Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, amemtaka mkandarasi anayejenga Kampasi ya Tanga ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huo ili ukamilike kwa wakati.
Kikwete alitoa agizo hilo baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa kampasi hiyo jijini Tanga, akisema Serikali inatarajia jengo hilo kukamilika ifikapo Mei 2027 na kuanza kutumika.
Alisema ujenzi wa kampasi hiyo una umuhimu mkubwa kwa Serikali kwa kuwa unalenga kutoa elimu na mafunzo kwa wananchi wa Mkoa wa Tanga na maeneo mengine nchini.
“Serikali haitaki majengo haya yajengwe kwa ajili ya kuonekana pekee, bali yanapaswa kukamilika na kutumika kufikia malengo yaliyowekwa,” amesema.
Kikwete amepongeza uongozi wa TPSC kwa usimamizi wa mradi huo, huku akimtaka mkandarasi kuongeza kasi ya kazi na kuzingatia viwango vinavyohitajika ili kukamilisha mradi kwa wakati.
Alisema mkandarasi anapaswa kutekeleza majukumu yake kwa wakati ili kuepusha uwezekano wa kuchukuliwa hatua, ikiwemo kubadilishwa iwapo atashindwa kutimiza matakwa ya mkataba.
Kikwete alisema kukamilika kwa jengo hilo kutatoa fursa ya kuendelea na ujenzi wa majengo mengine yaliyopangwa ndani ya Kampasi ya Tanga.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tanga ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Gilbert Kalima, ameishukuru Serikali kwa kuupa umuhimu mradi wa ujenzi wa Kampasi ya TPSC katika Mkoa wa Tanga.
Alisema uwepo wa kampasi hiyo utaongeza fursa za elimu na mafunzo kwa wananchi, sambamba na kuchangia maendeleo ya Mkoa wa Tanga.
Naye Kaimu Katibu Mkuu-Utumishi ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Prisca Lwangili, amemshukuru Waziri Kikwete kwa kuendelea kufuatilia utekelezaji wa majukumu ya wizara, ikiwemo maendeleo ya ujenzi wa Kampasi ya Tanga.
Alisema ufuatiliaji huo unasaidia kuhakikisha mipango inayowekwa na Serikali inatekelezwa kwa kuzingatia malengo yaliyokusudiwa.
Akitoa taarifa ya maendeleo ya mradi huo, Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa TPSC, Dkt. Ernest Mabonesho, amesema kampasi hiyo ikikamilika itakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 2,000.
Mabonesho alimshukuru Waziri Kikwete kwa ufuatiliaji wa mara kwa mara wa maendeleo ya mradi huo na kuendelea kuhimiza uongozi wa chuo kuhakikisha utekelezaji wa majukumu unakwenda kwa kasi inayotarajiwa.
Ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo unatarajiwa kufungua fursa mbalimbali za kiuchumi kwa wananchi wa Bagamoyo na maeneo jirani, ikiwemo ajira, biashara, usafirishaji na huduma mbalimbali zitakazochochewa na uwepo wa mradi huo mkubwa wa kimkakati.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo, amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua kuhakikisha wananchi wanaodai fidia kwa ajili ya kupisha ujenzi wa bandari hiyo wanalipwa stahiki zao.
Nyongo amesema Bandari ya Bagamoyo ni mradi wa kimkakati utakaosaidia kupunguza msongamano katika Bandari ya Dar es Salaam, huku ikiunganishwa na kongani za viwanda na kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa katika viwanda vya Mkoa wa Pwani.
Alisema hayo jana alipofanya ziara ya siku moja katika Wilaya ya Bagamoyo, ambapo alikagua miradi mbalimbali, ikiwemo eneo la ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo lililopo Mbegani.
“Bandari hii inajengwa katika eneo langu la utawala. Nitashirikiana na mamlaka zinazohusika kuhakikisha wananchi wanaodai fidia wanalipwa, lakini pia nitakuwa karibu kufuatilia utekelezaji wa ujenzi ili wananchi waweze kunufaika na fursa za kiuchumi zitakazotokana na mradi huu,” alisema Nyongo.
Aliwataka wananchi kutoa ushirikiano katika ujenzi wa bandari hiyo, akisema mradi huo utatoa fursa za kiuchumi kwa wakazi wa Bagamoyo na maeneo mengine ndani na nje ya wilaya hiyo.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Mhandisi Stephen Mbogela, alisema Serikali imekamilisha uthamini na utwaaji wa eneo lote la mradi lenye ukubwa wa hekta 887.
