
Na Vincent Mpepo
Watanzania wanaosafiri kuelekea maeneo mbalimbali nchini, hususan washarika wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), wametakiwa kuwa waangalifu nyakati za mwisho wa mwaka kutokana na changamoto mbalimbali za usafiri.
Wito huo umetolewa na Mwinjilisti Kiongozi wa Mtaa wa Kwembe, Emeline Mnzava, jana wakati wa ibada ya Siku ya Nne ya Majilio iliyofanyika katika mtaa huo. Alisisitiza umuhimu wa wanaosafiri kubeba nyaraka au cheti cha utambulisho kinachoonyesha wanakotoka ili kurahisisha upatikanaji wa msaada popote watakapokwenda.
“Ni muhimu sana kuchukua cheti cha utambulisho wa safari kwa kuwa kitakusaidia kupata msaada wowote utakapohitajika,” alisema Mwinjilisti Mnzava.
Aidha, aliwataka washarika wa mtaa huo kuendelea kuimba na kumtukuza Mungu hata pale ambapo vyombo vya muziki havifanyi kazi, akisisitiza kuwa Walutheri wana nyimbo zao zinazoweza kuimbwa bila kuhitaji vyombo vya muziki.
Akihubiri katika ibada hiyo, Mtendakazi wa Mtaa huo, Anna Mauki, alizungumzia umuhimu wa jamii kuwajali wahitaji, hususan katika kipindi cha sikukuu za mwisho wa mwaka ikiwemo Krismasi na Mwaka Mpya, kama sehemu ya kutekeleza maandiko kwa vitendo.

Alisema maandiko yanahimiza matengenezo ya mioyo na kuhudumiana, na kwamba ili kuishi kulingana na neno la Mungu, kuna ulazima wa wanajamii ikiwemo Wakristo kuwakumbuka wahitaji kama vile wajane, yatima na watu wenye mahitaji maalumu.
Anna alieleza kuwa matengenezo ya kiroho wakati wa Majilio yanapaswa kwenda sambamba na maandalizi ya kimwili, ikiwemo kuwajali na kuwakumbuka wenye mahitaji katika jamii, akisisitiza kuanza katika familia na kwa majirani.
“Hakuna asiyejua maana ya Noeli kutokana na maandalizi ya kimwili yanayofanyika kila mwaka,” alisema.
Aliongeza kuwa pamoja na maandalizi hayo, sikukuu yoyote huwa na maana zaidi endapo watu wote wana afya njema. “Unaweza kuwa na kila kitu, lakini ukawekewa masharti ya kula au kutokula vitu fulani kutokana na afya,” alisisitiza.
Pia aliwakumbusha Wakristo kufanya tathmini ya mahusiano yao na Mungu kwa kipindi cha mwaka mzima ili kubaini mwenendo wao katika masuala mbalimbali, ikiwemo utekelezaji wa ahadi na huduma katika nafasi walizonazo, iwe ni mtu binafsi au katika vikundi kama kwaya.
“Kutotunza ahadi, ikiwemo kutofanya mazoezi, wakati mwingine kunatukosesha baraka,” alisema Mtendakazi Anna.
Mwisho, aliwapongeza washarika wa mtaa huo, hususan wanawake, kwa mchango wao mkubwa katika utunzaji wa mazingira ya kanisa.

Leave a reply to GODWIN AKYOO Cancel reply