilia wataalamu wanaojenga majengo ya umma bila kuzingatia taratibu, kanuni na viwango vilivyowekwa.

    “Leo hii jamvi linafunikwa bila utaratibu, nondo za mita nane zinatumika badala ya nondo za mita 12 na mbao zinazotumika kujenga majengo mawili si zile zilizo kwenye BOQ, hili ni kosa kubwa,” alisema DC Moyo.

    Alisema kitendo hicho kinaashiria matumizi mabaya ya fedha za umma na ujenzi wa miundombinu isiyokidhi viwango vya ubora.

    “Naagiza TAKUKURU kuwakamata na kuwafikisha mahakamani wahandisi wote wanaohusika ili kujibu kwa nini wanajenga chini ya kiwango na kutumia vifaa visivyoidhinishwa”, alisema DC Moyo.

    Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea ambaye pia ni Afisa Mipango, Joshua Mnyang’ali, alikiri kuwepo kwa makosa katika ujenzi huo na kumuomba DC Moyo msamaha mbele ya hadhira.

    Hata hivyo, DC Moyo alisisitiza kuwa suala hilo litashughulikiwa kikamilifu kupitia ofisi za TAKUKURU ili kuhakikisha haki inatendeka na fedha za serikali hazipotei.

    Inakumbukwa kuwa mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Nammanga umetengewa zaidi ya milioni 200 hadi kufikia Februari 2026, kiasi kinachotarajiwa kukamilisha ujenzi huo kwa viwango vinavyokubalika.

  • Na OWM (KAM) – DODOMA

    Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) umepongezwa kwa hatua kubwa ilizochukua katika kuboresha upatikanaji wa huduma kwa wananchi, hususan utoaji wa fidia kwa wafanyakazi wanaokumbana na madhila ya ajali ama ugonjwa unaotokana na kazi.

    Pongezi hizo zimetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Sangu jana jijini Dodoma wakati wa ziara yake katika Ofisi za Makao Makuu ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) alipokutana na menejimenti na baadhi ya watumishi wa WCF kwa lengo la kujua majukumu ya Mfuko huo sambamba na kutoa maelekezo ya kiutendaji yanayolenga kuongeza tija na ufanisi.

    Sangu alisema huduma hizo bora zimechangia kuimarisha imani ya wananchi kwa mfuko, ambapo wafanyakazi wanaopatwa na majanga kutokana na kazi wamekuwa wakipatiwa huduma kwa wakati na kwa kiwango kinachostahili hivyo kuongeza ufanisi na kupunguza usumbufu kwa wafanyakazi,

    Katika hatua nyingine, Waziri Sangu ameitaka Menejimenti ya WCF kuendeleza ubunifu katika utekelezaji wa majukumu yao, ikiwemo kuongeza nguvu ya mifumo mipya ya kidijitali inayoboresha mbinu za utoaji huduma kwa wakati na ufanisi zaidi ili kufikia wananchi kwa haraka.

    Awali, akizungumza, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Rahma Kisuo, amehamasisha Menejimenti ya Mfuko huo kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu majukumu na huduma zinazotolewa na Mfuko, ili kuongeza uelewa kwa waajiri wengi zaidi.

    Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa WCF Dkt. John Mduma alisema WCF imejipanga kuendelea kuboresha mifumo ya utoaji huduma ili kuhakikisha madai ya fidia yanashughulikiwa kwa wakati, uwazi na ufanisi zaidi.

  • Na Mwandishi Wetu

    Wizara ya Maliasili na Utalii imesema ushindi wa Tanzania kwenye tuzo za World Travele Award 2025 ikiwemo tuzo kubwa ya Utalii wa safari bora duniani ni uthibitisho kuwa nchi ina vivutio vya utalii vinavyokubalika kimataifa.

    Akizungumza Desemba 8, 2025 mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam, akitokea Bahrain, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk. Hassan Abbas amesema  ushindi huo unaonesha kuwa dunia imeitambua Tanzania kama kitovu bora cha utalii wa safari.

    “Kwa mwaka wa pili mfululizo tumeshinda tuzo kubwa zaidi ya utalii wa safari duniani. Hii ni sawa na tuzo za Oscars kwa filamu au Grammy kwa muziki,” alisema Dk. Abbas.