Alisema kati ya eneo hilo, hekta 407 zitatumika kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya bandari, huku hekta 480 zikitengwa kwa ajili ya maeneo ya lojistiki na usafirishaji.
Mhandisi Mbogela alisema Sh bilioni 49 tayari zimelipwa kama fidia kwa wananchi waliopisha mradi wa ujenzi wa bandari hiyo katika eneo la Mbegani.
Alisema Bandari ya Dar es Salaam inakaribia kufikia ukomo wa uwezo wake wa kuhudumia shehena na meli kubwa za kisasa, hivyo Bandari ya Bagamoyo itakuwa kitovu muhimu cha ziada kitakachosaidia kupunguza muda wa meli kusubiri kutia nanga na kuhudumia shehena.
“Shehena inayohudumiwa nchini imefikia zaidi ya tani milioni 30 kwa mwaka 2026 na inatarajiwa kufikia zaidi ya tani milioni 50 ifikapo mwaka 2030, kiasi ambacho kinahitaji miundombinu mipya na thabiti,” alisema Mhandisi Mbogela.
Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kupitia Kituo cha Taifa cha Kudhibiti Matukio ya Sumu (NPCC), imewataka wananchi kuacha kutumia vijiwe kama njia ya kutibu madhara yatokanayo na kung’atwa na nyoka, na badala yake kuwahi katika vituo vya afya au hospitali kwa ajili ya kupata matibabu sahihi kwa wakati.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Kituo cha Taifa cha Kudhibiti Matukio ya Sumu, Yohana Goshashy, wakati akitoa elimu kwa wananchi wa Kibaha, mkoani Pwani, kuhusu namna ya kujikinga na matukio ya kung’atwa na nyoka, hatua zinazopaswa kuchukuliwa endapo mtu atang’atwa na nyoka na madhara yanayoweza kujitokeza iwapo mhanga hatapata huduma ya kitabibu kwa wakati.
Goshashy alisema bado kuna baadhi ya wananchi wanaoamini matumizi ya vijiwe kama tiba ya kuondoa sumu baada ya kung’atwa na nyoka, hali ambayo inaweza kuchelewesha upatikanaji wa huduma stahiki.
“Tunawasihi wananchi kuacha kutumia vijiwe kama dawa ya kutibu mtu aliyeng’atwa na nyoka,” alisema Goshashy.
Alisema mtu anapong’atwa na nyoka anapaswa kuchukuliwa kama mgonjwa anayehitaji huduma ya kitabibu na kupelekwa hospitalini haraka iwezekanavyo, badala ya kutumia tiba ambazo hazijathibitishwa kitaalamu.
Aliongeza kuwa kuwahi hospitalini ni muhimu kwa kuwa wataalamu wa afya wanaweza kufanya tathmini ya hali ya mgonjwa na kutoa huduma kulingana na madhara yaliyosababishwa na kung’atwa na nyoka.
Aidha, aliwataka wananchi kuepuka kutumia njia za kienyeji ambazo zinaweza kuongeza madhara kwa mhanga, ikiwemo kuchanja sehemu iliyong’atwa, kunyonya damu au sumu, kuchoma eneo lililong’atwa au kufunga kiungo kwa nguvu bila ushauri wa kitaalamu.
Goshashy alisema matukio ya kung’atwa na nyoka yanaweza kutokea katika maeneo mbalimbali, hususan ambako shughuli za wananchi zinahusisha kilimo, ufugaji, uwindaji au shughuli nyingine zinazowaweka katika mazingira yenye uwezekano wa kukutana na nyoka.
Mmoja wa wananchi wa Kijiji cha Soga, Iddi Pasi, alisema katika baadhi ya matukio watu wanapopatwa na changamoto hiyo huanza kutafuta msaada kutoka kwa watu wanaodai kuwa wana uwezo wa kutibu madhara ya sumu kwa kutumia tiba za jadi, hali inayoweza kuchelewesha upatikanaji wa huduma ya kitabibu.
“Changamoto kubwa kwetu ni pale mtu anapong’atwa na nyoka. Mara nyingi watu wanakuwa na hofu na hawajui waanzie wapi,” alisema Pasi.
Alisema wakati mwingine waathirika hupelekwa kwa watu wanaodai kutumia vijiwe au dawa za kienyeji, lakini elimu waliyopewa imewasaidia kuelewa kuwa hatua ya kwanza ni kumfikisha mhanga hospitalini.
Wananchi walioshiriki mafunzo hayo walisema elimu iliyotolewa na Mamlaka itawasaidia kujikinga na nyoka na kuchukua hatua sahihi endapo mtu atang’atwa, huku wakibainisha kuwa changamoto kubwa ni umbali wa vituo vya afya, hofu na ukosefu wa uelewa wa namna ya kutoa msaada wa awali kwa waathirika.
