Na Mwandishi Wetu

Wananchi 268 wamefanyiwa upasuaji wa macho bure, huku wengine 1,345 wakipatiwa miwani ya kusomea bila malipo katika Kituo cha Afya Ikwiriri, Wilaya ya Rufiji, mkoani Pwani, kupitia kambi maalumu ya uchunguzi na matibabu ya macho iliyolenga kusogeza huduma hizo karibu na wananchi.

Kambi hiyo iliyoandaliwa na Lions Club DSM Host kwa kushirikiana na Majey Foundation, pia imewezesha wagonjwa 2,338 kupata huduma za matibabu ya macho kwa njia ya wagonjwa wa nje, pamoja na huduma za uchunguzi na dawa.

Akizungumza na waandishi wa habari, Daktari Bingwa wa Macho kutoka Majey Foundation, Dk. Majala Majala, alisema huduma hizo zilitolewa bure kwa siku tatu na kambi hiyo ilihitimishwa Oktoba 18, 2026.

“Tumekuwa na huduma za uchunguzi wa macho, ugawaji wa dawa na miwani, pamoja na upasuaji bure. Tumeshafanya upasuaji wa wagonjwa 268, tumegawa miwani 1,345 na kwa wagonjwa wa nje tumewahudumia 2,338,” alisema Dk. Majala.

Alisema taasisi hizo zimekuwa zikiendesha kambi za aina hiyo katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuwasaidia wananchi wenye changamoto za macho kupata uchunguzi na matibabu bila kikwazo cha gharama.

Aliongeza kuwa baada ya kumaliza huduma Rufiji, wanatarajia kuelekea Simiyu, Chanika na Mwanza kwa ajili ya kuendesha kambi nyingine, huku akiwahimiza wananchi kujitokeza kupata vipimo na matibabu pindi wanapopata taarifa za huduma hizo.

Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya Ikwiriri, Dk. Jumanne Mapande, alishukuru waandaaji wa kambi hiyo kwa kuwasaidia wananchi waliokuwa na uhitaji wa huduma za matibabu ya macho.

Alisema baadhi ya wagonjwa wamekuwa wakishindwa kupata huduma za madaktari bingwa katika hospitali kubwa kutokana na changamoto za kifedha, hivyo kambi hiyo imewapa fursa ya kupata huduma walizokuwa wakizihitaji bila malipo.

Dk. Mapande aliomba kambi hizo ziwe zinafanyika mara kwa mara ili kuwasaidia wananchi wenye kipato cha chini ambao wanakabiliwa na changamoto ya gharama za kufuata huduma za kibingwa.

Kwa upande wao, baadhi ya wananchi walionufaika na huduma hizo walieleza kufurahishwa na uwepo wa kambi hiyo kwa kuwa imewawezesha kupata matibabu karibu na makazi yao bila gharama.

Kasimu Yassini, mmoja wa wagonjwa waliopata huduma, aliishukuru Serikali kwa kuunga mkono juhudi za kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.

Naye Yusra Mitume, mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Samia Suluhu Hassan, alisema kambi hiyo imemsaidia kupata dawa za macho kwa ajili ya kutibu changamoto iliyokuwa ikimsumbua kwa muda mrefu.

Posted in

Leave a Reply