    Alisema kutokana na ushindi  huo, nchi imepewa heshima ya kuwa mwenyeji wa tuzo za dunia za utalii mwaka 2026, ambapo wadau wakubwa wa sekta hiyo duniani watakusanyika nchini.

    Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania, Ephraim Mafuru, amewashukuru wadau wa utalii kwa kuipigia kura Tanzania, akisema ushindi huo umetokana na imani ya dunia kwa Serengeti na hifadhi nyingine.

    “Tanzania imeshinda tuzo ya Hifadhi bora duniani kupitia Serengeti, pamoja na tuzo ya Utalii wa Safari Bora Duniani mafanikio haya yametokana na  uboreshaji miundombinu ikiwemo barabara  zaidi ya kilomita 2,800 ndani ya hifadhi na  kuvifanya vivutio kufikika kwa urahisi,” alisema Mafuru.

  • Na Mwandishi Wetu

    Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita limewataka viongozi  wa makundi ya mitandao ya kijamii, hususan WhatsApp, kudhibiti usambazaji wa taarifa za uchochezi, uvunjifu wa amani.

    Wito huo umetolewa  Desemba 8, 2025 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, SACP Safia Jongo, alipoungana na Mtandao wa Polisi Wanawake Tanzania (TPF-Net) mkoani humo  kutoa msaada katika Kituo cha Afya Nyankumbu  ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga ukatili wa kijinsia.

    Kamanda Jongo alisema mitandao ya kijamii, hususan makundi ya WhatsApp, isiruhusiwe kuwa majukwaa ya kusambaza chuki, vitisho, taarifa za upotoshaji na unyanyasaji wa kidijitali dhidi ya wanawake na wasichana.

    Alisema wasimamizi wa makundi ya WhatsApp na watumiaji wa mitandao ya kijamii wanayo nafasi kubwa ya kudhibiti maudhui yanayokiuka maadili, sheria na kuchochea uvunjifu wa amani.

    “Ni wajibu wao kuhakikisha mitandao haigeuki kuwa chanzo cha uhalifu na ukatili wa kijinsia,” alisema Kamanda Jongo.

    Alizungumzia Mtandao wa TPF-Net unaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kupambana na ukatili unaotekelezwa kupitia majukwaa ya kidijitali, sambamba na kuhamasisha wananchi kutoa taarifa mapema wanapobaini au kukumbana na vitendo vya ukatili.

    Aidha, amewataka wananchi kuepuka vitendo vya vurugu, uhalifu na uvunjifu wa amani, huku akisisitiza umuhimu wa kukomesha vitendo vyote vya ukatili, hususan unaofanywa mtandaoni dhidi ya wanawake na wasichana.

  • Na Vincent Mpepo

    Walimu wanaosoma somo la Kifaransa kama mmoja ya somo la kufundishia wametakiwa kuwekeza nguvu nyingi na kujibidiisha kwani kuna fursa nyingi za ajira za ndani na nje ya nchi kupitia lugha hiyo.

    Wito huo umetolewa mwishoni mwa wiki katika mijadala mbalimbali ya Siku ya Walimu wa Kifansa Duniani iliyofanyika katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari Azania ambapo fursa za Lugha hiyo zilibabinishwa.

    Mwenyekiti wa Chama cha Walimu wa Kifaransa Tanzania (TAFT), Dkt. Costantine Njalambaya alisema Kifaransa si tu lugha ya kujifunza, bali ni fursa ya ubunifu na chombo cha mshikamano kinachotumika kujieleza kupitia utamaduni na daraja linalounganisha watu.

    Dkt. Njalambaya aliushukuru Ubalozi wa Ufaransa kwa msaada wa kifedha, ambao umewezesha sherehe hizo kufanyika na kwamba unasaidia kimarisha dhamira chama hicho kukuza ufundishaji wa lugha ya Kifaransa nchini Tanzania na kuendeleza jamii kielimu.

    Aidha alizungumzia mipango na mikakati ambayo chama chake kimeiweka ili kuwafikia walimu wengi wa Kifaransa nchini mijini na vijijini ili kuongeza wigo wa walimu wa Kifansa nchini.

    Mwalimu wa Kifaransa, Frola Musikula ambaye kwa sasa amestaafu, alisema kuna fursa nyingi kwa vijana ambao wanasoma Kifaransa na kutanabaisha kuwa kwa uzoefu wake amegundua wanafunzi wanaomliza Shule ya Msingi wengi wao wanapenda sana Kifaransa.