Wananchi wa Boko Mnemela wakimsikiliza mwezeshaji (hayupo pichani), akitoa elimu kuhusu matukio ya nyoka.
Tanzania inalenga kukusanya Sh trilioni 36.99 kutokana na kodi katika mwaka wa fedha 2026/27, huku Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, akisisitiza matumizi ya teknolojia kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato na kurahisisha ulipaji kodi.
Ndejembi alisema matumizi ya teknolojia katika usimamizi wa kodi ni muhimu katika kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato ya ndani na kupunguza vikwazo kwa walipa kodi wanaofuata sheria.
Alisema hayo jana alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika ufunguzi wa Mkutano wa 46 wa Chama cha Wasimamizi wa Kodi wa Jumuiya ya Madola (CATA), unaofanyika katika Ukumbi wa Gran Melia jijini Arusha.
Alisema katika bajeti ya mwaka 2026/27, mapato ya ndani yanatarajiwa kugharamia takribani asilimia 74.2 ya Bajeti ya Taifa, akisisitiza kuwa matumizi ya rasilimali za ndani, hususan mapato ya kodi, ni muhimu katika kugharamia huduma za umma, miundombinu, uwekezaji wenye tija na kuimarisha kujitegemea kiuchumi.
“Ongezeko endelevu la mapato linahitaji uchumi kukua, idadi ya walipa kodi kuongezeka, wananchi kuendelea kulipa kodi kwa hiari pamoja na matumizi sahihi ya teknolojia na takwimu,” alisema.
Ndejembi alisema mifumo ya kodi inapaswa kutumia teknolojia kurahisisha ulipaji wa kodi kwa hiari, kuboresha huduma kwa walipa kodi na kuwezesha mamlaka za mapato kutumia data katika kufanya maamuzi na kutambua maeneo yenye changamoto.
Alisema mfumo mzuri wa kodi unapaswa pia kuwezesha biashara halali, kuhimiza uwekezaji na urasimishaji wa shughuli za kiuchumi, bila kuweka vikwazo vinavyoweza kudhoofisha shughuli zenye tija.
Akirejea kaulimbiu ya mkutano huo, “Leveraging Technology for Efficient Revenue Collection”, Ndejembi alisema teknolojia inapaswa kusaidia Serikali kupunguza gharama za kiutawala, kurahisisha ulipaji kodi na kuimarisha mazingira ya biashara.
Alisema ushirikiano wa kimataifa katika masuala ya kodi ni muhimu katika kubadilishana taarifa, uzoefu na mbinu bora za usimamizi wa mapato, huku nchi zikihitaji kutafsiri uzoefu huo katika maboresho yanayoweza kupimika ndani ya mifumo yao.
Ndejembi alisema Tanzania imeendelea kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika masuala ya kodi, ikiwemo kubadilishana taarifa za kikodi na kutoa usaidizi wa kiutawala kati ya nchi.
Alisema maendeleo hayo yanapaswa kwenda sambamba na kuendelea kuboresha sheria na uwezo wa taasisi ili kuendana na viwango vya kimataifa vya uwazi na usimamizi wa kodi vinavyoendelea kubadilika.
Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Wasimamizi wa Kodi wa Jumuiya ya Madola (CATA), Dkt. Abu Tariq Jamaluddin, alisema jumuiya hiyo inalenga kuwaunganisha viongozi na wataalamu wa kodi ili kubadilishana uzoefu na kujifunza mbinu zinazoweza kuboresha utawala wa kodi.
Alisema katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, CATA imeendelea kuimarisha programu zake katika maeneo ya uongozi, mipango na teknolojia, pamoja na kutumia mijadala ya mtandaoni kuongeza fursa za kujifunza kwa wanachama.
Jamaluddin alisema lengo ni kuboresha utawala wa kodi, kurahisisha ulipaji wa kodi kwa hiari, kuongeza ufanisi wa watendaji na kuimarisha matumizi ya data katika usimamizi wa mapato.
Awali, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), CPA Yusuph Mwenda, alisema Serikali imeendelea kuwekeza katika mifumo ya kisasa ya ukusanyaji na usimamizi wa mapato.
Mwenda alitaja Mfumo Jumuishi wa Usimamizi wa Mapato ya Ndani (IDRAS) kuwa miongoni mwa mifumo hiyo, ukiwa na jumla ya moduli 17 zinazolenga kuboresha utoaji wa huduma na usimamizi wa mapato.
