• Na Vincent Mpepo

    Wadahiliwa wa Shahada za Uzamili na Uzamivu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania Mkoa wa Dar es salaam wameelezea mipango na mikakati yao binafsi ili kuhakikisha wanamaliza masomo yao kwa wakati na kwa mafanikio.

    Wakizungumza na mwandishi wetu katika mahojiano, wadahiliwa hao  walionesha kufurahia mafunzo elekekezi yaliyotolewa na chuo hicho kwani yamewafungua kuona namna ya usomaji chuoni hapo.

    Mwanaidi Salim, mdahiliwa wa Shahada ya Uzamili katika Eilimu, Sera na Mipango alisema mafunzo elekezi aliyoyapata yamemsaidia kutambua mifumo ya kujifuza na kujifunzia huku akidai kuwa vitu vingi vimerahishishwa.

    “Kila kitu kipo mtandaoni kuanzia masomo na sehemu ya kuhifadhi taarifa za malipo”, alisema Mwanaidi.

    Alisema wameelekezwa kuwatambua waratibu wa programu ambao ndio waongoza njia katika safari yao ya masomo kwa kuwa wana taarifa muhimu katika programu wasomazo.

    Kwa upande wake, Beatus Kamugisha mdahiliwa wa Shahada ya Uzamili ya Usimamizi wa Maktaba na Habari alisema amejipanga vyema kuanza masomo na kwamba mafunzo elekekezi yamemsaidia kujua namna ya kusoma hususani kwa mfumo wa elimu huria na masafa ambao nyezo yake kuu ni mtandao.

    “Tumefundishwa mifumo ya kusomea, matumizi ya programu tumizi kama vile Zoom na namna ya kutoa mrejesho kwa walimu kwa kazi za darasani”, alisema Kamugisha.

    Mdahiliwa wa Shahada ya Uzamivu katika masuala ya kibenki na mifumo ya malipo katika Kitivo cha Usiamizi wa Biashara, William Fidelis alisema mafunzo elekezi n muhimu lakini kuna sehemu ya wajibu kati ya mwanafunzi na msimamizi wa utafiti.

    “Mafunzo elekezi yametoa matumaini na mwanga kwa wadahiliwa hususani sisi ambao ni watu wazima kwa kuwa tumepata miongozo itakayotusaidia kuenenda katika safari ya masomo”, alisema William.

    Alisema elimu ya utu uzima ina changamoto hususani elimu  huria na masafa ambayo mwanafunzi anasoma kwa namna ya kutokakaa darasani ambapo atatakiwa kuwa makini zaidi ili aendane na matakwa ya asomeacho kwa miongozo iliyopo.

    “Uthabiti na usaidizi wa msimamizi kwa mwanafunzi ndio kitu muhimu ili kuhakikisha kuwa hakuna anayemfelisha mwingine”, alisema William.

    Mratibu wa Idara Usimamizi na Kumbukumbu wa Kurugenzi ya Masomo ya juu chuoni hapo, Mhadhiri Mary Ogondiek alielezea wajibu wa mwanafunzi na msimamizi katika mchakato wa utafiti huku akiwataka wanafunzi kujenga utaratibu wa mawasiliano ya mara kwa mara na wasimamizi wao.

  • Na Mack Francis-Arusha ‎ ‎

    Mwanamuziki maarufu wa Bongo Fleva na mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulazizi Abubakari Chende almaarufu Dogo Janja, ameibuka mshindi wa kura za maoni na kutangazwa rasmi kuwa mgombea udiwani wa CCM katika Kata ya Ngarenaro, jijini Arusha. ‎ ‎

    Katika uchaguzi huo wa ndani wa chama uliofanyika hivi karibuni, Dogo Janja amepata ushindi wa kishindo kwa kura 76, akimshinda aliyekuwa Diwani wa Kata hiyo, Isaya Doita, ambaye alipata kura 60, huku Benjamin Mboyo akipata kura 2 pekee. ‎ ‎

    Kura hizo zilihesabiwa mbele ya wasimamizi wa uchaguzi wa CCM, Sophia Islam na Rajab Mwaliko, waliothibitisha kuwa uchaguzi ulikuwa huru na wa haki. ‎ ‎Ushindi huo unamuweka Dogo Janja kwenye nafasi ya kugombea rasmi nafasi ya Udiwani wa Kata ya Ngarenaro katika Uchaguzi Mkuu wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.

  • Na Mack Francis – Arusha ‎ ‎

    Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, amezitaka nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuweka mikakati ya pamoja ya kupambana na rushwa.

    Majaliwa alitoa wito huo hivi karibuni 2025 Jijini Arusha wakati akimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, katika ufunguzi wa warsha ya kikanda kwa viongozi wa taasisi za kupambana na rushwa kwa nchi za SADC iliyofanyika Jiji humo kwa siku Mbili. ‎

    ‎Katika hotuba yake, Waziri Mkuu alisema mapambano dhidi ya rushwa hayawezi kufanikiwa bila ushirikishwaji wa wadau mbalimbali wakiwemo sekta binafsi, taasisi za dini na vyombo vya habari, akisisitiza kuwa ushirikiano huo ni muhimu kwa kudhibiti mizizi ya rushwa.