    “Watoto wangu wawili wanafundisha Kifaransa na pia Kifaransa kimeniwezesha kugfanya kazi kwenye maeneo mengi ikiwemo sekta ya utalii na ualimu huko Zanzibar”, alisema Mwalimu Flora.

    Alisema pamoja na kwamba amestaafu bado anafundisha Kifaransa kwa wanafunzi waliomaliza darasa la saba ambao wanajiandaa kuingia kidato cha kwanza katika kituo cha ‘Pugu Intercity Academy’.

    Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, Afisa Elimu Kata, Upanga Magharibi ambaye alimwakilisha Afisa Elimu Jiji la Dar es Salaam, Mwalimu Immaculata Ngure alisema wakati umefika kwa serikali kubadilika na kuongeza idadi ya walimu wa somo la kifaransa kutokana na umuhimu na faida za somo hilo katika nchi na kwa mtu mmojammoja.

    “Uhamasishaji ufanyike ili kuhakikisha watoto wetu wanasoma lugha ya kifaransa”, alisema Mwalimu Immaculata.

    Akizungumzia matumizi ya nyimbo katika ufundishaji alisema ni zana muhimu katika kusaidia kukuza uelewa na kuweka kumbukumbu hatahivyo alishauri uchaguzi wa nyimbo hizo ufanyike kwa makini ili kuwa na maudhui yanayofaa kwa kuwa siyo nyimbo zote zinaweza kutumika.

    Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Azania, Mwalimu Magreth Lawrance alisema shule hiyo ina darasa maalumu la Kifaransa na ameshukuru kusikia kuwa uongozi wa chama hicho unakusudia kufanya maboresho katika darasa hilo jambo ambalo ni jema.

    “Sisi kama watanzania tumewasikia wenzetu kutoka Zanziobar na kilichotuunganisha ni Lugha ya Kifaransa kama ambvyo Mwalimu Nyerere alivyofanikiwa kuwaunganisha watanzania kwa kutumia Lugha”, alisema Mwalimu Magreth.

    Aidha alishauri walimu wa shule nyingine kuanzisha somo hilo la Kifaransa kwa kuwa watoto wanapenda n ani fursa nzuri kwao.

    Maadhimisho ya mwaka huu yenye kaulimbiu “Kuimba, Kucheza, Kufundisha: Lugha ya Kifaransa katika Muziki,” yanaangazia sanaa na michezo inavyotumika kwenye kufundisha lugha ya Kifaransa yamewakutanisha walimu, wahadhiri, wanafunzi wa lugha ya Kifaransa nchini yakihusisha bara na visiwani huku ikibanika kuwa Lugha hiyo ina ladha ya kipekee kwenye muziki hivyo ni rahisi kufundishika.

  • Mgeni Rasmi wa katika maadhimisho ya Siku ya Kifaransa Duniani, Afisa Elimu Kata ya Upanga Magharibi, Mwalimu Immaculata Ngure katika picha ya pamoja na meza kuu pamoja na walimu wa Kifaransa waliohudhuria katika maadhimisho hayo jana Katika Shule ya Sekondari Azania, jijini Dar es Salaam. (Picha na Vincent Mpepo).

    Na Vincent Mpepo

    Wadau wa lugha ya Kifaransa nchini wamekutana katika Shule ya Sekondari ya Azania kuadhimisha Siku ya Kifaransa Duniani, ikiwa ni sehemu ya kuienzi lugha hiyo adhimu na kubainisha fursa mbalimbali zinazopatikana kwa wanaojifunza Kifaransa.

    Katika maadhimisho hayo yaliyofanyika jana jijini Dar es Salaam, wahadhiri, wakufunzi, walimu na wanafunzi wa lugha ya Kifaransa walisema bado kunahitajika hamasa zaidi kwa jamii ili kuongeza uelewa na mapenzi ya kujifunza lugha hiyo.

    Mwenyekiti wa Chama cha Walimu wa Kifaransa Tanzania (TAFT), Dkt. Costantine Njalambaya, alisema Kifaransa si lugha ya kujifunza pekee, bali ni daraja la utamaduni, ubunifu na mshikamano linalowawezesha watu kujieleza na kuunganishwa kimataifa.