Alisema mojawapo ya moduli hizo inahusu utoaji wa ankara za kielektroniki, inayowawezesha walipa kodi kutoa ankara za kielektroniki kupitia mfumo huo bila kulazimika kutumia mashine halisi.
Mkutano huo unawakutanisha zaidi ya wataalamu na viongozi 400 kutoka nchi 48 za Jumuiya ya Madola kwa ajili ya kubadilishana maarifa na uzoefu kuhusu matumizi ya teknolojia katika kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa kodi.
Mjadala wa mkutano huo pia umejikita katika umuhimu wa kubadili mtazamo wa wananchi kuhusu ulipaji kodi, kuunganisha huduma za kikodi na mitandao ya simu, pamoja na kuweka motisha zitakazohamasisha wananchi kudai risiti wanapofanya malipo.
Mwekezaji na aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Madaba, Joseph Mhagama, ambaye ni mmiliki wa kampuni ya SOAGRO, ameomba Serikali imuongezee eneo la uwekezaji katika Kata ya Muhukuru Lilai, Wilaya ya Songea Vijijini, mkoani Ruvuma.
Mhagama alitoa ombi hilo hivi karibuni kwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Kaspar Kaspar Mmuya, aliyefanya ziara ya kikazi katika eneo hilo la uwekezaji.
Mhagama, ambaye kwa sasa anamiliki shamba la mitamba lenye ukubwa wa hekta 1,000 katika eneo la Muhukuru Lilai, ameomba kuongezewa hekta 3,679.7 ili kufikisha jumla ya hekta 4,679.7 kwa ajili ya kupanua uwekezaji wake.
Akizungumza mbele ya Naibu Waziri Mmuya, Mhagama alisema eneo hilo la ziada analoomba litatumika kuendeleza ufugaji wa kisasa wa ng’ombe, mbuzi na kondoo, pamoja na kuanzisha kiwanda cha kuchakata nyama.
“Mheshimiwa Naibu Waziri, ninaomba Serikali iniongezee hekta 3,679.7 kutoka hekta 1,000 nilizonazo sasa. Dhamira yangu ni kuongeza uwekezaji katika sekta ya mifugo na hatimaye kuanzisha kiwanda cha kuchakata nyama hapa hapa Muhukuru Lilai,” alisema Mhagama.
Alisema kiwanda hicho kitakuwa na manufaa kwa wananchi wa Songea Vijijini kwa kuongeza thamani ya mifugo inayozalishwa na wafugaji wa maeneo hayo, huku pia kikiwapatia soko la uhakika.
Mhagama alisema iwapo Serikali itampatia eneo hilo la ziada, atawekeza kikamilifu na kuhakikisha wananchi wa Kata ya Muhukuru Lilai wananufaika moja kwa moja kupitia fursa mbalimbali zitakazotokana na uwekezaji huo.
Alizitaja fursa hizo kuwa ni pamoja na ajira za moja kwa moja shambani na kiwandani, ajira za msimu, mafunzo ya ufugaji bora na wa kisasa, pamoja na kuboresha miundombinu ya kijamii katika kata hiyo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Kaspar Kaspar Mmuya, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika ziara hiyo, alitembelea na kujionea shamba hilo la uwekezaji na kusikiliza maombi ya mwekezaji.
Wananchi wa Muhukuru Lilai waliojitokeza kwa wingi kumlaki Naibu Waziri walimuomba kuishauri Serikali kuridhia ombi la mwekezaji huyo, wakisema uwekezaji huo utachochea maendeleo na kuchangia ukombozi wa kiuchumi, hususan kwa vijana wanaokosa ajira katika eneo hilo.
Watoto wenye mahitaji maalum wilayani Simanjiro, Manyara, wamepatiwa vitimwendo saba vitakavyowasaidia kuwa na uhuru zaidi katika kufanya shughuli zao za kila siku, huku pia vikitumika kupunguza changamoto kwa wazazi na walezi wanaowabeba wanapowapeleka shule na katika shughuli nyingine.
Msaada huo umetolewa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Regina Qwaray, ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Manyara, katika hatua inayolenga kuwawezesha watoto hao kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na kupata elimu kwa urahisi zaidi.
Akizungumza wakati wa kukabidhi vitimwendo hivyo jana, Qwaray amesema watoto wenye mahitaji maalum wanahitaji ushirikiano wa jamii ili waweze kupata elimu, kuendeleza vipaji na uwezo wao, pamoja na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii.