  • Na Mack Francis-Arusha ‎ ‎

    Serikali imetoa shilingi bilioni 139 kwa mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara kwa ajili ya kuwezesha utekelezaji wa miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji, ikiwa ni jitihada za kuwaondoa wakulima kwenye kilimo cha kutegemea mvua. ‎

    Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga aliyaema hayo wakati akifungua Maonesho ya 31 ya Kilimo na Ufugaji Kanda ya Kaskazini, yanayoendelea katika viwanja vya Themi, mkoani Arusha, Agosti 5, 2025. ‎ ‎

    Alieleza kuwa sehemu ya fedha hizo ni matokeo ya ongezeko la bajeti ya taifa kwa ajili ya umwagiliaji, ambapo imeongezeka kutoka bilioni 46 mwaka 2021/2022 hadi kufikia bilioni 403.

    “Ongezeko hilo limechangia kuzalishwa kwa mazao mbalimbali nchini kwa wingi, hivyo kuongeza usalama wa chakula na mauzo ya bidhaa za kilimo nje ya nchi”, alisema Sendiga.

  • Na Mack Francis, Arusha

    ‎‎Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Kenani Kihongosi na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Marianne Louise Young wamekubnaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta ya afya na utalii mkoani Arusha.

    ‎‎Mazungumzo hayo yalifanyika hivi karibuni wakati Balozi Young akiwa ziarani mkoani humo, akiambatana na Mkuu wa Diplomasia ya Uchumi wa Ubalozi wa Uingereza nchini, Bi. Tammy Clayton.

    Ujumbe huo wa Balozo wa Uingereza ulitemebelea na kukagua miradi mbalimbali inayofadhiliwa na Serikali ya Uingereza pamoja na kukutana na wawekezaji kutoka Uingereza waliopo Kanda ya Kaskazini, hususani katika sekta ya utalii.

    ‎‎Kihongosi alisema Mkoa wa Arusha unaendelea kuimarika katika miundombinu ya usafiri na utoaji wa huduma muhimu kwa wageni na watalii akisisitiza kuwa usalama na amani ni mambo yaliyotamalaki mkoani humo.

    “Kwa sasa kupitia Programu ya TACTIC, tunaanza ujenzi wa zaidi ya kilomita 30 za barabara ndani ya jiji na katika maeneo ya hifadhi ya Ngorongoro ili kuboresha upatikanaji wa huduma na kurahisisha shughuli za utalii katika misimu yote ya mwaka”, alisema RC Kihingosi,

    ‎‎Aidha, Mkuu huyo wa mkoa alisema ofisi yake iko wazi kwa kushirikiana na wadau wote wa maendeleo wakiwemo wawekezaji na wageni, kwa lengo la kuboresha mazingira ya biashara na kuvutia watalii zaidi.

    ‎‎Balozi Young alipongeza jitihada za mkoa wa Arusha katika kukuza utalii na huduma za kijamii, huku akionesha utayari wa kuendelea kushirikiana na serikali ya mkoa katika maeneo mapya ya uwekezaji.

    Alisema takribani watalii 80,000 kutoka Uingereza walitembelea Tanzania mwaka 2024, wengi wao wakifika Arusha na Zanzibar.

    ‎‎Balozi Young pia ametangaza mpango wake wa kurejea Arusha wiki ijayo pamoja na familia yake kwa ajili ya kusherehekea siku yake ya kuzaliwa ndani ya hifadhi ya Ngorongoro akieleza furaha yake juu ya mandhari na vivutio vya kipekee vya utalii vilivyopo mkoani humo.

    ‎‎Mhe. Kihongosi kwa upande wake alimhakikishia Balozi Young kuwa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025 hautaathiri shughuli za utalii, huku akitoa wito kwa wageni wa ndani na nje ya nchi kuendelea kutembelea mkoa wa Arusha kutokana na  uwepo wa vivutio vya utalii vyenye upekee.

  • Na Cartace Ngajiro

    Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Pinda amewaasa wafanyabiashara wa mazao ya kilimo nchini kutumia Bandari ya Tanga kusafirsha mazao yao kwenda kwenye Soko la Kimataifa.

    Pinda aliyasema hayo wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya Nanenae Kanda ya Mashariki 2025, yanayojumuisha Mikoa minne Tanga, Dar es Salama, Pwani na Morogoro yanayofanyika katika Uwanja wa Mwalimu JK Nyerere maarufu kama ‘Viwanja vya NaneNane’

    “Bandari ya Tanga inatupa heshima sana katika nchi yetu  hivyo natoa  rai kwa  wafanyabiashara  wa mazao ya kilimo nchini kutumia Bandari hiyo ambayo imeboresha huduma zake” aliongeza Mhe Pinda

    Aidha alitoa wito kwa Shirika la Reli la Tanzania (TRC) na Bandari ya Tanga kuendelea kushirikiana  ili kupanua wigo katika utoaji wa huduma katika sekta ya usafirishaji chini kanda ya mashariki.