    Mwenyekiti wa Chama cha Walimu wa Kifaransa Tanzania (TAFT), Dkt. Costantine Njalambaya akihutubia hadhara ya wanafunzi, wakufunzi, wahadhiri na wadau mbalimbali wa Lugha ya Kifaransa katika maadhimisho ya Lugha hiyo yaliyofanyika jana katika Shule ya Azania jijini Dar es Salaam. (Picha na Vincent Mpepo).

    Alibainisha kuwa maadhimisho ya mwaka huu yenye kaulimbiu “Kuimba, Kucheza, Kufundisha: Lugha ya Kifaransa katika Muziki” yameangazia namna sanaa na michezo vinavyoweza kutumika kuboresha ufundishaji wa lugha hiyo.

    Aidha, aliushukuru Ubalozi wa Ufaransa kwa msaada wa kifedha uliowezesha kufanyika kwa maadhimisho hayo, akisisitiza kuwa mchango huo umeendelea kuimarisha jitihada za chama hicho katika kukuza ufundishaji wa Kifaransa nchini.

    Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Walimu wa Kifaransa Mkoa wa Dar es Salaam ambaye pia ni mwalimu wa Kifaransa katika Shule ya Sekondari Chang’ombe, John Daudi, alisema chama hicho kimepiga hatua kubwa, huku akishukuru serikali kwa ushirikiano inaotoa.

    “Kwa mfano, mwaka jana tuliandaa Siku ya Walimu wa Kifaransa katika Kituo cha Utamaduni cha Kifaransa hapa Dar es Salaam, na mwaka huu tumefanya hapa Sekondari ya Azania,” alisema Mwalimu Daudi.

    Naye Mgeni Rasmi wa maadhimisho hayo, Afisa Elimu Kata ya Upanga Magharibi, Mwalimu Immaculata Ngure, aliyemwakilisha Afisa Elimu wa Jiji la Dar es Salaam, alikipongeza chama hicho kwa juhudi za kuwaunganisha wadau wa lugha hiyo wakiwemo walimu, wakufunzi, wahadhiri na wanafunzi.

    Afisa Elimu Kata ya Upanga Magharibi, Mwalimu Immaculata Ngure akihutubia washiriki wa maadhimisho ya Siku ya Walimu wa Kifaransa Duniani yaliyofanyika jana katika Shule ya Azania jijini Dar es Salaam. (Picha na Vincent Mpepo).

    Alisema wakati umefika kwa serikali kuongeza idadi ya walimu wa somo la Kifaransa kutokana na umuhimu na manufaa yake kwa nchi na kwa mtu mmoja mmoja. Alisisitiza pia kuwepo kwa uhamasishaji zaidi ili watoto wawe na motisha ya kujifunza lugha hiyo.

    Akizungumzia matumizi ya nyimbo katika ufundishaji wa lugha, Mwalimu Immaculata alisema nyimbo ni zana muhimu inayosaidia kuongeza uelewa na kuhifadhi kumbukumbu za kudumu kwa wanafunzi, hasa watoto.

    Aidha, alieleza kuwa kuanzia mwaka huu Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) limeanza kutahini wanafunzi wa shule za msingi katika lugha mbalimbali ikiwemo Kifaransa, Kichina na Kiarabu, akibainisha kuwa hatua hiyo ni fursa kubwa kwa wanafunzi kupata manufaa ya lugha hizo za kimataifa.

    Katika maadhimisho hayo, mada mbalimbali ziliwasilishwa ikiwemo umuhimu wa kutumia muziki katika ufundishaji wa Kifaransa, ambapo ilibainika kuwa mbinu hiyo inachochea uelewa wa haraka na husaidia wanafunzi kukumbuka wanachojifunza kwa urahisi.

    Maadhimisho ya mwaka huu yamewakutanisha walimu, wahadhiri na wanafunzi wa Kifaransa kutoka Tanzania Bara na Visiwani, yakionyesha kwa mara nyingine kuwa lugha hiyo ina mvuto wa kipekee katika muziki na hivyo kuwa rahisi kufundisha na kujifunza.

    Sehemu ya washiriki wa maadhimisho ya Siku ya Walimu wa Kifaransa Duniani wakifuatilia mijadala hapo jana katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari Azania. (Picha na Vincent Mpepo).