Alisema amekuwa akiwakumbuka watoto hao kila anapopata nafasi ya kuwasaidia, akisisitiza kuwa kuwasaidia watu wenye mahitaji maalum ni sehemu ya kujenga mazingira bora ya kuishi na kushiriki katika jamii.
Kwa mujibu wa Qwaray, vitimwendo hivyo vitasaidia kupunguza changamoto wanazokutana nazo wazazi na walezi ambao wakati mwingine hulazimika kuwabeba watoto wenye ulemavu wanapowapeleka shuleni au katika shughuli mbalimbali.
“Vitimwendo hivi vitasaidia kupunguza mzigo kwa wazazi na walezi ambao wamekuwa wakiwabeba watoto wao wanapokwenda shule na maeneo mengine,” alisema Qwaray.
Aidha, aliwataka watoto waliopokea msaada huo kuvitunza na kuvitumia kwa uangalifu ili viweze kuwasaidia kwa muda mrefu.
Qwaray pia ametoa wito kwa jamii kuacha kuwaficha watoto wenye mahitaji maalum, badala yake kuwapa fursa ya kupata elimu, kushiriki katika shughuli za kijamii na kuendeleza uwezo wao.
Kwa upande wao, madiwani wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) katika Halmashauri ya Simanjiro wamempongeza Qwaray kwa hatua hiyo, huku wakitoa wito kwa viongozi na wadau wengine kuunga mkono juhudi za kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalum.
Baadhi ya wazazi waliopokea msaada huo wamemshukuru Qwaray, wakisema vitimwendo hivyo vitawasaidia watoto wao kuwa na uhuru zaidi wa kushiriki katika shughuli mbalimbali na kupunguza changamoto ya kuwabeba, hasa wanapokwenda shule.
Chama Kikuu cha Ushirika cha Runali Ltd, kinachohudumia wakulima katika Wilaya za Ruangwa, Nachingwea na Liwale, kimeweka mikakati ya kuboresha usimamizi na uendeshaji wa ununuzi na uuzaji wa zao la korosho katika msimu wa 2026/2027.
Mikakati hiyo imejadiliwa katika kikao kazi cha maandalizi ya msimu wa korosho 2026/2027 kilichofanyika katika ukumbi uliopo kwenye jengo la Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, mkoani Lindi.
Kikao hicho kimewakutanisha wadau mbalimbali wanaohusika katika mnyororo wa thamani wa zao la korosho, wakiwemo wawakilishi wa taasisi za fedha, Bodi ya Korosho Tanzania, sekta ya usafirishaji, waendesha maghala, maafisa kilimo, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), mitandao ya simu pamoja na Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Mohamed Hassan Moyo, aliyekuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Adam Kigoma Ali Malima, amewataka wadau wote wanaohusika katika mnyororo wa thamani wa korosho kuwa waadilifu na kuhakikisha wakulima wanahudumiwa ipasavyo.
Moyo amesema ushirikiano na uadilifu wa wadau ni muhimu katika kuhakikisha wakulima wanapata manufaa stahiki kutokana na mazao yao, jambo ambalo litasaidia kuongeza kipato na thamani ya zao la korosho.
“Wadau wote mnaohusika katika mnyororo huu wa thamani mnatakiwa kuwa waadilifu ili kuhakikisha wakulima wanahudumiwa ipasavyo na kupata thamani halisi ya mazao yao,” alisema Moyo.
Kwa upande wake, Mrajisi Msaidizi wa Mkoa wa Lindi, Kenneth Shemdoe, amewataka wadau wote kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na uwajibikaji ili kuhakikisha mchakato wa mauzo ya mazao ya wakulima unasimamiwa kikamilifu.
Shemdoe amesema uwajibikaji wa kila mdau katika hatua mbalimbali za mnyororo wa thamani ni msingi wa kuhakikisha msimu wa korosho unaendeshwa kwa ufanisi na kwa manufaa ya mkulima.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Liwale, Gudluck Mlinga, ametoa onyo kali kwa watu watakaohusika na ununuzi au uuzaji wa korosho zisizokidhi viwango, akisema hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Aidha, amewataka wakulima kuendelea kufuata taratibu bora za kuhifadhi fedha wanazopata kutokana na mauzo ya mazao yao, hususan kutumia huduma za benki, ili kuepuka matumizi holela na yasiyo na tija.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Runali Ltd, Odas Mpunga, amewataka wadau wote kuwa waadilifu katika msimu wa mauzo ya korosho wa 2026/2027, akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha wakulima wanapata malipo yao kwa wakati.