    Maonesho ya NaneNane Kanda ya Mashariki, 2025   yanayoshirikisha taasisi za umma na binafsi na Bandari ya Tanga ni mshiriki wa maonesho hayo yenye kauli mbiu ya ‘Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi 2025’

  • Na Mack Francis

    ‎Zaidi ya vijana na viongozi wa mila wapatao elfu kumi kutoka jamii ya kifugaji ya Kimasai wamekusanyika katika viwanja vya Elerai, jijini Arusha, kutoa adhabu ya kimila kwa vijana wawili waliokiri kutumia lugha chafu dhidi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan, kupitia video iliyosambazwa mitandaoni.

    ‎‎Vijana hao, waliotambulika kwa majina ya Laurence Kuesoy na David Zakayo, wote wakazi wa Arusha, walijitokeza hadharani na kuomba radhi mbele ya umati mkubwa, wakielekeza msamaha wao kwa Rais Samia mbele ya wazee wa mila katika eneo la kimila la Elerai ambapo kila mmoja alitakiwa kulipa faini ya dume la ng’ombe kama njia ya kutubu na kurudisha heshima ya jamii.

    ‎‎Kwa mujibu wa viongozi wa kimila wa jamii ya Kimasai wakiongozwa na Laigwanani Mkuu, Isack Ole Kissongo, walieleza kuwa wamechukizwa sana na maudhui ya video iliyorekodiwa na vijana hao tarehe 20 Juni 2025, katika eneo hilo la kimila wakati wakifanya shughuli za usafi na kisha kuiweka kwenye mitandao ya kijamii ikiwa na maudhui yasiyofaa kwa kiongozi wa nchi.‎

    ‎Laigwanani Kissongo alisisitiza kuwa jamii ya Kimasai haikubaliani na tabia ya matusi kwa viongozi wa kitaifa, na kwamba hatua hiyo ya kutoa faini ni ya kimila, inayolenga kudumisha maadili, nidhamu na heshima kwa viongozi wa taifa.‎

    ‎Kulingana na hayo viongozi wa kimila waliomba radhi kwa niaba ya jamii ya Kimasai kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kumhakikishia Rais Samia kuwa jamii hiyo itaendelea kuwa mstari wa mbele katika kuimarisha nidhamu, amani, na heshima kwa viongozi wa kitaifa.

    ‎‎Katika hatua nyingine, Laigwanani Mkuu Isack Ole Kissongo aliiomba serikali kuhakikisha kuwa eneo la kimila la Elerai lenye zaidi ya ekari 100, lililopo Kata ya Elerai, Mtaa wa Majengo, halivamiwi wala kugawanywa kiholela, kwa kuwa lina umuhimu mkubwa kwa shughuli za mila na utamaduni wa jamii hiyo.

  • Na Tabia Mchakama, Dar es salaam

    Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) jana wameingia kwenye makubaliano rasmi ya ushirikiano wa kimkakati kwa lengo la kukuza na kupanua sekta ya fedha nchini.

    Makubaliano hayo yalisainiwa jijini Dar es Salaam kati ya Kamishna wa Bima, Dkt. Baghayo Saqware na Mkurugenzi Mtendaji wa DSE, Peter Nalitolela yakilenga kushirikiana katika maeneo manne ya msingi, ikiwemo utoaji wa mafunzo, kuboresha uelewa wa umma juu ya bidhaa za kifedha, kukuza masoko ya mitaji na kuimarisha ujumuishaji wa kifedha.

    Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini, Kamishna wa Bima Dkt. Saqware alisema ushirikiano huo utafungua fursa zaidi kwa kampuni za bima nchini kuongeza mtaji wao kupitia masoko ya mitaji ikiwemo utoaji wa hati fungani na mauzo ya hisa kwa umma.

    “Masoko ya bima yana uhusiano wa karibu na masoko ya mitaji. Kwa kuunganisha nguvu, taasisi zetu zitasaidia kuwezesha kampuni za bima kutumia fursa zilizopo katika soko la hisa ili kuimarisha uwezo wao wa kifedha,” alisema Dkt. Saqware.

    Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa DSE, Peter Nalitolela, alieleza kuwa makubaliano hayo ni hatua muhimu katika kuleta mapinduzi ya kifedha nchini hususan katika kutoa elimu kwa umma kuhusu bidhaa za bima na uwekezaji, pamoja na kuunga mkono juhudi za serikali za kuongeza ushiriki wa wananchi katika sekta rasmi za kifedha.

    “Tunatarajia kuona ongezeko la uelewa kwa umma kuhusu huduma za kifedha, na kwa pamoja tutachangia katika kujenga uchumi jumuishi unaowanufaisha watanzania wote,” alisema Nalitolela.

    Makubaliano haya yanatajwa kuwa hatua ya kimkakati katika kufungua fursa mpya kwa taasisi za fedha nchini na kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha kwa makundi mbalimbali ya Wananchi katika kuimarisha mazingira rafiki ya uwekezaji ndani ya Tanzania.