
Na Cartace Ngajiro – Tanga
Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imewekeza shilingi bilioni 429.1 katika Mradi wa Uboreshaji wa Bandari ya Tanga, uliotekelezwa kuanzia mwaka 2019 hadi 2023, hatua iliyoboresha miundombinu, kuongeza ufanisi wa uendeshaji na uwezo wa bandari kuhudumia meli na shehena mbalimbali.
Uwekezaji huo umewezesha meli kutia nanga moja kwa moja kwenye gati, pamoja na upatikanaji wa mitambo na vifaa 16 vya kisasa, hatua inayochochea ukuaji wa shughuli za kibiashara na kuongeza ushindani wa bandari hiyo.
Mabalozi wa Umoja wa Ulaya walifanya ziara katika Bandari hiyo kwa lengo la kujifunza shughuli za uendeshaji, kufahamu mafanikio yaliyopatikana, mipango ya maendeleo pamoja na fursa za uwekezaji zilizopo.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Meneja wa Bandari ya Tanga, Salehe Mbega, aliesema maboresho yaliyofanywa na Serikali kupitia TPA yameiwezesha bandari hiyo kuimarisha huduma na kuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kuhudumia meli na shehena mbalimbali.
Alisema TPA ina mpango wa muda mrefu wa kuendeleza eneo la Mwambani lenye ukubwa wa hekta 174, ambapo wawekezaji wa sekta binafsi wanakaribishwa kuwekeza ili kuongeza uwezo wa Bandari ya Tanga kuhudumia shehena zinazoongezeka.
Mbega alisema Bandari ya Tanga ina fursa kubwa ya kuhudumia masoko ya ndani na nchi jirani, huku ikiendelea na mikakati ya kuvutia meli za makontena kufanya safari za moja kwa moja kupitia bandari hiyo.
Ziara hiyo imehitimishwa kwa mabalozi hao kupongeza uongozi wa Bandari ya Tanga kwa kueleza maendeleo, mafanikio na fursa za uwekezaji zilizopo, huku wakieleza kufurahishwa na ziara hiyo pamoja na kujionea shughuli za uendeshaji wa bandari.


Leave a Reply