Mpunga amesema Runali Ltd itaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha upatikanaji wa vifungashio, uhifadhi na ulinzi wa ubora wa korosho, pamoja na kuimarisha mifumo ya usimamizi wa mauzo ya mazao ya wakulima.
Amesema hatua hizo ni muhimu katika kuhakikisha mnyororo mzima wa thamani wa zao la korosho unaendeshwa kwa ufanisi na bila changamoto, huku mkulima akiwa mnufaika mkuu wa shughuli za biashara ya zao hilo.
Kikao hicho ni sehemu ya maandalizi ya Runali Ltd kuhakikisha msimu wa korosho 2026/2027 unaendeshwa kwa uwazi, uwajibikaji na uadilifu, kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa, kwa lengo la kuongeza tija na kipato kwa wakulima wa korosho katika Wilaya za Ruangwa, Nachingwea na Liwale.
Serikali imewataka wadau wanaosimamia programu ya mikopo kwa kampuni changa za TEHAMA kuhakikisha Sh bilioni tano zilizotengwa kuwawezesha vijana zinatumika kwa ufanisi na kuleta matokeo yanayoweza kupimika.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, ametoa wito huo hivi karibuni jijini Dodoma wakati akizindua programu inayolenga kuongeza uwezo wa kampuni changa kupata mitaji kwa ajili ya kukuza biashara na ubunifu.
Kairuki alisema utekelezaji wa programu hiyo unapaswa kuangalia zaidi matokeo yatakayopatikana kwa wanufaika, ikiwemo ukuaji wa kampuni, uundaji wa ajira, ongezeko la mauzo na mapato, upanuzi wa masoko pamoja na urejeshaji wa mikopo.
Alisema mikopo hiyo itatolewa kwa makundi matatu kulingana na mahitaji ya biashara. Kiwango cha kwanza ni kuanzia Sh milioni moja hadi Sh milioni 25, cha pili ni zaidi ya Sh milioni 25 hadi Sh milioni 100, na kiwango cha juu ni zaidi ya Sh milioni 100 hadi Sh milioni 500.
Katika hatua nyingine, Kairuki aliitaka Tume ya TEHAMA kukamilisha mwongozo utakaowezesha kampuni changa za TEHAMA kushiriki katika zabuni za Serikali na kuuwasilisha kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kwa hatua zinazofuata.
Aidha, aliziagiza Wizara, Tume ya TEHAMA na Benki ya Azania kuweka mfumo maalumu wa kufuatilia matokeo ya programu hiyo, ikiwemo maendeleo ya kampuni zitakazonufaika na namna zitakavyotumia fedha hizo.
Kwa upande wa kampuni zinazolengwa, Waziri huyo amewataka wabunifu kujisajili kupitia Mfumo wa Jamii Hunt, ambao umetajwa kuwa njia rasmi ya utambuzi na uwasilishaji wa maombi ya programu hiyo.
Pia, amewataka wabunifu kuangalia uwezekano wa kuunda umoja rasmi kwa kuzingatia sheria na taratibu, akisema hatua hiyo inaweza kurahisisha uwakilishi wao na kusaidia kutambua changamoto pamoja na mahitaji yao.
Kairuki alisisitiza umuhimu wa kuwepo kwa mpango wa kutoa elimu kwa umma ili kampuni changa na wabunifu waelewe vigezo vya kupata mikopo, namna ya kuomba, wajibu wa wanufaika na manufaa yanayotarajiwa kutokana na programu hiyo.
Alisema wanufaika wanapaswa kutumia fedha hizo kwa madhumuni yaliyokusudiwa, kukuza biashara zao na kutafuta masoko ya ndani na nje ya Tanzania ili kuongeza mchango wa kampuni changa katika sekta ya TEHAMA.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Azania, Dkt. Esther Mang’enya, alisema benki hiyo itashirikiana na Wizara katika kufanya tathmini na kutoa mikopo kwa kampuni zitakazokidhi vigezo vilivyowekwa.
Alisema pamoja na fedha, kampuni zitakazonufaika zitapatiwa pia ujuzi kuhusu usimamizi wa fedha, utunzaji wa kumbukumbu na uandaaji wa mipango ya biashara, hatua inayolenga kusaidia kujenga kampuni zenye uwezo wa kukua, kuendelea na kuzalisha ajira.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waanzilishi wa Biashara Bunifu Tanzania (TSA), Zahoro Muhaji, ambaye pia alizungumza kwa niaba ya chama hicho upande wa Zanzibar, aliwataka wanufaika kutumia mikopo hiyo kwa malengo yaliyokusudiwa na kuhakikisha inarejeshwa ili kuwawezesha wabunifu wengine kunufaika.
Alisema matumizi yenye tija na urejeshaji wa mikopo ni miongoni mwa mambo yatakayosaidia kujenga uaminifu na kuwezesha fursa zaidi za uwekezaji katika sekta ya TEHAMA.
Asubuhi inaanza kama kawaida. Mtu anaamka, anaoga, anakunywa chai na kujiandaa kwenda kazini. Kwa nje, kila kitu kinaonekana sawa.
Lakini ndani ya mwili wake kunaweza kuwa kunaendelea jambo ambalo hajui. Huenda ni shinikizo la damu, kisukari au ugonjwa mwingine sugu ambao bado haujaonyesha dalili kubwa.
Anaendelea na maisha yake ya kila siku, siku moja baada ya nyingine.
Hii ndiyo sehemu ya kutisha kuhusu magonjwa yasiyoambukiza. Mara nyingi hayaji kwa kishindo. Hayana mlipuko unaoonekana wala taharuki inayowafanya watu kukimbilia mitaani. Huja taratibu, wakati mwingine bila dalili, hadi madhara yake yanapoanza kuonekana.
Na Afrika inaanza kuhisi uzito wa tishio hilo.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), magonjwa yasiyoambukiza yalichangia asilimia 37 ya vifo katika Kanda ya Afrika mwaka 2019, kutoka asilimia 24 mwaka 2000. Takribani asilimia 64 ya vifo hivyo vilitokea kabla ya mtu kufikisha umri wa miaka 70.
Hizi si namba tu.
Nyuma ya kila asilimia kuna mtu. Kuna familia inayoweza kumpoteza mzazi, mtoto anayehitaji matibabu ya muda mrefu au mfanyakazi anayelazimika kupunguza shughuli zake kutokana na ugonjwa.
Magonjwa kama saratani, kisukari, magonjwa ya moyo na magonjwa sugu ya mfumo wa upumuaji yanaweza kuhitaji matibabu na ufuatiliaji wa muda mrefu.
Kwa baadhi ya wagonjwa, safari ya afya si ya wiki moja wala mwezi mmoja; inaweza kuwa safari ya miaka na miaka.
Ugonjwa Unapokuja Kimya
Changamoto nyingine ni kwamba baadhi ya magonjwa haya yanaweza kuendelea bila dalili zinazoonekana wazi. Mtu anaweza kuendelea kufanya kazi, kulea familia na kushiriki shughuli za kila siku bila kujua kuwa afya yake iko hatarini.
Ndiyo maana uchunguzi wa mapema na wa mara kwa mara una umuhimu mkubwa. Tatizo linapogunduliwa mapema, mgonjwa anaweza kuanza matibabu na ufuatiliaji kabla hali haijawa mbaya zaidi.
Lakini kwa mtu anayeishi mbali na kituo cha afya chenye huduma zinazohitajika, hata kupata uchunguzi huo kunaweza kuwa changamoto.
Hapo ndipo umbali unapoanza kuwa sehemu ya tatizo.
Mjadala wa Kusogeza Huduma Karibu na Wananchi
Mjadala huo ulipewa uzito wakati Dar es Salaam ilipokuwa mwenyeji wa Mkutano wa Tatu wa Kimataifa wa PEN-Plus Barani Afrika, uliofanyika Juni 23 hadi 25, 2026.
Mkutano huo uliwaleta pamoja wataalamu wa afya, watunga sera na wadau mbalimbali kujadili namna ya kuimarisha huduma kwa watu wenye magonjwa yasiyoambukiza sugu na makali.
Katika mjadala huo, Prof. Mohamed Yakub Janabi, Mkurugenzi wa Kanda wa WHO kwa Afrika, alisisitiza kwamba mjadala wa afya haupaswi kuishia kwenye majengo na fedha pekee.
“Afya si kuhusu majengo wala bajeti. Ni kuhusu watu. Ni kuhusu utu, na ni kuhusu haki,” alisema Prof. Janabi.
Kauli hiyo inaweka sura ya mwanadamu katikati ya mjadala ambao mara nyingi hujaa takwimu, sera na mipango.
Kwa sababu mwisho wa siku, lengo la kujenga hospitali, kununua vifaa au kuongeza bajeti si majengo yenyewe. Ni kuhakikisha mtu anayehitaji huduma anaweza kuipata.
Hilo ndilo wazo linalosukumwa na mkakati wa PEN-Plus—kusogeza huduma za magonjwa sugu na makali kutoka kutegemea hospitali kubwa pekee na kuziimarisha katika vituo vya ngazi za chini, hasa maeneo ya vijijini na yaliyo mbali na huduma za rufaa.
Hospitali Inapokuwa Mbali
Fikiria mgonjwa anayeishi eneo la mbali na hospitali kubwa.
Anahitaji kipimo. Anahitaji dawa. Anahitaji kumuona daktari tena. Na baada ya wiki au mwezi, anahitaji kurudi kwa ufuatiliaji.
Kwa mtu wa mjini, safari hiyo inaweza kuonekana kuwa ya kawaida. Kwa mwingine, inaweza kumaanisha kutumia siku nzima kusafiri, kugharamia usafiri na chakula akiwa njiani, na wakati mwingine kulipia malazi.
Ndiyo maana upatikanaji wa huduma hauwezi kupimwa kwa kuuliza tu kama hospitali ipo.
Swali muhimu zaidi ni: Je, mgonjwa anaweza kuifikia?
Mkutano wa PEN-Plus ulisisitiza umuhimu wa utambuzi wa mapema, uchunguzi, matibabu na huduma za muda mrefu katika ngazi mbalimbali za mfumo wa afya, kwa msisitizo wa huduma za msingi na vituo vya kwanza vya rufaa.
Mapambano Hayaanzii Hospitalini
Lakini hadithi ya magonjwa yasiyoambukiza haiishii hospitalini.
Inaweza kuanzia kwenye kile kilicho kwenye sahani ya mtu. Inaweza kuhusishwa na kutofanya mazoezi, matumizi ya tumbaku na pombe, pamoja na vihatarishi vingine vya kiafya.
Hivyo, wakati hospitali zinaendelea kuhudumia wagonjwa wanaohitaji matibabu, jamii nayo ina nafasi muhimu katika kuzuia baadhi ya magonjwa hayo.
Elimu ya afya, uchunguzi wa mara kwa mara na kugundua ugonjwa mapema vinaweza kumsaidia mtu kuchukua hatua kabla tatizo halijawa kubwa.
Kwa hiyo, mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza yana sura mbili: kumsaidia yule ambaye tayari ni mgonjwa na kuzuia wengine wasifike katika hatua hiyo.
Tishio Lisilo na Kelele
Magonjwa yasiyoambukiza yanaendelea kubadilisha sura ya changamoto za afya barani Afrika. Hayahitaji tu dawa na madaktari. Yanahitaji mifumo inayomfikia mwananchi, taarifa sahihi za afya na huduma zinazopatikana kwa wakati.
Na pengine hapo ndipo maana ya maneno ya Prof. Janabi inapokuwa wazi zaidi.
Afya si majengo pekee. Si bajeti pekee.
Ni mtu anayesubiri huduma. Ni familia inayohitaji mzazi wake awe na afya. Ni mgonjwa anayehitaji dawa bila kusafiri mamia ya kilomita. Na ni jamii inayohitaji kujua tatizo kabla halijawa kubwa.
Kwa sababu magonjwa haya yanaweza kuja bila kelele.
Lakini athari zake zinaweza kusikika katika maisha ya mtu, familia yake na jamii nzima.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limewakamata Razaki Makolo na Luka Dotto, wakazi wa Mabatini, Wilaya ya Chunya, kwa tuhuma za kumuua Sira John (20) kwa kumchoma kwa kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali za mwili.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, SACP Benjamin Kuzaga, tukio hilo lilitokea Septemba 30, 2026, katika Kitongoji cha Mabatini, Kata ya Chokaa, baada ya marehemu na watuhumiwa kudaiwa kunywa pombe pamoja na kisha kutokea ugomvi.
Inadaiwa kuwa baada ya kuondoka katika kilabu hicho, Sira alikutana na watuhumiwa akiwa njiani kuelekea kambini alipokuwa akifanyia kazi. Watuhumiwa hao wanadaiwa kumvizia na kumchoma sehemu mbalimbali za mwili, hali iliyosababisha kifo chake.
Kamanda Kuzaga amesema Polisi, kupitia Kikosi Maalum cha Kupambana na Mauaji, ilifanya ufuatiliaji na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao.
Katika misako na operesheni zilizofanyika mwezi Septemba, Polisi pia iliwakamata watuhumiwa 29 waliokuwa na jumla ya kilo 13.816 za bangi, watuhumiwa wanane waliokuwa na lita 90 za gongo, watuhumiwa 15 waliokuwa na bidhaa za magendo zenye thamani ya Sh milioni 3.3, pamoja na mtuhumiwa mmoja aliyekuwa na silaha aina ya gobore bila kibali.